NANI NI NANI SERIKALI YA JPM?: Ummy Mwalimu – Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Muktasari:
Ummy Ally Mwalimu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli. Ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM mkoani Tanga. Ana miaka 42 hivi sasa na atatimiza miaka 43 Septemba mwaka huu, kwani alizaliwa Septemba 05, 1973 mkoani Tanga.
HISTORIA NA ELIMU
Ummy Ally Mwalimu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli. Ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CCM mkoani Tanga. Ana miaka 42 hivi sasa na atatimiza miaka 43 Septemba mwaka huu, kwani alizaliwa Septemba 05, 1973 mkoani Tanga.
Baba yake mzazi ni Makwaya Ally Mwalimu, mwenyeji na mzaliwa wa Tanga, ni mtumishi mstaafu wa Serikali aliyekuwa bwana afya msaidizi katika Hospitali ya Bombo, Tanga. Mama yake anaitwa Mzuri, ni mama wa nyumbani na ni mzaliwa na mwenyeji wa Mkoa wa Tanga. Ummy ni mtoto wa tano kati ya sita wa Mzee Makwaya na Bibi Mzuri.
Alianza masomo mwaka 1980 hadi 1981 katika Shule ya Msingi Chanika, wilaya ya Handeni, Tanga, akahamia Shule ya Msingi Mkwakwani, Tanga Mjini kuanzia mwaka 1982 hadi alipohitimu darasa la saba mwaka 1986.
Amepata elimu ya sekondari katika shule ya Usagara kuanzia 1987 hadi kuhitimu kidato cha nne mwaka 1990. Kisha akaendelea na sekondari ya juu kuanzia mwaka 1991 hadi 1993 alipohitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe. Mwaka huohuo 1993, alijiunga kwenye kambi ya mafunzo ya JKT, Mafinga, Iringa na kufuzu mafunzo hayo kwa miezi sita.
Alianza kubobea katika masuala ya kitaaluma alipojiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1995 akidahiliwa kusoma Shahada ya Sheria (L LB) ambayo aliihitimu mwaka 1998. Mwaka 1998 hadi 1999 alihudhuria na kufuzu mafunzo ya uanasheria wa Serikali yalitolewa na wizara ya Katiba na Sheria.
Mwaka 2000, alikwenda Afrika ya Kusini kujinoa zaidi kielimu kwa kujiunga na programu ya sheria, alihitimu mwaka 2001 na kutunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sheria (L LM) akibobea kwenye Haki za Binadamu na Demokrasia katika bara la Afrika.
Mwaka 2008, alitunukiwa cheti baada ya kufuzu kozi ya masomo yanayohusu wakimbizi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.
Ummy ameolewa, na mumewe ni mtu waliyefahamiana kwa muda mrefu tangu wakisoma wote chuo kikuu na wana watoto wawili wa kike.
UZOEFU
Tangu afanye juhudi na kuwa mbobezi wa sheria, Ummy amewahi kufanya kazi mbalimbali ambazo zimempa uzoefu usiotia shaka.
Kwanza amefanya kazi na Kamisheni ya Mabadiliko ya Sheria Tanzania (The Law Reform Commission of Tanzania) akiwa Ofisa Utafiti wa Sheria mwaka 2000 hadi 2001. Mwaka 2001 alikuwa mshauri wa kisheria mdogo “junior”, katika Sekretarieti ya Umoja wa Afrika wakati huo (OAU). Mwaka 2003 alikuwa Mtafiti Msaidizi katika Shirika la ESRF linalojihusisha na masuala ya Utafiti wa Uchumi na Jamii nchini.
Mwaka 2004, alikuwa Ofisa wa Sheria kwenye Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na mwaka huohuo aliajiriwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Denmark (Danida) lililokuwa linaendesha kazi zake kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark Tanzania akiwa Ofisa wa Jinsia na Utawala nafasi aliyoitumikia kwa miaka sita hadi 2010.
Alishiriki kura za maoni ndani ya CCM mwaka 2010 akiusaka ubunge wa viti maalumu. Alifanikiwa kuwashinda washindani wake na vikao vya CCM vikampitisha kuwa kwenye orodha ya nafasi hizo kutoka mkoani Tanga hadi alipoufikia uteuzi wa mwisho na kuwa mbunge.
