Deco azuia dili la Rashford kujiunga Barcelona
Muktasari:
- Barcelona inatajwa kuwa na nia ya kumsajili Luis Diaz wa Liverpool, huku Bayern Munich nao wakiwa wanamwania winga huyo wa Colombia.
Manchester, England. Hatma ya Marcus Rashford kujiunga na Barcelona msimu huu wa joto imeingia doa kufuatia ripoti kuwa mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Hispania, Deco, ndiye kikwazo kikuu cha dili hilo kufanyika.
Rashford (27), ambaye amekuwa Manchester United tangu akiwa na umri wa miaka saba, alifichua Desemba mwaka jana kuwa anahitaji changamoto mpya.
Msimu uliopita, alitolewa kwa mkopo kwenda Aston Villa ambapo alifunga mabao manne katika mechi 17, lakini klabu hiyo iliamua kutomsajili moja kwa moja mwishoni mwa mkopo wake kutokana na mshahara mkubwa anaolipwa Rashford. Hii imemrejesha Old Trafford, ambako bado ana mkataba hadi Juni 2028.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Hispania, baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili ya Barcelona wanavutiwa na usajili wa Rashford, lakini Deco aliyekuwa nyota wa zamani wa Chelsea haridhishwi na ubora wa mchezaji huyo, hasa ukizingatia kiwango chake cha mshahara kinachozidi pauni 300,000 zaidi ya Sh1 bilioni kwa wiki.
Mwandishi Javi Miguel ameandika kwenye ukurasa wake wa X kuwa:
“Deco bado ndiye kikwazo kikubwa katika operesheni ya Rashford. Bado kuna mgongano mkubwa wa maoni ndani ya Kamati ya Usajili kuhusu winga wa kushambulia. Kwa sasa, kipaumbele ni kuondoa wachezaji ili kupunguza mzigo wa mishahara.”
Barcelona tayari wanahaha kupunguza matumizi ya mshahara ili kutimiza masharti ya La Liga na kupata nafasi ya kuwasajili wachezaji wapya.
Hadi sasa, usajili wa gharama kubwa zaidi chini ya Deco umekuwa ni Dani Olmo kutoka RB Leipzig kwa takriban pauni milioni 50. United kwa upande wao wako tayari kumuuza Rashford kwa dau dogo zaidi, hasa kutokana na kutaka kuondoa mzigo wa mishahara ya juu.
Barcelona pia inatajwa kuwa na nia ya kumsajili Luis Diaz wa Liverpool, huku Bayern Munich nao wakiwa wanamwania winga huyo wa Colombia.
Hali hiyo inamaanisha kuwa Rashford atalazimika kupunguza matarajio ya mshahara au kusubiri dili la Barcelona litimie endapo Deco atabadilisha msimamo wake.