Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MALOTO: CUF na tiketi ya kwanza ya urais kando ya Profesa Lipumba

Chama cha Wananchi (CUF), kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, kimeweka matumaini yao ya mapambano ya kisiasa kwenye mabega ya Gombo Samandito Gombo. Yeye ndiye mgombea urais. Mgombea mwenza wake ni Husna Mohamed Abdallah.

Katika uchaguzi wa kisiasa, mgombea urais ndiye hebeba uhai wa chama. Nguvu yake hutegemewa kunyanyua wagombea wa nafasi za chini. Kwa Tanzania ni ubunge na udiwani. Gombo anapaswa kujenga ushawishi ili achaguliwe kuwa Rais, vilevile wabunge na madiwani wa CUF.

Tanzania ni taifa lenye Serikali mbili. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, hutegemewa pia kuongesha ushawishi kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, vilevile madiwani wa halmashauri za Zanzibar. Hii inaitwa Coattail Effect.

Ufafanuzi huo unadhihirisha wajibu wajibu mkubwa wa Gombo kwenye uchaguzi ambao kipyenga chake kimeshapulizwa. Kinachosubiriwa ni taarifa ya uteuzi wa mwisho wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), ambayo inatarajiwa kutolewa Jumatano (Agosti 27, 2025).

Baada ya uteuzi wa Inec, kama atateuliwa, Gombo anatarajiwa kuzunguka Tanzania Bara na Visiwani akijinadi na mgombea mwenza wake, akiwanadi wagombea wengine; mgombea urais wa CUF Zanzibar, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

Uchaguzi Mkuu 2025, CUF wametoka nje ya mazowea. Mgombea wake wa urais (Gombo) ni uamuzi mpya. Inawezekana ndiyo mwanzo wa zama mpya za chama hicho, ambacho kilipata kuongoza upinzani kwa miaka 15 (mwaka 1995 mpaka 2010).


CUF ilipotoka

Ilete orodha ya wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu 1995, ambao ulikuwa wa kwanza nchini wenye kuhusisha mfumo wa vyama vingi vya siasa baada ya uhuru wa Tanzania.

Pitia wote, utakumbuka kuwa wasifu wa darasani wa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, ulimfanya awe tishio mno.

Viongozi, wanachama na mashabiki wa CUF, kwa fahari na majivuno makubwa, walimnadi Profesa Lipumba kwa sifa zenye umaalum dhidi ya wagombea wenzake; Benjamin William Mkapa (CCM), Augustino Lyatonga Mrema (NCCR-Mageuzi) na John Momose Cheyo (UDP).

Ilinadiwa kuwa Lipumba ni mmoja wa wasomi wachache wa uchumi wenye alama nyingi zaidi duniani. CUF walimpamba kwamba wasomi daraja la Lipumba ni wanne tu duniani.

Na wasifu ulipoandikwa, kulikuwa na maneno “full bright”, kwamba ilithibitishwa kuwa uanazuoni wa Lipumba ulichagizwa na akili nyingi.

Basi, hilo ndilo lililokuwa debe kubwa la CUF kwa Lipumba wao. Msomi wa hali ya juu. Mchumi wa dunia. Full bright. Na kila aina ya maneno chanya yenye kumpambanua kama msomi aliyetukuka. Na haikuwa sifa za debe tupu, bali kweli Lipumba ni mtu mahiri mno katika nyanja ya uchumi.

Kuweka historia sawa ni kwamba Lipumba alikuwa mgombea urais wa mwisho kutangazwa na chama chake mwaka 1995. Halafu, akawa mgombea kijana kuliko wote. Alikuwa na umri wa miaka 43 tu, wakati wenzake wote watatu walikuwa na umri wa miaka ya 50 kuelekea 60. Mkapa alikuwa na umri wa miaka 57. Mrema takriban miaka 51. Cheyo alikuwa hapishani sana Mkapa.

Msomi zaidi. Alikuwa pekee mwenye shahada ya uzamivu (PhD). Alitambulishwa kuwa mwanazuoni aliyekuwa akitumiwa sana na taasisi kubwa za kifedha duniani kama mshauri na mwelekezi.

Na wakati anagombea urais wa Tanzania mwaka 1995, alikuwa anatokea kwenye ajira ya mshauri wa uchumi wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Alitambulishwa pia kuwa alipata kuwa mshauri wa kiuchumi wa Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.

