Amorim anavyoiona njia ya kutokea United

Muktasari:
- Ruben Amorim, anakabiliwa na shinikizo kubwa kufuatia matokeo mabaya ya timu, ikiwa ni pamoja na kushuka hadi nafasi ya 14 kwenye Ligi Kuu England.
Baada ya Manchester United kumfuta kazi Mkurugenzi wa Michezo, Dan Ashworth, ndani ya siku 159 tu tangu ateuliwe, huku Sporting nayo ikiachana na kocha Joao Pereira aliyetangazwa kikosini hapo Novemba 11 mwaka huu na kuondolewa Desemba 25, kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, amesema anaelewa kuwa nafasi yake si salama endapo hatofanikiwa kuzuia kushuka kwa klabu hiyo kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Hayo ameyasema baada ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wolverhampton, Desemba 26 mwaka huu ambacho kilikuwa ni kichapo cha tatu mfululizo kwa Manchester United baada kutoka kupoteza dhidi ya Bournemouth na Tottenham kwenye Kombe la Carabao.
"Nafahamu aina ya kibarua nilichonacho, kocha wa Manchester United hawezi kuwa na utulivu bila kujali hali yoyote anayopitia ndani ya timu, kila kocha yuko hatarini," amesema Amorim.
Tangu alipotua kwenye viunga vya Old Trafford, Amorim ameiongoza Man United kucheza mechi 10 katika mashindano yote ambapo amepoteza mechi tano, amepata ushindi mechi nne, sare ni moja.
Amorim (39) amesema changamoto ya kazi hiyo ni kukosa muda wa kuandaa kikosi chake ambapo alitamani kuanza kazi msimu ujao lakini uongozi wa United ulimkatalia huku akitishiwa kuikosa kazi.
Mchezo ujao United itakuwa nyumbani dhidi ya Newcastle huku ikiwakosa baadhi ya nyota wake akiwemo nahodha, Bruno Fernandes ambaye atakosa mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi iliyopita dhidi ya Wolverhampton. Manuel Ugarte naye atakosekana kutokana na kadi tano za njano.
Amorim hajafichua kama atamkabidhi Harry Maguire unahodha katika mechi ijayo, lakini amemsifia kwa nidhamu yake na mchango kwa timu.
"Anafanya kazi kwa bidii na hana visingizio, hata baada ya kupitia nyakati ngumu, yupo tayari kusaidia timu," amesema Amorim