Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utitiri wa gesti mitaani, wageni au kuna jingine

Katika miaka ya karibuni, maeneo mengi ya mijini na hata vijijini yameshuhudia ongezeko kubwa la ujenzi wa nyumba za wageni maarufu kama "gesti" hasa ndani ya vichochoro, mbali na macho ya jamii na mamlaka.

Kasi ya ujenzi wa nyumba hizi si tu ya kushangaza, bali pia ya kutia shaka. Je, ni kweli zinajengwa kwa ajili ya wageni wanaosafiri, au kuna sababu fiche zaidi nyuma ya pazia?

Katika miji kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na hata miji midogo kama Morogoro na Babati, nyumba za wageni zimekuwa zikichipuka kila kona, wengi zikijengwa katika maeneo yasiyo rasmi, ndani ya mitaa midogo, au hata jirani kabisa na shule na nyumba za ibada.

 Ni jambo la kawaida leo kuona nyumba za wageni zilizo jirani na makazi ya watu, mara nyingine zikiwa zimefichwa nyuma ya majengo mengine makuu.

Swali kuu hapa ni: Kasi hii ya ujenzi inatokana na uhitaji halisi wa huduma kwa wageni wa safari, au kuna matumizi mengine yasiyotajwa hadharani?

Kwa kawaida, gesti nyingi hujengwa kwa malengo ya kuwahudumia watu kama vile

wafanyabiashara wanaosafiri kati ya miji na mij, wagonjwa na ndugu zao wanaokuja kutafuta matibabu mijini, wanafunzi au walimu wa muda,

wafanyakazi wa muda mfupi kama mafundi, madereva, au wasanii.

Kwa muktadha huu, ujenzi wa gesti unaweza kuonekana kuwa ni jibu kwa uhitaji halisi wa kijamii katika kujaza pengo la huduma ya makazi ya muda mfupi kwa gharama nafuu tofauti na kupanga chumba katika nyumba maalumu..

Kwa mtazamo wa haraka, nyumba hizi huonekana kama mahala sahihi na pia a sehemu za mapumziko kwa wasafiri wa mbali au wageni wa kibiashara.

Hata hivyo, ukweli mchungu ni kwamba sehemu kubwa ya matumizi ya nyumba hizi ni ya muda mfupi mara nyingine saa chache tu.

Hii imezua maswali kuhusu matumizi halisi ya nyumba hizi, huku baadhi ya watu wakidai kuwa zimekuwa maficho ya matendo ya usaliti wa ndoa, uhusiano wa siri unaohusisha watu walio kwenye ndoa na hata biashara ya ngono isiyo rasmi.

Kuna tuhuma kuwa baadhi ya gesti zinatumika kama sehemu za kukutana kwa watu walioko kwenye uhusiano wa siri.

Hili limefanya gesti kuchukuliwa na baadhi ya watu kama sehemu zinazochochea mmomonyoko wa maadili, hasa pale zinapojengwa karibu na makazi ya watu.

Serikali na taasisi za kidini zimekuwa zikipaza sauti juu ya ongezeko la talaka, migogoro ya ndoa, na kuporomoka kwa maadili miongoni mwa jamii.

Je, nyumba hizi za wageni zina mchango katika hali hii? Wapo wanaodai kuwa urahisi wa kupatikana kwa nyumba hizi katika maeneo ya karibu na nyumbani kumeharakisha usaliti wa ndoa, kwa sababu ni rahisi mtu "kupotea" kwa saa moja au mbili na kurudi kana kwamba hakuna kilichotokea.

Ni muhimu kujiuliza: Je, mamlaka za Serikali za mitaa zina utaratibu wa kuratibu, kusimamia, au hata kuchunguza madhumuni ya nyumba hizi za wageni? Hadi sasa, usimamizi unaonekana kulegalega.

Mara nyingi, wenye nyumba hizi hupewa vibali vya biashara bila uchunguzi wa kina juu ya madhumuni, maeneo yanayofaa kwa biashara kama hiyo, na athari kwa jamii inayowazunguka.

Taasisi kama halmashauri za miji, na Jeshi la Polisi, zinapaswa kuwa na nafasi ya kuhusika katika kutoa miongozo madhubuti ya mahali, wakati, na jinsi gani biashara hizi zinaruhusiwa kuendeshwa.

Wakati jamii inazidi kushuhudia ongezeko la matukio ya usaliti, talaka na kuanguka kwa maadili, ni muhimu kujiuliza iwapo miundombinu inayowezesha vitendo hivi, kama nyumba za wageni zilizojengwa kiholela vichochoroni inachangia hali hiyo.

Serikali kupitia wizara husika, serikali za mitaa na mamlaka za upangaji miji zinapaswa kuweka utaratibu madhubuti wa kutoa vibali vya ujenzi wa nyumba za wageni.

Pia kuangalia umbali wa nyumba hizi na taasisi nyeti kama shule na makanisa; kufuatilia matumizi halisi ya nyumba hizi ili zisitumike vibaya na kuanzisha kampeni za kutoa elimu juu ya athari za kuporomoka kwa maadili ya kifamilia.

Ni wakati wa kutazama upya mtindo huu wa ujenzi wa gesti kila kona, na kujiuliza: Tunajenga kwa ajili ya maendeleo au tunachimba kaburi la maadili yetu?

Kuna haja ya mamlaka husika (kama halmashauri, polisi, na mashirika ya maendeleo ya jamii) kuweka utaratibu wa kusajili na kusimamia gesti zote, kuhakikisha kuwa zinatoa huduma salama na halali kwa jamii.