Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ya kuzingatia wakati na kabla kukopa

Kukopa ni uamuzi muhimu sana katika maisha ya mtu, hasa anapotaka kukuza biashara au mradi wake. Hata hivyo, kabla ya kuchukua hatua ya kukopa, ni muhimu kuelewa maana ya mkopo na namna ya kuutumia kwa busara ili kuepuka matatizo ya baadaye.

Mkopo ni fedha unazopokea kutoka kwenye taasisi za kifedha kama vile benki, Saccos au Vicoba, ambazo unapaswa kurejesha kwa muda maalumu pamoja na riba. Ni muhimu kuelewa kwamba mkopo sio zawadi, bali ni deni ambalo lazima ulilipe kulingana na makubaliano na kwa wakati.

Mosi. Hakikisha kwamba mkopo utakaochukua utautumia kwa ajili ya kuzalisha au kuokoa gharama ambazo ni kubwa kuliko gharama ya mkopo wenyewe, na pia una uwezo wa kurudisha mkopo. Usichukue mkopo kwa ajili ya mradi ambao hautazalisha fedha za kutosha kulipa deni lako kwa wakati.

Mathalani umechukua mkopo wa Sh1 milioni kwa marejesho wiki 10, kila wiki Sh120,000. Hakikisha una mauzo yanayozidi Sh120,000 ili ziada iwe ni kwa matumizi mengine na uwe na uwezo wa kurudisha mkopo. Kwa mikopo binafsi, ni vizuri kuwa na chanzo thabiti cha mapato kabla hujafikiria kukopa.

Pili. Usichukue mkopo kwa ajili ya kuanzisha biashara mpya. Biashara mpya haina uhakika wa mafanikio, inawezekana ukawa na usiwe na uelewa wa kutosha kuelewa maendeleo ya biashara. Kama ni mfanyabiashara, hakikisha unachukua mkopo pale ambapo unataka kukuza biashara iliyoanzishwa tayari na inayoonesha dalili za kukua. Kwa mtu binafsi, ni vizuri kuelewa mazingira ya kazi kabla ya kufikiria kukopa.

Tatu. Andaa mpango mzuri wa namna utakavyotumia fedha za mkopo. Ni vizuri kutumia mkopo kwa kila ambacho umekipanga kukifanya kabla ya hata hujakopa. Kwa kawaida fedha ina haraka. Unaweza kupata mkopo ukasahau kabisa kuhusiana na marejesho na ukatumia kwa pupa au mambo ambayo hayaleti tija.

Ni muhimu kujua njia ambazo utatumia kurudisha fedha za mkopo kwa wakati kupitia mbinu mbalimbali. Kurudisha mkopo kwa wakati inafanya kuweka historia nzuri ya kukopa ambayo utaweza kuitumia kupata mkopo mwingine kwa haraka na pengine mkubwa zaidi, hivyo mbinu za ulipaji mkopo ni muhimu kuangaliwa kabla ya kukopa.

Nne. Epuka kutumia mkopo kwa matumizi binafsi au yasiyo na tija kama vile kulipia matumizi ya safari wakati wa likizo, kufanya sherehe, starehe au kununua magari yasiyozalisha au samani za nyumbani.

Tumia mkopo kuwekeza katika shughuli zinazozalisha au kuokoa gharama. Mfano wa kupunguza gharama ni pale ambapo pengine una uwezo wa kulipia kodi ya nyumba ya shilingi laki mbili. Lakini unaweza kukopa ukajenga nyumba na ukawa una uwezo wa kurudisha kiasi hicho hicho cha laki mbili ama na ziada wakati unaishi kwenye nyumba yako uliyoijenga kwa mkopo.

Tano. Usikope kwa ajili ya kumfurahisha mtu mwingine, ama kwenda sambamba na matumizi yake au kwa ajili ya kumkopesha mtu mwingine bila riba wala mikataba. Kuna watu wanakuwa wema kiasi kwamba anaweza kukopa ili kumsaidia au kumkopesha mtu mwingine. Hii si sawa kwa sababu kukopesha pia ni taaluma na kila mtu ana malengo yake kwenye mkopo.