Arsenal yafungua mwaka kibabe

Muktasari:
- Baada ya ushindi huo, Arsenal inapanda mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kutoka ya tatu ikifikisha pointi 39 ikiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo Liverpool yenye pointi 45.
Arsenal imeuanza vizuri mwaka 2025 baada ya kuchomoza na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Brentford katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Gtech Community, jana Jumatano, Januari 1, 2025.
Brentford ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 13 kupitia Bryan Mbeumo ambaye alipiga shuti baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mikkel Damsgaard.
Dakika ya 29, Gabriel Jesus aliisawazishia Arsenal akifunga bao la kichwa baada ya golikipa wa Brentford, Mark Flekken kupangua mpira uliopigwa na Thomas Partey.
Kipindi cha kwanza kilimalizika timu hizo zikitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 kabla ya kipindi cha pili dakika ya 50 Mikel Merino kuifungia Arsenal bao la pili wakati bao la tatu lilifungwa na Gabriel Martinelli dakika ya 53.
Baada ya ushindi huo, Arsenal inapanda mpaka nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England kutoka ya tatu ikifikisha pointi 39 ikiwa nyuma ya vinara wa ligi hiyo Liverpool yenye pointi 45.
Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kikosi chake kinalenga kufanya vizuri kila mchezo.
"Tunaweza kushinda kila mechi yetu inayofuata, kile kilicho mikononi mwetu tunapaswa kuhakikisha tunakifanyia kazi," amesema Arteta.
Mchezo unaofuata Arsenal itakuwa ugenini Januari 4, 2025 itakapokuwa na kibarua kigumu dhidi ya Brighton kwenye uwanja wa American Express.
MECHI ZIJAZO EPL
Jumamosi Januari 4, 2025
Tottenham v Newcastle 9:30 alasiri
Bournemouth v Everton 12:00 jioni
Aston Villa v Leicester City 12:00 jioni
Crystal Palace v Chelsea 12:00 jioni
Southampton v Brentford 12:00 jioni
Man City v West Ham 12:00 jioni
Brighton v Arsenal 2:30 usiku
Jumapili Januari 5, 2025
Fulham v Ipswich Town 11:00 jioni
Liverpoo v Man United 1:30 usiku
Jumatatu Januari 6, 2025
Wolves v Nottingham Forest 5:00 usiku