Chama aingia kwenye mifumo mitatu Yanga

Muktasari:

  • Chama alitangazwa na Yanga leo asubuhi baada ya mkataba wake na Simba kumalizika jana baada ya juhudi za kumuongezea mwingine kugonga mwamba

Dar es Salaam. Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye Clatous Chama amejiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja na sasa anaweza kucheza timu moja pamoja na nyota wengine kama vile Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya kwenye kikosi hicho.

Chama alitangazwa na Yanga leo asubuhi baada ya mkataba wake na Simba kumalizika jana baada ya juhudi za kumuongezea mwingine kugonga mwamba na sasa klabu hiyo itakuwa inasubiri usajili mmoja wa Prince Dube kwenye eneo la ushambuliaji ambaye anatajwa kuwa wanaweza kumalizana naye kabla ya wiki hii kumalizika baada ya sakata lake na waajiri wake wa zamani, Azam kufikia tamati.

Hata hivyo, kumekuwa na hofu kubwa ya mchezaji gani atakaa pembeni ili kumpa Chama nafasi kwenye kikosi cha kocha Miguel Gamondi ambacho kabla yake kilionekana kuwa kamili kikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ya msimu uliopita ikiongozwa na Stephane Aziz KI kwenye safu ya ushambuliaji ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi ligi kuu (71), ilikuwa na wastani wa kufunga zaidi ya mabao mawili (2.3).

Nyuma yake Yanga waliondokewa na aliyekuwa mshambuliaji kinara Fiston Mayele, hivyo Kennedy Musonda na Clement Mzize walishindwa kuvaa viatu vya Mkongomani huyo aliyetimkia Misri, ndipo wakati wa dirisha dogo alipotua Joseph Guede.

Kutua kwa Guede kulikuwa na maana kwamba Gamondi alihitaji nguvu zaidi eneo hilo na je? kuongezeka kwa Chama ambaye anatajwa kama kiungo mahiri zaidi kwenye Ligi Kuu Bara kuna maana gani? na Yanga inaweza kucheza vipi akiwa kikosini?

Kuna mifumo mitatu ambayo, kiungo huyo anaweza kuweno ndani, lakini elewa wachezaji ni 11 uwanjani, hivyo mmoja atakaa nje.


4-3-3

Huu ni miongoni mwa mifumo maarufu na wa kisasa, ambao unatoa uwiano mzuri wakati wa kushambulia na kuzuia. Unaundwa na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.

Katika mfumo huo kama Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao saba katika ligi akiwa na Azam FC akisaini kuitumikia timu hiyo, anaweza kuwa mshambuliaji kiongozi kati ya nyota watatu wa mwisho kwa kushirikiana na Pacome, Maxi Nzegeli/ Mzize au Mudathir ambaye hivi karibuni amekuwa akitumika katika eneo hilo ndio maana msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao tisa katika ligi.

Nani wa kuanza kati ya hao wa kusaidiana na Dube, itategemea na Gamondi atakavyoamka siku hiyo na aina ya mpinzani ambaye wanakabiliana naye lakini kati ya watatu wa nyuma ya Dube, anaweza kuanza Khalid Aucho kama kiungo pekee mwenye jukumu la kukaba huku kushoto akicheza Chama na kulia Aziz KI.

Nyota hao watakuwa huru katika eneo hilo kuchezesha timu, hivyo Yanga inaweza kuwa moja ya timu yenye safu bora zaidi ya viungo wachezeshaji kutokana na rekodi za wachezaji hao, wote ni wazuri katika upishi wa mabao kutokana na ufundi walionao.


Mfumo 4-4-2

Miongoni mwa mechi ambazo Yanga ya Gamondi iliutumia mfumo huo ni pamoja na ile ya hatua ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Gamondi aliwavuruga matajiri hao wa Afrika Kusini kwa kuanza na washambuliaji wawili kiasili, Mzize na Guede japo walikuwa na majukumu tofauti.

Katika mfumo huo, Chama anaingia moja kwa moja lakini kama Dube anaweza kusaini anaweza kuanza sambamba na Mzize au Musonda huku akicheza sambamba na kiungo mwenye uwezo wa kusimama eneo hilo ambaye ni Aziz KI ameonyesha msimu uliopita.

Kati ya viungo wanne wa nyuma kama Gamondi atataka kuanza na wawili wenye uwezo wa kukaba zaidi basi nafasi inaweza kuwa kwa Aucho na Mudathir huku jukumu la kuchezesha timu likiwa mikononi mwa Chama na Aziz KI watakaokuwa na jukumu la kushambulia kutokea pembeni, ingawa bado Aziz KI pia hajasaini, watakuwa mabeki wa kushoto na kulia ambao ni Kouassi Attohoula Yao na Nickson Kibabage au Chadrack Issaka Boka kama atasaini.

Ikiwa Gamondi atataka kuanza na kiungo mmoja tu mwenye sifa nzuri za kuzuia zaidi basi Aucho au Mudathir mmoja atasubiri benchi, lakini pia Pacome au Nzengeli mmoja ataanza na Chama pamoja na Aziz KI kunogesha eneo hilo na mwingine atakaa kwenye mbao.


4-2-3-1

Muundo huu unatoa nafasi ya kucheza na mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji, na watatu wanaoshambulia huku mshambuliaji wa kati akiwa mmoja.

Dube akisaini Yanga atasimama kama mshambuliaji kiongozi huku nyuma yake kukiwa na viungo watatu washambuliaji ambao wanaweza kuwa Chama, Aziz KI na Pacome au Nzengeli.

Inaonekana kwenye mifumo yote Chama anaingia, Gamondi hana jinsi hapa atawapanga viungo wawili wakabaji Mudathir na Aucho huku Jonas Mkude akiwa na kibarua cha kupambana kupenya eneo hilo sambamba na Salum Abubakar 'Sureboy'.


Angalizo

Muudo wa mifumo mingi inaonekana kumweka nje Mzize na Maxi Nzegeli, lakini huu siyo uamuzi wa mwisho kwani kocha anaweza kuja na mingine tofauti na hii au akatumia hii lakini isiwe na majina hayo.