Mwanamama huyu ni kati ya wanasiasa wachache ndani ya CCM ambao wamepata bahati ya kuanza na madaraka makubwa mara tu walipoingia bungeni. Alipopata ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010, aliteuliwa na Rais JK kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto akadumu kwenye wizara hiyo hadi Januari, 2014 alipohamishiwa Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa Naibu Waziri wa Nchi, anayeshughulikia Mazingira. Alikaa mwaka mmoja na Januari 2015 alihamishwa Wizara ya Katiba na Sheria kuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2015.
Kura za maoni za kusaka wabunge wa viti maalumu zilipofanyika mwaka 2015, alijitosa mkoani Tanga kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT). Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwake kushiriki na alishindana na wanamama machachari akiwamo Sharifa Abebe, Aisha Kigoda, Saumu Bendera na wengine kadhaa. Ummy ndiye aliyeongoza mpambano huo na kujihakikishia nafasi ya kurejea bungeni.
Baada ya kupitishwa na CCM na kuwa mbunge, ndipo JPM akamkabidhi rasmi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Novemba, 2015.
Nje ya siasa, Ummy amekuwa mjumbe wa mashirika mbalimbali na taasisi za kitaaluma kwa miaka kadhaa. Mathalan, amekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya Vijana ya Tanzania iliyoundwa mwaka 1998 ili kupambana na Ukimwi kwa vijana. Amekuwa mjumbe mshauri wa Bodi ya Taifa ya Ukimwi (kwa uteuzi wa Waziri Mkuu) kati ya mwaka 1999 hadi 2000, mwenyekiti wa Bodi hiyo alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Ummy pia amekuwa Mjumbe wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) tangu mwaka 2009, amekuwa mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Maendeleo ya Katiba cha Afrika Mashariki (Kituo cha Katiba – Uganda) kati ya mwaka 2006 hadi 2010. Pia, amekuwa mwenyekiti mwanzilishi wa Mpango wa Maendeleo ya wanawake wa Tanga (Tawode) tangu mwaka 2011.
Pia, amekuwa mjumbe mwanzilishi wa Wabunge wa Tanzania Marafiki wa Mazingira (Tapafe), tangu mwaka 2012 na amekuwa mjumbe mwanzilishi wa kundi la wabunge wanaopigania masuala ya lishe, uhakika wa chakula na haki za watoto tangu mwaka 2013.
NGUVU
Jambo la kwanza linalompa nguvu ni kuwa mmoja kati ya wanawake vijana wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM na kwenye Baraza la Mawaziri la JPM na kama CCM inaendeleza sera zake za kulea viongozi na kuwakuza, huenda mwanamama huyu naye anapitishwa kwenye tanuru hilo. Baraza la Mawaziri la sasa lina wanawake vijana wawili tu, yeye na Angela Kairuki na lazima tukubaliane hiyo ni nafasi ya kipekee kwao.
Pili, Ummy ana elimu nzuri ya darasani na ana uzoefu wa kufanya kazi na mashirika mbalimbali, binafsi na ya Serikali. Hiyo inamfanya kuwa mmoja wa mawaziri vijana wanaojitambua na wanaojua uongozi wa kisasa, ni mwepesi kwenye mawasiliano na miadi. Mkipanga na Ummy kukutana saa sita mchana yeye utamkuta alishafika dakika chache kabla na hilo ndilo limemsaidia kwani amekuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kwenye mazingira ya utendaji aliyopitia.
UDHAIFU
Hadi sasa Ummy ameshindwa kusimama kisiasa kwa miguu yake miwili. Alipopewa viti maalumu mwaka 2010 na kuwamo kwenye Baraza la Mawaziri la JK na kuchota uzoefu wa miaka mitano, ilitegemewa kuwa atajiondosha kwenye kada ya wanawake ambao “wameshawezeshwa na sasa wanaweza”. Kinyume na matarajio ya wengi, akajitosa tena kusaka ubunge wa viti maalumu wakati kwa uwezo, uzoefu na weledi wake, angeliweza kabisa kuwaangusha wanaume majimboni. Hiyo inatafsiriwa kwamba siyo mtu mwenye kuamini kuwa anaweza kusimama kisiasa peke yake.
