Amorim amvaa Rashford

Muktasari:
- Mara baada ya kusema hivyo, Rashford alifanya mahojiano juzi na kusema kwamba yupo tayari kuondoka na kwenda kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amekosoa uamuzi wa mchezaji wake Marcus Rashford kutoka hadharani na kusema anataka kuondoka kwenye timu hiyo.
Amorim hivi karibuni alisema aliwaacha Marcus Rashford na Alejandro Garnacho katika kikosi kilichosafiri kucheza na Manchester City jambo lililozua mjadala mkubwa na baada ya kuulizwa alisema hana furaha na baadhi ya mambo ya nje ya uwanja ya nyota hao.
Mara baada ya kusema hivyo, Rashford alifanya mahojiano juzi na kusema kwamba yupo tayari kuondoka na kwenda kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Tetesi za kuondoka kwa Rashford zilianza kushika kasi mara tu baada ya kuachwa katika kikosi cha Man United kilichosafiri kuvaana na Man City na zimezidi kupamba moto baada ya yeye mwenyewe kuthibitisha kwamba anataka kuondoka.
Staa huyu anayekunja karibia Pauni 350,000 kwa wiki, anadaiwa kuwa huenda akatimkia Arsenal ama Hispania ambako kuna utitiri wa timu zinazomhitaji.
Gwiji wa Man United, Roy Keane akapigilia msumari akisema anaamini huu wakati muafaka kwa Rashford kuondoka Old Trafford na kutafuta 'changamoto mpya'. Rashford amecheza mechi 426 akiitumikia United kwenye michuano yote na anashika nafasi ya 15 katika orodha ya wafungaji vinara wa muda wote wa klabu hiyo akitupia mabao 135. Wakati United ameshinda Kombe la FA, EFL Cup na Europa League.
Msimu huu, hata hivyo, nyota huyo aliyeitumikia timu ya taifa ya England katika mechi 60, amefunga mabao saba tu katika mechi 24, yakiwamo manne tu katika mechi 15 za Ligi Kuu England.
"Kuondoka kwa Marcus (Rashford) itamsaidia mchezaji – changamoto mpya kwake," Keane alisema.
"Amekuwa hapa kwa muda mrefu. Unapokuwa katika klabu kubwa kwa mwenendo wako hauko sawa – wakati mwingine ni vyema kuondoka."
Hata hivyo, kabla ya mchezo wao wa jana wa hatua ya robo fainali dhidi ya Tottenham, Amorim aliulizwa juu ya kauli za staa huyo alizosema hadharani kwamba anataka kuondoka.
"Kama ningekuwa mimi, nafikiri ningeanza kwanza kuzungumza na kocha.
Hata hivyo, Amorim alisema Rashford, 27, bado anaweza akapata changamoto ndani ya Man United na akaboresha kiwango chake kwani benchi la ufundi lina mipango naye.
"Tuko bora tukiwa na Marcus Rashford, na tunajaribu kufanya kila kitu ili kumrudisha katika kiwango chake. Aina hii ya klabu inahitaji mchezaji mwenye kipaji kikubwa, na yeye ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, anahitaji tu kufanya juhudi na kufikia sehemu tunayotaji na sisi kama benchi la ufundi tunataka kumsaidia Marcus. Hakuna kilichobadilika. Tunaamini katika yeye na bado ni mchezaji wa Manchester United."
Awali, baada ya kuwaacha kwenye mchezo dhidi ya Man City uliomalizika kwa United kushinda mabao 2-1, Amorim, 39, alithibitisha kwamba Rashford na Garnacho watarejea kikosini katika mchezo wa robo fainali ya Carabao dhidi ya Tottenham wa jana.
Hata hivyo, kutokana na alichokisema, Rashford hakujumuishwa tena katika kikosi ingawa mwenzake Garnacho, 20, alikuwamo.
Rashford aliwashangaza mashabiki wa Man United katika mahojiano yake na Henry Winter aliposema: "Nadhani niko tayari kwa changamoto mpya na hatua zinazofuata. Nitakapoondoka, sitokuwa na kinyongo chochote, sitosema vibaya kuhusu Man United, hivyo ndivyo nilivyo. Siwezi kusema kitu kibaya. Nimeona jinsi wachezaji wengine walivyoongea baada ya kuondoka hapo awali, mimi sitaki kuwa mtu huyo. Nitakapondoka, nitatoa taarifa, na itatoka kwangu."