Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata kuandika taarifa binafsi 'gesti' laibua hoja kinzani

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022, ni kosa kuandika majina na taarifa za mtu aendako, kabila na siku ya kutoka katika nyumba ya kulala wageni

Dar/Mikoani. Siku moja baada ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kueleza upungufu na hatua ambazo sheria inaelekeza katika utoaji wa taarifa kwenye vitabu vilivyoko kwenye nyumba za kulala wageni, baadhi ya watu wamepongeza namna sheria inavyoelekeza.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili Machi 2, 2025 baadhi ya wananchi wamesema hatua hiyo itasaidia usiri wa faragha za wateja zinazoonekana kukosa ulinzi.

Jana Machi mosi, 2025 kwenye warsha ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji wa Tume ya Taarifa na Ulinzi Binafsi (PDPC), Stephen Wangwe alisema kuandika majina na taarifa za mtu aendako, kabila na siku ya kutoka katika nyumba ya kulala wageni ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022.

Hata hivyo, amesema taarifa hizo zinaweza kutolewa na muhusika kama atakuwa ameridhia na asishinikizwe.

“Wateja wasishinikizwe, ukimshinikiza, unakiuka Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi anaweza akachukua hatua, lakini kama ataridhia mwenyewe, hayo ni makubaliano yenu mnayopaswa kuandikishiana kwa maandishi,” amesema Wangwe.

Dereva anayefanya safari zake kutoka Mbeya kwenda Tunduma, Emily Emily amesema mfumo wa awali wa wateja kuandika taarifa kwenye vitabu vya nyumba za wageni, zilikuwa na udanganyifu na hata kuhifadhi wahalifu.

"Mimi ni mlengwa kutokana na kazi zangu, asilimia kubwa ya wateja hutoa taarifa za uongo, hivyo hatua ya Serikali kueleza ukweli kuhusu jambo hili inapaswa kupongezwa na ilibidi wapige marufuku kabisa,” amesema.

Mkazi wa Mtaa wa Forest jijini Mbeya, Rachel Francis amesema anaipongeza Serikali kwa kuja na sheria hiyo kwa kuwa,  itasaidia kuondoa au kupunguza udanganyifu ambao watu walikuwa wakiutumia mara nyingi.

"Kwanza napongeza kitendo hicho, hata mimi nilikuwa nakereka sana naenda 'gesti' na mpenzi wangu natakiwa kuandika taarifa nitokako na niendako, kiukweli nilikuwa natoa taarifa za uongo kuanzia majina namba za simu na makazi,” amesema Rachel.


Wamiliki

Wakizungumzia na Mwananchi, baadhi ya wamiliki wa hoteli na nyumba za kulala wageni, wamesema sheria hiyo ya ulinzi wa taarifa binafsi, itawasaidia kupata uhalisia wa watu wanaolala kwenye nyumba zao kwa takwa la kisheria.

Mkurugenzi wa Hoteli ya County Side Katika Manispaa ya Iringa, Frank Nyalusi amesema kama sheria itafuatwa na kuzingatiwa, itasadia kulinda faragha za wateja wao.

Nyalusi amesema baadhi ya wateja wao huandika majina na namba za simu, kabila na mahali anakotoka na kwenda, ambazo si za kweli.

“Sasa uoga utandoka, kwa sababu si wafanyakazi wote ni waaminifu, wengine wanavujisha siri za wateja na kuwaingiza matatizoni,” amesema Nyalusi.

Mwenyekiti mstaafu wa wamiliki wa nyumba za kulala wageni mkoani Dodoma, Chavuma Taratibu amesema mfumo wa kuandika taarifa binafsi za mteja kwenye daftari la wageni umeletwa na baadhi ya halmashauri nchini kwa lengo la kukusanya mapato ya asilimia 10.

Taratibu amesema madaftari ya kuandika taarifa za wageni wanaolala huwa yametengenezwa na halmashauri, hivyo hulazimika kuyanunua kwa ajili ya matumizi na hawaruhusiwi kujaza kwenye madaftari mengine zaidi ya yale yanayotolewa na uongozi.

"Kwa hiyo zile taarifa ambazo zinatakiwa kujazwa zimeandaliwa huko huko na halmashauri na wana uwezo wa kuja kulikagua daftari hilo muda wowote hata kama ni saa saba usiku ili kujua kama taarifa zilizojazwa kwenye daftari zinaendana na hali halisi ya wageni waliopo," amesema Taratibu.

"Juzi nilikuwa Dar es salaam nililala nyumba ya wageni, muhudumu aliniuliza kama nina kitambulisho cha uraia au paspoti ya kusafiria nikampa kitambulisho cha uraia akaskani kwa kutumia simu yake ya mkononi akapata taarifa zote kuhusu mimi akanionyesha chumba nikaendelea kula maisha, sikuandikwa kwenye karatasi."

Mmiliki wa nyumba ya kulala wageni ya Mupako Lodge ya wilayani Handeni, Rose Mndeme amesema kuna umuhimu wa mteja kuandika jina anapolala, bila kufanya hivyo wamiliki wa nyumba za kulala wageni na Serikali watapoteza mapato kwa kutojua idadi ya wateja waliolala.

