Mudathir afungiwa mechi tatu, kuikosa Simba
Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya, amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni. Picha na Yanga
Muktasari:
- Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya Yanga na Simba ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya atakosekana katika mechi baina ya timu yake na Simba, Mei 3, 2026 kutokana na kutumikia adhabu.
Mchezaji huyo amepewa adhabu ya kufungiwa mechi tatu na faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumpiga kiwiko Ibrahim Abraham wa Pamba Jiji katika mechi baina ya timu hizo Aprili 8, 2026.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania leo, imefafanua kwamba Mudathir amepewa adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu msimu huu.
Kanuni hiyo inafafanua kwamba adhabu kwa kosa la kupiga ni kifungo kisichopungua mechi tatu, na faini ya fedha.
Simba imetozwa faini ya Sh15 milioni kwa makosa mawili iliyofanya katika mechi dhidi ya TRA United na Azam FC.
Kosa lililofanywa na Simba katika mechi dhidi ya TRA United ni walinzi wake kupigana na wale wa timu pinzani ambapo timu zote mbili zimetozwa Sh5 milioni.
Simba pia imetozwa Sh10 milioni kwa kosa la mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili katika mchezo dhidi ya Azam FC.
Katika adhabu hizo zilizotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya TPLB, Singida Black Star imetozwa Sh5 milioni kwa kosa la viongozi wake wawili kujihusisha na imani za kishirikina katika mchezo dhidi ya TRA United.
Coastal Union imetozwa Sh5 milioni kwa kosa la mashabiki wake kurusha chupa za maji kwa refa wa kati na msaidizi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Azam FC imetozwa Sh5 milioni kwa kutotumia mlango sahihi katika mechi dhidi ya Simba.