Usiyoyajua kuhusu kuandika majina yako kitabu cha wageni ‘gesti’

Muktasari:
- Imekuwa mazoea na wakati mwingine ni lazima kwa wageni wanaokwenda kwenye nyumba za wageni kuandika waendako, watokako na siku ya kuondoka. Hata hivyo Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imesema kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Morogoro. Wakati Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) ikitoa elimu ya namna ya kulinda taarifa binafsi, imeonekana kuwa hata kuandika utokako na uendako kwenye nyumba za wageni ni moja ya ukiukwaji wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi.
Akiwasilisha mada ya dhana ya ulinzi wa taarifa binafsi, Mkurugenzi wa usajili na Uzingatiaji wa PDPC, Stephen Wangwe, amesema ni muhimu watu wakaijua sheria ili kuepuka kuingia kwenye matatizo, na kwamba kwa kuandika mtu anatoka na kwenda wapi au kabila lake havihusiani na yeye kufikia kwenye nyumba aliyokwenda kulala.
"Unakwenda nyumba ya kulala wageni unaambiwa andika ulikotoka na unakokwenda, kabila lako lakini haya yote ni taarifa binafsi na wanavunja sheria. Au kipindi cha nyuma matokeo ya mitihani yalikuwa yanatangazwa kwa majina, inatakiwa kuweka namba ili kulinda taarifa za mtu,”amesema.
Amesema kinachopaswa kuandikwa ni namba ya kitambulisho cha Taifa ambayo zikihitajika taarifa za muhusika zinapatikana humo.
Amesema tangu kuwepo kwa sheria hiyo mtu anapoona taarifa zake zimetumika bila ridhaa yake anaruhusiwa kulalamika kisha hatua zitafuatwa dhidi yake.
"Taarifa zako zikitumika vibaya na huna kokote pa kulalamika maana yake hutakuwa na imani na huduma husika, kutokana na hali hiyo wapo ambao hawatoi fedha kwenye ATM hadi aende ndani ya benki, na baadhi ni kwa sababu wameshaumizwa kwa taarifa zao binafsi kuwa hadharani,”amesema Wangwe.
Wangwe amesema sheria imekuwepo ili kurudisha imani kwa watu, wote wanaochakata taarifa binafsi wanasajiliwa, kusikiliza, usuluhishi hadi mtu atakapopata haki yake.
Aidha, amefafanua kuwa misingi ulinzi wa taarifa binafsi ni mkusanyaji au mchakataji akusanye kihalali, afanye kwa haki bila kuonea, kwa uwazi anakusanya kwa lengo gani na madhumuni mahususi asivuke mpaka wake.
Mingine ni kukusanya kwa utoshelevu na asikusanye chini ya kiwango au zaidi ya kiwango kinachohitajika, taarifa zitoke kwa muhusika na zisionekane kwa wasiohusika, lazima ziwe sahihi na ziende na wakati, hairuhusiwi kuhifadhi taarifa chini ya muda au zaidi ya muda husika.
Misingi mingine ni taarifa zinazovuka nje ya mipaka ya nchi. Ambapo amesema kuwa kwa sasa ukitaka kupeleka taarifa nje ya nchi ni lazima kupata kibali cha nchi ili kujua zinakwenda wapi, kuna ulinzi wa kutosha wa taarifa zake na kuna fomu namba saba ya kujaza na kikubwa kuhakikisha zinapotoka ziwe na uhakika wake.
Amesema kuna mifumo 850 imeunganishwa na Kitambulisho cha Taifa (Nida) na kabla ya kuzitumia lazima apate cheti cha kufanya hivyo. “Kokote ambako taarifa yako itatumiwa na mtoa huduma yeyote utapata ujumbe ili uwe na ridhaa kwenye taarifa zako.”
Wangwe amesema pia ni kuhakikisha inajulikana taarifa za unatoka wapi unakwenda wapi haziwahusu wanakusanya taarifa za ziada ambazo sio zao, pia wanaotoa matokeo hawaruhusiwi kutangaza majina bali kuweka namba pekee.
Baadhi ya wananchi akiwamo Azizi Habibu amesema amekuwa akikereka hata pale anapoingia kwenye nyumba za wageni na kutakiwa kuandika siku anayotoka, aendako na atokako.
"Unafika mapokezi kwenye nyumba ya wageni muhudumu anakwambia uandike na tarehe ya kutoka mara oooh andika namba yako ya simu, mara andika majina yako hii mimi naiona kama ni uvijishaji wa taarifa binafsi," amesema Habibu.
Aisha Salumu ni muhudumu kwenye nyumba moja ya wageni katika Manispaa ya Morogoro amesema wao wanalazimika kuweka utaratibu huo kwa wageni wa kuandika majina, namba za simu, watokako, waendako na siku ya kutoka kwa sababu ya usalama wa mgeni husika na wageni wengine waliopo katika nyumba hizo.