Prime
Wabunge hawa Tanga tumbo joto, sababu hizi hapa

“Kazini kwa wabunge wa majimbo 10 mkoani Tanga kuna kazi”, ndiyo lugha nyepesi inayoweza kutumika kutafsiri mtifuano na kivumbi cha kuusaka ubunge kinachoendelea katika mkoa huo.
Kivumbi hicho, kinatajwa kukaribia kuweka rehani ubunge wa baadhi ya wabunge maarufu na waliowahi kushika wizara nyeti ndani ya Serikali, kutokana na kuibuka washindani wenye nguvu ya fedha na ushawishi wakinyatia majimbo hayo.
Majimbo yaliyo katika hekaheka hizo ni Tanga Mjini, Korogwe Mjini, Muheza, Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Mkinga, Lushoto na Mlalo.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye majimbo hayo, majimbo ya Bumbuli (January Makamba), Pangani (Jumaa Aweso), Kilindi (Omary Kigua) na Korogwe Vijijini (Timotheo Mzava), bado joto halijapanda ukilinganisha na majimbo mengine.
Tanga Mjini
Ukiachana na historia, wasifu na ukongwe wa Ummy Mwalimu katika ubunge, kuanzia viti maalumu hadi jimbo la Tanga Mjini, mwaka huu atakabiliwa na kibarua kigumu cha ushindani kutoka kwa kada wa muda mrefu wa CCM, Omary Ayubu.
Ayubu amewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Wilaya na Mjumbe wa Kamati wa Mkoa wa Tanga na turufu yake ni kile kinachodaiwa kuwa, anaungwa mkono na vigogo wa chama hicho.
Inaelezwa Ayubu, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Soka ya Coastal Union mjini Tanga, anamchachafya vya kutosha Ummy katika nafasi hiyo na kivumbi kitatimka kitakapopulizwa kipyenga cha mchakato wa ndani wa chama.
Muheza
Muheza nako iliko himaya ya Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma hakujapoa, kutokana na kinachoelezwa kuwa, aliyeliongoza jimbo hilo zamani, Balozi Adad Rajab analitaka tena.
Katika mchakato wa kura za maoni za mwaka 2020, Adadi, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), aliongoza kwa kura 577 akifuatiwa na Mwana FA aliyepata kura 296.
Wadadisi wa mambo wanasema huenda Balozi Adadi akajitosa tena, kwani inadaiwa wanachama wengi bado wana imani naye na wanaamini kwamba alidhulumiwa mwaka 2020.
Korogwe Mjini
Shughuli nyingine itakuwa Korogwe Mjini ambapo kuna makada Swaibu Mwanyoka ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, pamoja na Allan Kijazi wanayetajwa kuutaka ubunge katika eneo hilo.
Kama hiyo haitoshi, Handeni Mjini kutakuwa na kazi kwa Reuben Kwagilwa kwa kuwa na majina ya makada Sonia Magogo (aliyekuwa mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CUF) na Omary Kigoda (mbunge wa zamani wa jimbo hilo).
Handeni Vijijini, Lushoto Mjini na Mkinga
Vivyo hivyo, Handeni Vijijini kwa John Sallu ambako aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mboni Mhita (DC kwa sasa) anatajwa kupasha misuli kujitosa katika kinyang’anyiro hicho.
Katika Jimbo la Lushoto Mjini, linaloongozwa na Shaaban Shekilindi (CCM), inaelezwa atakabiliwa na Profesa Riziki Shemdoe (Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi), pamoja na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mathew Mbarouk.
Katika jimbo la Mkinga, kutakuwa na kibarua kingine kwa Dustan Kitandula ambaye ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa kuwa kuna makada wawili wenye nguvu wanaoliwania jimbo hilo. Makada hao ni Mwahija Twaha na Said Ntimizi.
Hata hivyo, haitakuwa mara ya kwanza kwa Ntimizi, ambaye huko nyuma aliwahi kujitosa lakini hakufanikiwa mbele ya Kitandula.
Wakati rafu na vurugu zikiendelea chini chini katika majimbo hayo, ukimya umetawala katika majimbo ya Bumbuli, Mlalo, Korogwe Vijijini, Kilindi na Pangani.
Bumbuli
Katika jimbo la Bumbuli, hivi karibuni, baadhi ya wananchi waliodai ni wakazi wa Bumbuli mkoani Tanga, walifanya mkutano jijini Dar es Salaam wakishinikiza mbunge wao, Makamba, ajiuzulu kwa madai ya kushindwa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Rashid Ayoub alisema Makamba ameshindwa kutatua kero za barabara, ufufuaji wa michezo hasa kujenga viwanja, ahadi ambazo aliahidi lakini hajazitekeleza ndani ya miaka 15 ya ubunge wake.
Mbali na madai ya wananchi hao, kuna mabango yaliyowekwa katika jimbo hilo yakieleza kwamba "Makamba imetosha" awapishe watu wengine kuongoza jimbo hilo.
Hata hivyo, Makamba alijibu madai hayo akisema mabango hayo hayakutengenezwa na wananchi wa Bumbuli, bali watu wanaoishi Dar es Salaam kwa lengo la kumchafua.
Wakazi wa Tanga walonga
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Tanga, waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema mchuano wa kura za maoni utakuwa mkali endapo wanaotajwa watajitosa rasmi katika mchakato huo.
Walisema mchuano huo utakuwa mkali kwa sababu baadhi ya wanaotajwa kuutaka ubunge walishawahi kuzitumikia nafasi hizo, lakini majina yao yalienguliwa mwaka 2020, licha ya kushinda katika kura za maoni.