Jumlisha sifa nyingine kemkemu. CUF walitembea kwa fahari kubwa na jina la Profesa Lipumba. Huo ukawa mwanzo wa upacha mkubwa, baina ya tiketi ya urais wa Cuf na Lipumba.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 1995, Lipumba alikubali ushawishi wa kuwa Mwenyekiti wa Cuf. Nafasi ambayo ameendelea kuishikilia mpaka sasa.

Mwaka 2000, Lipumba aliingia kwenye Uchaguzi Mkuu akibeba matumaini makubwa ya wapinzani.

Aliungwa mkono na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vilevile Chama cha Democratic (DP), ambacho wakati huo hakikuwa kimepata usajili.

Ni mwaka 2000, ungemuona aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila, akiizunguka nchi kufanya kampeni kumnadi Lipumba dhidi ya Mkapa aliyekuwa anawania kurejea madarakani kwa muhula wa pili.

Na ikumbukwe, wakati huo, Mtikila alikuwa ametoka jela, alikohukumiwa mwaka mmoja kwa hatia ya kauli ya kuudhi, juu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999.

Mwaka 2000, ungewaona waliokuwa vinara wa Chadema, Bob Makani (Mwenyekiti), Dk Aman Kabourou (Katibu Mkuu), Dk Willibrod Slaa (Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara), Freeman Mbowe na wengine, wakiwajibika kwenye majukwaa ya kampeni kumwombea kura Lipumba ili achaguliwe kuwa Rais wa Nne wa Tanzania.

Katika uchaguzi huo, Lipumba alimaliza nafasi ya pili, nyuma ya Mkapa. Alimaliza mbio akiwa mbele ya Mrema, aliyegombea kwa tiketi ya chama TLP, na ambaye mwaka 1995 ndiye alitoka wa pili akiwa na NCCR-Mageuzi.

Kwa maana hiyo, Lipumba aliibeba Cuf kupanda ngazi moja katika mbio za urais ndani ya miaka mitano. Cheyo na UDP yake, aliendelea kubaki wa nne.

Mwaka 2005, Lipumba aligombea urais kwa mara ya tatu. Safari hiyo dhidi ya Jakaya Kikwete (CCM), Freeman Mbowe (Chadema), Emmanuel Makaidi (NLD), Augustino Mrema (TLP), Sengondo Mvungi (NCCR-Mageuzi), Paul Kyara (SAU), Mtikila (DP), Anna Senkoro (PPT-Maendeleo) na Leonard Shayo (Demokrasia Makini). Katika uchaguzi huo, Lipumba alimaliza wa pili nyuma ya Kikwete.

Mwaka 2010, Lipumba aligombea urais kwa mara ya nne. Matokeo yalipotoka, alimaliza nafasi ya tatu, nyuma ya Kikwete aliyetetea urais wake na kuchaguliwa kuongoza muhula wa pili, na Dk Slaa wa Chadema, aliyegombea kwa tiketi ya Chadema.

Mwaka 2015, Lipumba hakugombea, kwani chama chake (Cuf), kilimuunga mkono mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, aliyeungwa mkono na muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Cuf, Chadema, NLD na NCCR-Mageuzi, ndivyo vyama vilivyounda Ukawa.

Mwaka 2020, Lipumba alichukua fomu ya kuwania urais katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020. Vijana wa Cuf walimchukulia fomu, naye akakubali. Na chama chake kilimpitisha. Katika uchaguzi huo, Lipumba alitoka wa tano nyuma ya wagombea wa vyama vya CCM, Chadema, ACT-Wazalendo na NRA. Yalikuwa matokeo mabaya zaidi katika historia ya CUF.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, CUF wakiwa wanamtegemea Gombo kama karata turufu, swali ni moja tu; je, Gombo atairudisha CUF kwenye enzi ya kuwa chama imara cha upinzani na chenye msuli wa kushindana katika uchaguzi, au atakididimiza zaidi? Vipi, atakibakisha chama hicho mahali alipokikuta? Yote yanaweza kuwa matokeo.

Majibu ya maswali yote ni namna karata za uchaguzi zitachangwa, kisha matokeo kutangazwa baada ya shughuli pevu ya siku nzima, Oktoba 29, 2025.

Muhimu kukumbuka, CUF haijawahi kuwa na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kando ya Profesa Lipumba. Gombo anakuwa wa kwanza.