Udhaifu wake wa pili unaweza kupimwa katika eneo la utoaji uamuzi na kuamini mawazo yake. Mara kadhaa amewahi kuonyesha kuwa pamoja na ubobezi alionao, bado haamini kwenye mawazo yake. Mathalani, kwenye Bunge Maalumu la Katiba alikuwa mchangiaji mkubwa wa masuala mbalimbali lakini kila mara ilimbidi ahakikishe kila anachotaka kukijengea hoja kutoka kwa nguli wa sheria, Andrew Chenge. Kichini chini, alipewa jina la “filimbi ya Chenge” kwamba sehemu kubwa ya michango aliyotoa hayakuwa mawazo yake.
Hayo mawili pamoja na rekodi ya kutokuwa na uamuzi yaliyoacha alama kwenye wizara alizopita, vinamfanya aonekane kama waziri anayejifunza kila siku. Umefika wakati aanze kufanya uamuzi mgumu bila kusubiri maelekezo ya wakubwa waliompa kazi, awe na maoni, muono mpana na mawazo binafsi yanayotokana na uzoefu wake ili aisaidie sekta ya afya na zile zinazoizunguka sekta hiyo kukua na kuleta tija kwa Taifa.
MATARAJIO
Katika miaka mitano ijayo, tunatarajia ni kuona sekta ya afya na masuala ya wazee, watoto na jinsia vikipiga hatua. Amejipanga kudhibiti mianya yote ambayo imekuwa ikikwamisha juhudi za Serikali kuboresha afya na anasema yuko tayari.
Wadau wa sekta ya afya, sekta ya haki za watoto na wazee na wale wa masuala ya jinsia, wanasema wizara anayoiongoza mara nyingi imebadilishwa mawaziri na hata wamewekwa waliobobea kwenye taaluma ya tiba ambao hutoa ahadi nyingi ambazo hawawezi kuzitekeleza, wanasema kuna matatizo ya msingi kwenye wizara hiyo na wanasubiri kuona mwarobaini gani Ummy na wenzake watakuja nao kubadilisha hali ya mambo.
CHANGAMOTO
Changamoto ya afya ni “donda ndugu” ambalo limekosa tabibu kwa miongo zaidi ya mitano, ndiyo maana baba wa Taifa Mwalimu Nyerere akaweka kipengele cha “maradhi” kama moja ya maadui wakuu wa Taifa letu. Maradhi yanamaanisha kuwa wananchi ni wagonjwa na afya zao ziko hatarini. Ummy na wenzake wana kazi ya ziada ya kuja mipango inayotekelezeka itakayoikwamua sekta ya afya Tanzania ambayo imezungukwa na rundo la matatizo hadi inakatisha tamaa.
Tanzania ni kati ya nchi ambazo hazina madaktari wa kutosha na hivyo wagonjwa wengi wanakufa au kuathirika kwa sababu madaktari wanazidiwa na kazi. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2006 zinaonyesha kuwa ni moja kati ya nchi zenye wataalamu wa afya wachache waliotahiniwa vizuri duniani. Nchi 57 duniani hadi mwaka huo, zilithibitishwa kuwa na upungufu wa madaktari na wauguzi wapatao milioni 2.4, Tanzania ikiwamo.
Wakati Afrika ilikuwa inakabiliwa na asilimia 25 ya magonjwa yote yaliyopo duniani, ilikuwa pia na asilimia 1.3 tu ya wataalamu wa afya. Uwiano wa daktari na wagonjwa kwa Tanzania wakati huo ilikuwa ni daktari mmoja anatibu wagonjwa 50,000, hali hiyo ya mwaka 2006 ina mabadiliko kiasi fulani kulinganisha na sasa ambapo daktari mmoja anatibu wastani wa wagonjwa 25,000 huku muuguzi mmoja akihudumia watu 23,000 takwimu ambazo ni za chini sana kulinganisha na Afrika Kusini ambako daktari mmoja anatibu wagonjwa chini ya 500.
Pamoja na kuongeza madaktari na wauguzi, Ummy ana kazi ya kuhakikisha miuondombinu ya utendaji wa wataalamu hawa inaboreshwa, kunakuwa na vifaa vya kutosha na vya kisasa vya utabibu, nyumba za kutosha za wafanyakazi wa sekta ya afya, zahanati za kutosha na mfumo wa uhakika wa utoaji wa dawa ili zisiendelee kuingia kwenye mikono ya madaktari wasio waaminifu.
