Yanga, Simba zagawa dozi Ligi Kuu kama Azam
Muktasari:
- Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa na pointi 76 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 75 huku Azam ikiwa nafasi ya tatu na pointi 60.
Dar es Salaam. Yanga na Simba zimenogesha mbio zao za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu baada kwa kila moja kupata ushindi mnono wa mabao 5-0 katika mechi za Ligi zilizochezwa leo.
Yanga imejizidi kujichimbia kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine Mbeya matokeo ambayo yameifanya ifikishe pointi 76.
Nyota wa Yanga katika mchezo huo alikuwa ni kiungo Pacome Zouzoua ambaye amepachika mabao mawili huku mengine yakifungwa na Israel Mwenda, Mudathir Yahya na Clatous Chama.
Mkoani Tabora kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Simba imetoka kifua mbele kwa kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Kengold.
Aliyeiongoza Simba kutoka kichapo hicho kwa Kengold ni Kibu Denis ambaye amefunga mabao mawili huku mengine yakiwekwa kimiani na Elie Mpanzu, Lionel Ateba na Charles Ahoua.
Matokeo hayo yameibakisha Simba katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ambapo imefikisha pointi 75.
Bao moja ambalo Ahoua amefunga, limemfanya azidi kunyemelea zawadi ya ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu ambapo sasa amefikisha mabao 16 yanayomfanya aendelee kuongoza chati ya ufungaji bora.
Kwa kutoruhusu bao leo, kipa wa Simba, Moussa Camara ameendelea kuongoza chati ya makipa waliocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao (clean sheets) akifikisha mechi 17.
Katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Azam FC imepata ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Tabora United ambayo yamepachikwa na Gibril Sillah aliyefunga mawili na mengine yamefungwa na Abdul Sopu, Iddy Selemani na Nassor Saadun.
Sare ya bao 1-1 ambayo Mashujaa FC na KMC zimepata kwenye mechi baina yao katika Uwanja wa wa Lake Tanganyika, Kigoma, yamezibakisha kwenye ligi timu zote mbili kwa vile kila moja imefikisha pointi 34.
Coastal Union iliyofikisha pointi 34 baada ya kuichapa Fountain Gate bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga nayo imekwepa rasmi kucheza mechi za mchujo za kuwania kubaki Ligi Kuu.
Kwingineko, Dodoma Jiji imefungwa mabao 2-1 nyumbani na Singida Black Stars, Pamba imeichapa JKT Tanzania kwa bao 1-0 huku Namungo FC ikilazimishwa sare tasa nyumbani na Kagera Sugar.