Tuweke mazingira haya kukuza ajira kwa vijana

Ukosefu wa ajira umeendelea kuwa moja ya changamoto kubwa inayowakumba vijana nchini.
Serikali inapaswa kutambua kuwa, changamoto ya ajira inazidi kuathiri vijana wengi, hivyo inahitajika mikakati ya muda mrefu ya kuhakikisha nafasi za ajira zinaongezeka. Uboreshaji wa mifumo ya ajira na upatikanaji wa nafasi zinazozingatia sifa halisi za waombaji ni hatua muhimu katika kuhakikisha ukosefu wa ajira unapungua na vijana wanapata fursa za kiuchumi.
Changamoto ya nafasi za kazi imedhihirika juzi katika matokeo ya ajira zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Takwimu kutoka kwa TRA zinaonesha kuwa, kati ya waombaji 80,888 waliofanya usaili wa awali kwa ajili ya nafasi za kazi, 74,383 walikosa sifa ya kuendelea na hatua inayofuata.
Hiyo ni idadi kubwa inayotoa taswira ya hali halisi ya changamoto ya ajira inayowakabili vijana wengi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na TRA, waombaji 6,505 ndio walichaguliwa kuendelea na mchakato wa usaili kwa njia ya kuandika, huku nafasi zinazotangazwa zikiwa ni 1,596 tu. Hatua hiyo inaonesha kwamba, hata wale wachache waliofaulu mtihani wa awali bado watakutana na ushindani mkubwa katika kupata nafasi za ajira.
Hata hivyo, idadi hiyo ya waombaji ni ndogo mno ukilinganisha na vijana wanaomaliza masomo na kutafuta ajira kila mwaka.
Hali hiyo inadhihirisha jinsi gani vijana wanavyojitahidi kuingia katika soko la ajira huku mfumo wa ajira ukiwaruhusu wengi kutafuta nafasi kwa walio na vigezo, lakini wanakutana na changamoto ya kutopata nafasi hizo.
Hali ya ukosefu wa ajira nchini, inahitaji hatua za haraka na madhubuti kutoka serikalini ili kupunguza changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene, Serikali inatarajia kushughulikia vibali 41,500 vya ajira katika mwaka wa fedha 2025/26 ili kujaza nafasi zilizoidhinishwa katika ikama.
Hata hivyo, hatua hiyo haitoshi kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira, kwa kuwa, idadi ya vijana wanaomaliza masomo na kutafuta kazi kila mwaka ni kubwa mno kuliko nafasi zinazopatikana.
Tunasema kuna umuhimu wa kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha vijana wanapata ajira au kujiajiri katika sekta nyingine nje ya utumishi wa umma ambao sasa unaonekana kuwa kimbilio la wahitimu wengi wa vyuo na wengineo.
Kwa mfano, Serikali inaweza kuwekeza zaidi katika sekta za kilimo, viwanda na teknolojia ili kuweka mazingira na nafasi zaidi za ajira kwa vijana.
Mazingira haya yanaweza kujumuisha utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa makundi ya vijana, ambapo fedha watakazopata wanaweza kuziwekeza kwenye miradi mbalimbali kama vile kilimo na usafrishaji.
Lakini pia kuweka mazingira ya kuvutia uwekezaji wa wageni kwenye viwanda ili kutoa ajira kwa Watanzania.
Aidha, kuna umuhimu wa kuanzisha programu za mafunzo ya ujuzi wa kazi na kujitegemea ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kupunguza utegemezi wa ajira za serikalini.
Tatizo la ukosefu wa ajira linahitaji mikakati madhubuti ya Serikali ili kuhakikisha vijana wanapata fursa za ajira.