Mkazi wa Tanga mjini, Kiama Mwaimu ambaye ni mchambuzi wa siasa, anasema Ummy atakuwa na kibarua kigumu cha kukabiliana na Ayubu, anayeungwa mkono pia na vijana wengine katika jimbo hilo.
“Muheza nasikia Balozi Adadi anataka kurudi tena, kwa hiyo kutakuwa na mchuano mgumu kati yake na Mwana FA. Mbunge wa sasa anatumia nyota yake ya usupastaa kwenye muziki kuvutia watu, hasa vijana kutokana na kizazi chake.
“Upinzani mkali unaweza ukatokea, vijana wengi sio wanaopiga kura, wanaweza kumshangilia lakini sio kumpigia kura. Balozi anatambulika sasa na huruma ndani yake kwamba mwaka 2020, alienguliwa, sasa wazee wengi wanamuona ni mtu aliyefanya mambo mazuri,” anasema Mwaimu.
Kuhusu Korogwe Mjini, Mwaimu anasema amesikia tetesi za kutajwa jina la Kijazi, akitaka kuwania ubunge katika jimbo hilo, akisema eneo halina mwenyewe na matokeo ya ubunge yamekuwa yakiwashangaza wengi.
“Allan Kijazi ni jina kubwa na ukoo mkubwa, inategemea namna atakavyozichanga karata zake kuelekea katika mchakato huo, kutakuwa upinzani. Kwa upande wa Lushoto siwezi kuongea maana waliopo wana nguvu wanazijua siasa za wilaya hiyo,” anasema Mwaimu.
Mkazi mwingine wa Tanga, Ramadhan Manyeko anaungana na Mwaimu akisema endapo makada wanaotajwa wakijitosa, wataleta ushindani mkubwa katika mchakato wa kura za maoni.
Kwa mujibu wa Manyeko, baadhi ya wabunge wanaomaliza muda wao wamewekeza zaidi kwa wajumbe, si kwa wananchi.
“Kilio chetu kama wakazi wa Tanga kipo kwa wajumbe wanaowapitisha hawa wagombea. Baadhi ya wajumbe wanawaangalia wagombea si wananchi, ndiyo maana wakifika kwenye sanduku la kura, wanaangalia masilahi yao badala ya wananchi,” anasema Manyeko.
Mbali na hilo, Manyeko anasema kuna baadhi ya wabunge wa mkoa wa Tanga wamewaangusha wapigakura wao, hivyo si ajabu kuona kuna ushindani kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
“Mchuano ni mkali sana, hawa wote waliotajwa wana nguvu na ushawishi mkubwa katika majimbo husika,” anasema.
Mchambuzi afafanua
Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya kijamii na mkazi wa Tanga, Andrew Swai alisema kinachoonekana kinathibitisha kuwa mtindo wa siasa umebadilika.
Mabadiliko hayo ni kile alichofafanua, kwa sasa watu wanatumia mbinu yoyote kuwania uongozi na inafanyika hivyo wakidhamiria kipato baada ya cheo.
“Kinachoangaliwa sasa ni uwezo wa mtu kupambania na kuminyana katika namna yoyote kupata nafasi,” alisema.
Alisisitiza siasa ya sasa imekuwa kama biashara, hasa kwenye nafasi za ubunge watu wanaangalia zaidi watapata nini baada ya kushinda, ndiyo sababu mchuano majimboni umekuwa mkali.
Ingawa katika majimbo ya mkoani humo ushindani unafanywa kwa chinichini nyakati hizi, alisema dalili zinaonyesha kuna uwezekano wa baadhi ya wabunge wakongwe wakaangushwa.
Baada ya uhuru, Tanga ilikuwa miongoni mwa mikoa yenye wabunge waliokuwa na ushawishi mkubwa katika maendeleo ya kitaifa.
Historia ya ubunge Tanga
Wakati wa mfumo wa chama kimoja (1965-1992), ubunge ulikuwa sehemu muhimu ya uongozi wa TANU na baadaye CCM, huku majimbo kama vile Tanga Mjini, Muheza, na Korogwe yakichangia sana katika siasa za nchi.
Katika kipindi hicho, wabunge wa Tanga walikuwa sehemu ya Serikali Kuu na walishiriki katika uundaji wa sera za maendeleo.
Majimbo ya Tanga yalikuwa na wawakilishi waliotokana na uchaguzi wa ndani wa CCM, huku wagombea wengi wakipita bila kupingwa. Wabunge kama Rashid Kawawa na Amani Karume walihusiana kwa karibu na maendeleo ya kisiasa ya eneo hili. Mwaka 1992, Tanzania iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, hali iliyoleta ushindani mpya katika siasa za Tanga.
Vyama kama CUF, Chadema, na NCCR-Mageuzi vilianza kushindana na CCM katika uchaguzi wa bunge. Katika baadhi ya vipindi, baadhi ya majimbo yalichukuliwa na upinzani, ingawa CCM imeendelea kuwa na ushawishi mkubwa.
Majimbo kama Tanga Mjini, Pangani, na Handeni yamekuwa yakibadilika kulingana na mwelekeo wa kisiasa wa taifa. Wabunge mashuhuri waliowahi kuongoza majimbo haya ni Salim Turky na Omari Nundu.
Kwa upande wa Muheza, Dk Haji Hussein na Balozi Adadi Rajabu, huku Korogwe ni Mary Chatanda na Stephen Ngonyani, maarufu kama ‘Profesa Majimarefu’.