Guede awagawa mabosi Yanga

Muktasari:

  • Joseph Guede amezidi kuwaweka mabosi Yanga njia panda kutokana na kiwango alichoonyesha baada ya kusajiliwa msimu uliopita na kuonyesha kiwango kizuri.

Dar es Salaam. Kumezuka makundi mawili ndani ya Yanga juu ya hatma ya mshambuliaji wao Joseph Guede kila moja likiwa na hoja zake kwamba jamaa abaki au apewe 'Thank you'.

Yanga inataka kuachana na washambuliaji wake wawili Kennedy Musonda na Guede kisha zitafutwe mashine zingine wakiona kama mastaa hao hawajafanya kikubwa ingawa wote wameitumikia timu hiyo kwa nyakati tofauti.

Lakini Mwananchi linajua hata Kocha Miguel Gamondi bado anataka kusalia na Guede kwa vile tayari gari limeshawaka lakini viongozi wamemletea watu wa kazi mezani na kutaka wasajiliwa hao.

Mabosi wa Yanga wanapigania saini ya mshambuliaji Jonathan Sowah wa Ghana, Guede akapigiwa hesabu za kukatwa lakini hatua hiyo ikakutana na upinzani kutokana na uwezo wa jamaa huyo kwenye michezo ya mwisho mwa msimu uliopita.

Wanaotaka Guede afyekwe wanasisitiza na Musonda naye limkute hilohilo kwa kuwa washambuliaji hao wawili wameshindwa kufunga angalau mabao 10 kila mmoja wakiwa na kikosi hicho.

Guede ameifungia Yanga mabao sita pekee kwenye ligi ndani ya nusu msimu tu uliopita aliosajiliwa wakati Musonda akifunga mabao matano msimu mzima wa Ligi Kuu Bara ambayo Yanga ilitetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo.

Hata hivyo, Musonda amemzidi Guede katika anga la kimataifa kwa kuifungia Yanga mabao matatu mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wakati mwenzake akiwa na bao moja pekee.

Kundi la pili linalomtetea Guede linaona mshambuliaji huyo kama amefunga mabao sita kwenye nusu msimu, kama akipewa nafasi zaidi kwa msimu ujao anaweza kufanya makubwa kwa namna ya usajili mzito ambao wameufanya lakini likisisitiza kuwa staa huyo alipotoka hakuwa amepata nafasi ya kutosha ya kucheza.

Wanaomtetea Guede wakapata nguvu kubwa kutoka kwa kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi ambaye Mwananchi linafahamu kuwa ripoti yake imembakiza mshambuliaji huyo kwa sharti kwamba kama ataachwa awe amepatikana mtu ambaye hataleta mashaka kwenye kufunga.

Hatua rahisi kwa Yanga ni kwamba washambuliaji hao wawili wote mikataba yao imefikia mwisho ambapo maamuzi yoyote ya kuwabakisha yanahitaji mchakato wa kuwaongezea muda zaidi lakini kukiwa na hofu kuwa wanaweza kuletwa watu wengine ambao watashindwa kufanya mambo makubwa.

"Hadi sasa tunamsubiri Rais (Injinia Hersi Said) aliyepo Arusha kwa mapumziko kuangalia wataamua nini akishirikiana na kocha (Gamondi).

Hatua rahisi kwa Yanga ni kwamba washambuliaji hao wawili wote mikataba yao imefikia mwisho ambapo maamuzi yoyote ya kuwabakisha yanahitaji mchakato wa kuwaongezea muda zaidi, lakini Guede mwalimu alishasema anataka abaki, tusubiri tuone," kilisema chanzo cha ndani kutoka Yanga.

Hata hivyo nafasi yake inawindwa na Sowah ambapo naye hajaonyesha kiwangoi cha juu kwa nusu msimu tangu ajiunge na Al-Nasr Benghazi dirisha dogo akiwa amefanikiwa kufunga mabao matano tu na aling'aa kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal Benghaz aliofunga mabao manne peke yake wakati timu yake ikishinda 6-3.

Hata hivyo staa huyo alionyesha kiwango cha juu akiwa na Medeame ya Ghana ambapo aliifungia timu yake bao la kuongoza ilipovaana na Yanga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 kabla ya timu yake kuchapwa 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa

Kocha matetea

Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons Adolf Richard, amesema ni mchezaji ambaye alianza vibaya lakini kadri alivyokuwa anaizoea Ligi Kuu Bara alianza kuonyesha uwezo hivyo hawezi kuingilia mipango ya kocha kama yeye ndio kapitisha hilo huenda kuna kitu kaona.

"Miezi sita aliyocheza ndani ya timu hiyo na idadi ya mabao aliyofunga alitakiwa kupewa muda zaidi kwani tayari alianza kuingia kwenye mfumo lakini Miguel Gamondi ndio anafanya naye kazi kwa muda mrefu huenda kuna vitu kaona hampi kama anavyotaka.

"Kocha anayefundisha ndio mwenye maamuzi ya mwisho sisi wengine tumekuwa tukitoa maoni kutokana na tunavyowaona kwenye mechi hivyo naamini endapo angeaminiwa zaidi ni mshambuliaji ambaye angefanya mambo makubwa ndani ya timu hiyo msimu ujao na anaonekana ana uzoefu wa kutosha na ameshazoea." alisema.