Amorim awafungia Rashford na wenzake mazoezini
Muktasari:
- Kwa sasa wachezaji hao wameagizwa kurudi Carrington, lakini wataripoti saa 11 jioni.
Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, amefanya maamuzi makali kwa kuwatenga nyota watano ambao alitangaza kuwaacha akiwemo Marcus Rashford na kuwapiga marufuku kushiriki mazoezi pamoja na wachezaji wengine wa kikosi chake hadi watakapoondoka mazoezini.
Kwa mujibu wa taarifa, Amorim alifikia uamuzi huo siku kumi zilizopita, ambapo aliamua kwamba Rashford, Alejandro Garnacho, Jadon Sancho, Antony, na Tyrell Malacia wasiwe sehemu ya kikosi kinachofanya maandalizi ya msimu mpya. Badala yake, walipewa muda wa ziada kutafuta timu mpya ingawa mpaka sasa hakuna dili lililokamilika.
Kwa sasa wachezaji hao wameagizwa kurudi Carrington, lakini wataripoti saa 11 jioni muda ambao Amorim na kikosi chake tayari watakuwa wamemaliza kufanya mazoezi na kuondoka.
Hakuna kurejea kikosini
Hadi sasa, hakuna mpango wa kuwarejesha tena katika kikosi cha kwanza. Amorim ameweka ratiba ya mazoezi asubuhi na mchana na kuhakikisha kuwa kikosi chake kinamaliza kila kitu kabla ya kundi la waliotengwa kufika.
Hata hivyo, United walisisitiza kuwa vifaa vya mazoezi vitabaki wazi kwao, japokuwa hawajumuishwi katika programu ya timu. Inaripotiwa kuwa Rashford na Garnacho waliitumia fursa hiyo kufanya mazoezi pamoja siku ya Alhamisi iliyopita.
Katika tukio la kuvutia, Rashford aliwasili Carrington dakika nane tu baada ya kocha kuondoka, na wakati huo wachezaji pekee waliokuwapo walikuwa watoto wa timu ya chini ya umri wa miaka 10.
Nyota huyo wa England anasemekana kuwa anaendelea kufanya kazi kwa bidii kujitunza fiti, huku akihitaji kufanikisha uhamisho kabla ya dirisha kufungwa. Barcelona wanatajwa kuwa na nia naye na Rashford anaamini wataweka mezani ofa rasmi hivi karibuni.
Hatma ya wachezaji waliotengwa
Jadon Sancho anatajwa kuwa karibu na uhamisho kwenda Juventus wakati Alejandro Garnacho amewekwa kwenye rada ya Chelsea, lakini tayari amekataa ofa kutoka Saudi Arabia. Antony anaweza kurejea Real Betis, ambako aling'ara kwa mkopo msimu uliopita. Huku Tyrell Malacia ambaye amekuwa majeruhi muda mrefu, sasa anawindwa na Celtic ya Scotland.
Man United wanatafuta fedha kwa ajili ya usajili mpya
United wanatarajia kuuza wachezaji hao watano ili kumwezesha Amorim kufanya usajili mkubwa. Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo ya Pauni milioni 65 (Sh225 bilioni) kwa ajili ya kumsajili Bryan Mbuemo kutoka Brentford.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Cameroon ameripoti kambini kwa Brentford Jumatatu iliyopita, lakini mazungumzo bado yanaendelea.
Amorim angetamani awe na Mbuemo tayari wiki ijayo wakati kikosi cha United kitaelekea Marekani kwa mechi tatu za kirafiki dhidi ya Bournemouth, West Ham na Everton.