Bahati aliyonayo ni kwamba anafanya kazi na Naibu Waziri ambaye ni mbobezi kwenye masuala ya afya, ili afanikiwe kwenye wizara hii, inampasa amuamini naibu wake na amsikilize sana yanapokuja masuala ya kitaalamu, wafanye kazi pamoja usiku na mchana. Wizara hii ina vijana, wakishirikiana na kuaminiana, watakuwa mawaziri wa mfano. Wakipigana vita na kushughulikiana, sekta ya afya itadorora na changamoto hazitaondoka huku wote wakianguka kisiasa.
Kwa sababu afya inaendana na watoto na wizara hii pia inashughulika nao, Ummy ana changamoto nyingine kubwa. Idadi ya vifo kwa watoto wachanga iko juu na kila mwaka Tanzania hupoteza takribani watoto 47,000 ambao huzaliwa wakiwa wamekufa. Pia, wastani wa watoto wachanga 39,000 huishi kwa mwezi mmoja tu baada ya kuzaliwa na hufariki na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 11 zenye idadi kubwa ya vifo vya watoto duniani.
Tusisahau pia kwamba Tanzania imeendelea kupokea watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) takribani 213,500 kila mwaka na hivyo kuifanya kuwa ya 12 kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa wakiwa njiti Afrika. Manyanyaso ya watoto, kuongezeka kwa watoto yatima mitaani, wazazi wao kufariki kwa magonjwa sugu, ni mambo yanayowazunguka watoto. Suluhisho la kudumu ni kutatua vyanzo vya matatizo ya watoto, mathalani – kama tunataka kupunguza watoto wa mitaani lazima tupambane na vyanzo vinavyowaondoa wazazi wao duniani, kuwa na mikakati ya kuimarisha uchumi wa wazazi, kuwa na mikakati ya kuimarisha ndoa, mikakati ya kutoa chakula shuleni ili kuwavutia. Wizara ya Afya inapaswa kusimama kidete na kupigania mabadiliko ya sera na mfumo wa maisha ya Watanzania ili ijipunguzie changamoto za watoto kwa muda mrefu.
Changamoto za wazee, jinsia na maendeleo ya jamii ziko lukuki. Moja muhimu kuliko zote ni namna gani Taifa litajali afya za wazee. Ukizunguka katika vijiji na miji mingi hapa Tanzania unawakuta wazee waliotoa jasho lao kwa Tifa hili mashambani na kazini wakiwa wamechoka na kudhofika kiafya na hawana mahali pa kupata matibabu. Sera ya Taifa ya kutoa matibabu bure kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 60 na watoto wa chini ya miaka mitano imebaki “mazingaombwe”. Wazee wamesahaulika kwa asilimia 100 kwenye matibabu na hadi sasa hakuna mipango ya kweli kuwakwamua kutoka kwenye vifo ambavyo vingeepukika. Ummy na wenzake wana kitanzi kikali mbele yao. Hii ni wizara ngumu.
HITIMISHO
Watu waliofanya kazi na Ummy ikiwamo ubalozi wa Denmark wameniambia ni rahisi kumpima kwa uaminifu. Pamoja na kuwa wanawake wengi ni waaminifu, ni mtu anayeaminika kirahisi, ukimpa majukumu yanayohusu fedha atarudisha hadi chenji ya mwisho, rekodi hiyo ilimbeba alipokuwa Danida na ubalozini. Uaminifu wake nadhani pia ndiyo umemrahisishia kazi na kuwamo kwenye baraza la JK kwa miaka yote mitano na sasa anapandishwa kuwa waziri kamili kwenye Serikali hii ya JPM. Naamini akiendelea mbele namna hiyo na akaweka jitihada za kupambana kulinda ajenda alizokabidhiwa, anaweza akaisaidia wizara yake kufanya kazi vizuri. La! akigeuka kuwa mtu wa kusubiri maelekezo kutoka juu, kukosa ubunifu na kutojiamini, anaweza kuingia kwenye rekodi ya mawaziri wa afya waliowahi kushindwa vibaya. Namtakia kila la heri.
*Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi.
KUHUSU MCHAMBUZI
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri ya Usimamizi wa Umma (MPA) na Shahada ya sheria (L LB) – Simu: +255787536759, Tovuti: www.juliusmtatiro.com, Email; [email protected]).