"Mara nyingi wanaoandika taarifa za uongo wanakuwa ni wahalifu au wamekwenda kwenye mambo yao ya starehe na hawataki wajulikane kama walikuwepo hiyo sehemu, lakini tu mwenye nia nzuri hawezi kusema uongo na akiwa ameaga vizuri,” amesema Rose.

Meneja wa Hoteli ya Macheto wilayani Handeni Mkoa wa Tanga, Janeth Sendenga amesisitiza umuhimu wa wateja kuandika taarifa zao wanapoingia kwenye nyumba za wageni.

Janeth amesema baadhi ya wateja huondoka na funguo za vyumba walivyokaa, lakini kupitia mawasiliano yao, wahusika wanaweza kuwasiliana nao ili warejeshe funguo hizo badala ya kuvunja milango na kusababisha gharama zisizo za lazima.

Pia, ametaja faida nyingine kwa wateja, kama vile kusaidia kurudisha mali zao wanazoweza kusahau, kama kompyuta, simu au vitu vingine vya thamani.

“Kupitia namba za simu zilizoandikishwa, kabila na mahali anapoishi, wateja hufahamishwa na kupatiwa mwongozo wa jinsi ya kurejeshewa mali zao.

“Taarifa za mteja kwetu ni siri, haturuhusu mtu mwingine kushika kitabu cha wageni na kusoma taarifa hizo. Ni uongozi wa hoteli na watumishi wa Serikali wanaohusika na ukusanyaji wa mapato pekee ndio wenye mamlaka ya kupitia orodha hiyo kwa ajili ya makadirio ya kodi na tozo," amesema Janeth.


Changamoto za matumizi ya NIDA

Wasimamizi wa nyumba za wageni wamesema ingawa matumizi ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) kama ilivyopendekezwa na PDPC yangesaidia kupata taarifa sahihi, bado kuna changamoto kwa sababu si wateja wote wana vitambulisho hivyo.

Kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Sheria ya Hoteli, Sura ya 105, kila mmiliki au mhudumu wa nyumba ya kulala wageni anapaswa kuweka kitabu cha wageni kwa ajili ya kuandika majina na anwani za wageni, pamoja na taarifa nyingine zinazohitajika.

Johnson Lawi, msimamizi wa nyumba ya kulala wageni ya Malawi, iliyopo Mabibo amesema kuwa kutegemea kitambulisho cha Taifa pekee ni changamoto kwani si kila mteja anacho. Amesema ni vyema kutumika vitambulisho vingine vyenye picha za wahusika badala ya kutegemea NIDA pekee.

"Matukio ya uhalifu yamewahi kutokea, mtu ameandika taarifa zake kikamilifu lakini namba za simu zinakuwa za uongo. Hili linafanya kuwa vigumu kuwafuatilia wahusika," amesema Lawi.

Mmiliki wa Lodge ya Safari Yetu, Herrison Mbilinyi amesema kuwa kwa sasa hawatumii vitambulisho kwa sababu wateja wengi wanasema hawana vitambulisho wala kazi rasmi, hivyo huishia kuandika kabila na umri wao pekee.


Maoni ya viongozi wa Serikali za Mitaa

Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Mwingamno amesema  matumizi ya kitambulisho cha Taifa si wazo baya kwa sababu yanaweza kusaidia kupata taarifa sahihi za wageni na kupunguza tatizo la watu kuandika majina yasiyo yao.

"Changamoto kubwa ni kwamba watu wengi wanaamini nyumba za wageni ni sehemu ya starehe pekee, bila kujali kuwa kuna wengine wanaotumia kwa malazi wakati wakiwa safari za kikazi au shughuli nyingine," amesema Mwingamno.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson amesema kwa sasa wanahitaji kanuni inayotafsiri Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya 2022 ili kuona hatua zinazofaa kuchukuliwa endapo tatizo linatokea kwenye nyumba za kulala wageni.

"Kuna haja ya kuwa na mfumo wa kutambua wageni unaoendana na sheria za faragha za mtu binafsi, huku ukihakikisha usalama na ukusanyaji sahihi wa mapato," amesema Johnson.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema sheria hiyo inalinda faragha za watu lakini pia inakabiliwa na changamoto katika utekelezaji wake, hasa kwa masuala ya usalama wa wageni na nchi kwa jumla.

"Usalama ninaouzungumzia hapa ni wa mgeni mwenyewe, wale unaowakuta kwenye nyumba hiyo na usalama wa Taifa kwa jumla. Nafikiri taarifa zinazopaswa kutolewa ni zile za kawaida kama majina, namba ya simu au namba ya NIDA. Sioni kama hizi taarifa ni za siri," amesema Malima.

Amesema taarifa binafsi zinazochambua maisha ya mtu binafsi au familia yake, kama vile anakokwenda, anachofanya au hali yake ya ndoa, ndizo zinazopaswa kulindwa.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema huwezi kuwa na wageni wanaoingia kwenye nyumba za kulala bila kuandika taarifa muhimu za utambuzi, kwa sababu hilo litapunguza mapato ya halmashauri na risiti haziwezi kutolewa bila taarifa sahihi.


Imeandikwa na Denis Sinkonde (Songwe),Hamida Sharif (Morogoro),Rajabu Athuman (Tanga) Devotha Kihwelo (Dar), Bahati Chume na Yesse Tunuka (Moshi),Hawa Mathias (Mbeya), Mgongo Kaitira (Mwanza), Hellen Mdinda (Shinyanga) na Christina Thobias Iringa