Prime
UCHAMBUZI WA MJEMA: Hivi wabunge mnafahamu ni kipi kinawasubiri huko majimboni?

Tumebakiza takribani siku 150 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu 2025 na siku 32 kabla ya Bunge la Tanzania kufungwa rasmi na wabunge kurejea majimboni kama raia, niwatonye tu kuwa kuna makundi mawili yanawasubiri kwa hamu.
Sisi tulio huku mitaani, tunayasikia makundi haya namna yalivyojiandaa kupitisha hukumu ya haki dhidi ya wabunge hivyo ni vyema kwa wale wenye nia ya kutetea ubunge wao basi wajue kuwa kila Mbunge atavuna kile alichopanda miaka mitano.
Wala siwatishi, kwa sababu Bunge la 11 tulizoea kusikia Rais aliyekuwepo, John Pombe Magufuli na baadhi ya mawaziri na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakisema wabunge wa upinzani walikuwa wanachelewesha maendeleo. Ndio maana miaka 8 iliyopita, Magufuli alizuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kwa miaka mitano akisema “Nisingependa mtu yeyote (vyama vya upinzani) anicheleweshe kuyatekeleza hayo niliyoyaahidi kwa wananchi (2015-2020)”
Aliongeza kusema “Niwaombe wanasiasa wenzangu wafanye siasa za ushindani baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyowaahidi tumetekeleza”, CCM ilikuwa na wabunge wa kuchaguliwa 189, Chadema 34 na CUF walikuwa 32.
Sasa Bunge hili la 12 lina wabunge 256 wa kuchaguliwa kutoka CCM ambao ni sawa na karibu asilimia 97 ya wabunge wote na kufanya bunge lionekane kama la chama kimoja licha ya uwepo wa wabunge nane kutoka vyama vitatu vya upinzani.
Serikali iliyopo madarakani na inayomaliza muda wake Oktoba ni ya CCM, kwa hiyo kwa maneno mengine ilani ya uchaguzi 2020-2025 inayotekelezwa ni ya CCM, hivyo kama kuna manung’uniko ya wananchi, kitanzi ni kwa CCM si upinzani.
Nimetanguliza kueleza hayo kama Yohana Mbatizaji katika Biblia ambaye alikuja kusafisha njia ili sasa nitakapoyataja haya makundi mawili na kwanini ndio yataamua kama wabunge wa sasa warejee bungeni ama la, niweze kueleweka. Ninayasema haya kwa sababu uchaguzi mkuu 2015 na 2020, CCM kiliingia madarakani kupitia ushawishi wa ahadi (promise voting), lakini hii 2025 CCM kitachaguliwa kwa kupima ufanisi wa utekelezaji ahadi ama Performance Voting. Kundi la kwanza ambalo linawasubiri kwa hamu wabunge wetu na hapa nazungumzia wa CCM ambao ndio wenye Dola, ni wajumbe watakaoshiriki kura za maoni ndani ya CCM kwa wale ambao wana mpango wa kutetea viti vyao.
Nawakumbusha tu kuwa mkumbuke mazingira ya mchakato wa kura za maoni ulivyofanyika 2020 na mjipime wenyewe kimoyo moyo kama wewe unayenisoma ulishinda kweli kura za maoni au ulibebwa na ‘God Father’ ambaye leo hayupo?
Mkumbuke, kuna wenzenu waliongoza kura za maoni kihalali lakini kwa sababu ambazo mimi na wewe hatuzijui, ‘God Father’ aliwaengua, na kuna walioongoza kwa kucheza rafu ambao hao walienguliwa kihalali kabisa kwa sababu walistahili.
Sasa wale wajumbe ambao walikunyima kura mjue wapo wengi walirudi katika uchaguzi wa ndani ya CCM 2022 na kichinjio bado wanacho na wana hasira na mtu asiwadanganye kuwa makundi yalivunjwa, wana kinyongo mioyoni mwao.
Lakini pia mjue wako ambao walishinda kura za maoni lakini wakaenguliwa kwa figisu ambao wametangaza nia ya kurejea tena wakiamini kwa kuwa ‘God Father’ hayupo, basi wanaamini uwanja wa ushindani utakuwa ni wa huru na haki.
