Amorim arudi kwa Gyokeres

Manchester, England. Baada ya kuona eneo lake la ushambuliaji halipo vizuri, inaelezwa kuwa Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim amewaambia mabosi wa timu hiyo anamtaka mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres.
Awali ripoti zilibainisha kuwa, Amorim hakuwa na mpango wa kumsajili mshambuliaji huyo raia wa Sweden kipindi hiki cha Januari, lakini amebadili mawazo kutokana na kuona kuna uhitaji huo haraka.
Katika mikakati ya kuboresha eneo la ushambuliaji, imeelezwa Man United inaweza kuwauza Marcus Rashford na Joshua Zirkzee Januari hii kwani hawaonekani katika mipango ya Amorim.
Kwa mujibu wa Daily Star, Amorim amewaambia viongozi wa juu kuwa ni muhimu sana kumsajili Gyokeres mwezi huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alitua Lisbon mwaka 2023 akitokea Coventry City na kufundishwa na Amorim kabla ya kocha huyo kujiunga na Man United Novemba 11, 2024 kuchukua nafasi ya Erik ten Hag.
Uhamisho wa Gyokeres kutua Old Trafford utaigharimu Man United zaidi ya Pauni 80 milioni ambayo ni bei yake iliyowekwa katika mkataba kwa timu inayohitaji kuuvunja.