Prime
Tunachafuliwa! Tuwe wazalendo tusinyamazie uchafuzi huu!

waungwana husema hivi, “Uongo ukisemwa, ujibiwe, usipojibiwa utageuka kuwa ukweli.” Katika hili ninalolijadili le, tusipokuwa makini, tutachafuka, tuwaambie tu.
Nasema hivyo kwa sababu uzalendo wa kweli wa Mtanzania ni kuipigania nchi yake kwa dhati na kuweka maslahi ya taifa mbele, iwe ni wakati wa heri au wa dhiki.
Mzalendo wa kweli hatakubali kuona nchi yake au Rais wake anatukanwa au kusemwa vibaya kwa hoja za uongo, hususan kutoka kwenye vyombo vya habari vya mataifa ya nje, wakiwamo majirani zetu. Hali hii haiwezi kupuuzwa, hasa pale vyombo vyetu vya habari navyo vikiamua kukaa kimya.
Kwa kuwa shutuma hizo zinahusu matukio yanayodaiwa kufanywa na vyombo vya mamlaka ndani ya nchi, ni wajibu wa vyombo vyetu vya habari na taasisi zetu rasmi kujitokeza kufanya uchunguzi wa kina na baada ya kujiridhisha kuwa ni uongo, vitoke hadharani kuukanusha. Aidha, mamlaka za serikali hazipaswi tu kutoa kauli za kukanusha, bali pia zinapaswa kudai radhi rasmi kutoka kwa wale wanaochafua taswira ya Tanzania kama kisiwa cha amani.
Kwa sababu uongo, ukirudiwa na kutojibiwa, hatimaye unaanza kuaminika. Kauli zinaumba, na hivyo, hatari kubwa ni kwamba taswira ya Tanzania inaweza kuharibika kimataifa bila sababu za kweli.
Makala hii ninaiandika kufuatia kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani, Tundu Lissu iliyoitwa mahakamani wiki iliyopita.
Wanaharakati kutoka nchi jirani walitaka kuja kuhudhuria kesi hiyo bila vibali, wakazuiwa kuingia nchini na wengine kurudishwa wakiwa uwanja wa ndege. Hali hii ilisababisha kilio kikubwa cha kutotendewa haki, kilichosababisha hadi Bunge la Ulaya nalo likajaribu kutaka kuingilia mambo yetu ya ndani.
Wengine waliopenyeza nchini kwa njia zisizo rasmi waliishia kushikiliwa na mamlaka zetu na kurejeshwa makwao salama.
Hata hivyo, waliporudi makwao, walitoa madai mazito ya kudhulumiwa na kudhalilishwa kingono.
Shutuma hizi zikawakumbusha Wamarekani kuingilia pia, huku vyombo vya habari vya jirani na vya dunia vikituandika vibaya na mitandao ya kijamii ikitumika kututukana Watanzania, kumtukana Rais na kuichafua nchi huku mamlaka na vyombo vya habari vikikaa kimya kama vimepigwa ganzi.
Ni lazima tutambue kwamba Rais wa nchi ni kielelezo cha taifa. Anapotukanwa, si yeye binafsi tu anayechafuliwa, bali taifa lote linakumbwa na aibu. Hoja yangu ya msingi ni kwamba, mamlaka zetu haziwezi kuendelea kukaa kimya. Zinapaswa kusema ukweli wa kilichotokea.
Yale wanayodai wanaharakati hawa siyo vitendo vinavyolingana na mwenendo wa taasisi zetu rasmi za serikali.
Kama wasemavyo Wazungu: “Silence is the admission of guilt” kimya ni ishara ya kukiri kosa. Usipoyajibu madai ya uongo, dunia haitajua ukweli bali itayaamini.
Hili linaweza kuathiri siyo tu taswira ya nchi, bali pia ustawi wa sekta zote zinazotegemea amani ya Tanzania.
Mimi kama mwandishi wa habari, mtangazaji wa kujitegemea, mwanasheria na wakili, siwezi kuamini moja kwa moja shutuma hizi hadi pale mamlaka zetu zitakapojitokeza kuthibitisha au kukanusha.
Ninatoa wito kwa Watanzania wote, tusikubali kuamini kila baya linalosemwa kuhusu nchi yetu bila uthibitisho wa mamlaka zetu.
Ni kweli kuna matukio ya watu kupotea na mamlaka kubaki kimya, jambo linalotia wasiwasi.
Mamlaka zinapaswa kujitokeza na kutueleza kama kuna wahusika ‘wasiojulikana’ wanaofanya vitendo hivi, basi sasa wamevuka mipaka kwa kuwakandamiza hata wageni walioko mahotelini. Hili haliwezi kukubaliwa.
Ushauri Wangu
Shughulikieni Chanzo: Haya yote ni matokeo, siyo chanzo. Ni muhimu kuhakikisha mizizi ya tatizo inakabiliwa. Nadhani “kale ka Simba ka Kizimkazi” kakiachiwe kunyamazisha hizi kelele zote.
Kama kuna ukweli kwenye tuhuma hizi, wote waliohusika katika kuwapiga, kuwadhalilisha au kuwatenda vibaya wanaharakati hawa, basi washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
Kwa kuwa EU na Marekani nao wameshaongea, tusikae tena kimya. Lazima tujibu mapigo, kwa hoja na kwa ukweli. Uzalendo wa kweli ni kuilinda heshima ya nchi lakini pia, kuhakikisha ukweli unatajwa na uongo unafutwa mapema kabla haujageuka kuwa ukweli wa mitaani.