Hilo ni kundi la kwanza ambalo linawasubiri kwa hamu wabunge wanaotokana na CCM na wanasubiri tu kipenga kipulizwe, na nasema mchakato huu, unaweza kuvunja rekodi kwa idadi ya wabunge wengi waliopo sasa kushindwa kupenya.
Kundi la Pili linalowasubiri wabunge kwa hamu ni wananchi ili waweze kuwahukumu wale ambao wameshindwa kuitumia vyema Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 katika kuwawakilisha bungeni.
Ibara hiyo ndogo ya Katiba inasema Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.
Majukumu hayo ni pamoja na kumuuliza Waziri yeyoyote swali lo lote kuhusu mambo ya umma hapa Tanzania ambayo yako katika wajibu wake na kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti.
Mbali na wajibu huo, lakini mbunge ana wajibu wa kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi, kutunga sheria na kujadili na kuridhia mikataba inayohusu Tanzania na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa.
Kulingana na ratiba ya mkutano wa kumi na tisa wa Bunge (mkutano wa Bajeti) ulioanza Aprili 8 hadi Juni, 26 2025, Rais Samia Suluhu Hassan atalifunga bunge hilo Juni 27,2025 na hapa sasa inakuwa rasmi mchakato wa uchaguzi kuanza.
Ukiacha wajibu huo, mbunge anapaswa kuhudhuria vikao vya Kamati na vile vya Baraza la Madiwani kwa kuwa navyo huhusika na mipango ya maendeleo katika ngazi ya kata na vijiji, hivyo uwakilishi wake pia ni muhimu kama alivyo diwani.
Leo hii tungekuwa na Katiba ile iliyotokana na maoni ya wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba (mstaafu), wananchi wasingesubiri hadi bunge livunjwa ndio wawajibishe wabunge wao.
Ibara ya 129 (a) na (b) ya rasimu ya Katiba hiyo iliwapa mamlaka wapiga kura kumwajibisha mbunge bila kusubiri kumalizika kwa kipindi cha miaka mitano.
Sababu mojawapo ni kama atakuunga mkono sera ambazo zinaenda kinyume na maslahi ya wapiga kura au kinyume na maslahi ya Taifa na kama atashindwa kuwasilisha au kutetea kwa dhati hoja zinazotokana na kero za wapiga kura wake.
Tungekuwa na Ibara hiyo katika katiba yetu ya sasa, nina uhakika wapo wabunge ambao sijui idadi yao, wangepigwa chini na wapiga kura wao kutokana na kile tunachokishuhudia katika Bunge la 12 linalofikia Ukomo wake Juni 27,2025.
Mathalani, na hili mtakutana nalo huku uraiani, mtaulizwa nini Bunge limefanya kwa kutumia mamlaka yake ya ile ya Ibara ya 63 katika kuisimamia na kuishauri Serikali kutokana na kuibuka kwa wimbi la utekaji, mauaji na kupotea kwa watu.
Maana siku hizi Bunge ni LIVE (mbashara) hivyo kila mtu anaona japo mvuto wake umepungua, sasa sisi raia tutataka mtuambie Bunge limefanya nini katika jambo hili, ni lini suala hili limejadiliwa au hata tu kuunda Kamati Teule kuchunguza.
Sisi raia wema tena wazalendo, tutahitaji majibu kutoka kwenu namna mlivyotumia ibara hiyo kusimamia Serikali na vyombo vyake ili chaguzi zetu ziwe za huru na haki na mfano halisi ni uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa 2024.
Ukiacha masuala ya utekaji na kupotezwa kwa watu kunakofanya na genge la uhalifu ambalo hadi sasa halijulikani, Jeshi letu la Polisi linanyooshewa kidole sana katika ukiukwaji wa haki za binadamu na mifano ipo mingi, mlifanya nini?
Sitaki kuwatajia mambo mengi ili msijiandae na majibu, maswali mtashtukizwa nayo huku uraiani na kwa kweli tutahitaji majibu kuhusu kupanda kwa gharama za maisha na kuendelea kuwepo kwa sheria kandamizi katika vitabu vyetu vya sheria.
Kwa kifupi tu niwanong’oneze, mambo ni mengi ila muda ni mchache. Umma unahitaji majibu ya kutosha kwenu kwani tunawaona LIVE mnayoyafanya, mnayoyasimami na tunaona vijembe, ngonjera na mipasho ya baadhi yenu.
Jiandaeni na majibu, umma wa watanzania unawasubiri kwa hamu majimboni
0656600900