Balla Conte, Kouma mzani umekaa sawa Yanga
Muktasari:
Hivi karibuni, Yanga imetambulisha nyota wanne wa kigeni ambao imewanasa kutoka klabu tofauti Afrika huku majina yaliyokuwa gumzo yakiwa ni Mousa Balla Conte na Lassine Kouma.
Hivi karibuni, Yanga imetambulisha nyota wanne wa kigeni ambao imewanasa kutoka klabu tofauti Afrika huku majina yaliyokuwa gumzo yakiwa ni Mousa Balla Conte na Lassine Kouma.
Balla Conte amejiunga na Yanga akitokea CS Sfaxien ya Tunisia wakati huo Lassine Kouma akitokea Stade Malien ya Mali.
Ukiondoa hao wengine ni Andy Boyeli aliyenaswa kwa mkopo kutokea Sekhukune ya Afrika Kusini na Celestin Ecua aliyesajiliwa kutoka klabu ya Zoman ya Ivory Coast.
Wanne hao wanachukua nafasi zilizoachwa na Stephane Aziz Ki ambaye ameuzwa kwenda klabu ya Wydad ya Morocco na Clatous Chama, Kennedy Musonda na Khalid Aucho ambao Yanga imeamua kutowaongezea mikataba.
Kwa Yanga, usajili wa Ecua, Boyeli, Conte na Kouma sio tu umeonekana kulenga kuiboresha kiubora timu hiyo bali pia umesaidia kupunguza wastani wa umri mkubwa wa wachezaji wa kigeni katika kikosi chake.
Wachezaji wanne ambao Yanga imeachana nao, walikuwa na wastani wa miaka 31 kila mmoja wakati nyota wanne waliosajiliwa hivi sasa wana wastani wa umri wa miaka 22.
Chama mwenye umri wa miaka 34, nafasi yake imechukuliwa na Kouma mwenye umri wa miaka 21 wakati Musonda mwenye umri wa miaka 30, nafasi yake imechukuliwa na Boyeli mwenye umri wa miaka 24.
Wakati Yanga Aziz Ki akiondoka Yanga huku akiwa na umri wa miaka 29, mbadala wake ambaye ni Celestin Ecua ana umri wa miaka 23 na Khalid Aucho anayeachana na Yanga akiwa na umri wa miaka 31, nafasi yake inazibwa na Mousa Balla Conte mwenye umri wa miaka 21.
Uwepo wa Chama, Aucho, Musonda na Aziz Ki pamoja na wachezaji wengine nane wa kigeni ambao wamebakia hivi sasa katika kikosi cha Yanga, ulifanya wastani wa umri wa mchezaji wa kigeni katika timu hiyo kuwa miaka 25.
Lakini baada ya wanne hao kuondoka kisha Ecua, Kouma, Conte na Boyeli kuingia, wastani wa umri wa wachezaji wa kigeni katika kikosi cha Yanga kwa sasa ni miaka 23 kwa mchezaji mmoja.
Wakati msimu uliopita mchezaji wa kigeni aliyekuwa na umri mkubwa katika kikosi cha Yanga akiwa ni Chama na umri wake wa miaka 34, kwa sasa mchezaji mwenye umri mkubwa ni Duke Abuya mwenye miaka 31.