Prime
Kelele za mlango hazimkoseshi mwenye nyumba usingizi, zikizidi zinakera!

Leo naendelea na mfululizo wa makala kuhusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), kwa kuangazia dhana ya sovereignty, yaani uhuru wa nchi na kutokuingiliwa katika masuala yake ya ndani.
Mada hii imeibuliwa kufuatia malalamiko ya baadhi ya Watanzania kwamba Bunge la Ulaya limepitisha maazimio yanayodhaniwa kuingilia uhuru wa nchi yetu.
Kwa maana ya moja kwa moja, sovereignty ni haki ya nchi kuwa huru kuamua na kusimamia mambo yake bila kuingiliwa na mtu, taasisi au taifa lolote.
Hivyo, hatua ya Bunge la Ulaya kutoa maazimio kuhusu Tanzania inaweza kutafsiriwa kama kuingilia mamlaka yetu ya kujiamulia mambo wenyewe.
Kikanda na kimataifa, Tanzania ni nchi moja yenye Rais mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba moja ya JMT na mamlaka kamili ya kujiongoza.
Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya JMT, sheria zilizotungwa na Bunge lake, pamoja na kanuni na taratibu zake.
Hata hivyo, nchi zote duniani huongozwa kwa mchanganyiko wa sheria za ndani na za kimataifa.
Miongoni mwazo ni Sheria za Ndani (Domestic Laws). Hizi hutungwa na Bunge la JMT kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Nyingine ni Sheria za Kimataifa. Hizi zinazungumzia makubaliano au mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania huiridhia kupitia Bunge kwa mchakato uitwao ratification.
Mara tu sheria hizi zikiridhiwa, huwa sehemu ya sheria za nchi na hivyo lazima zizingatiwe.
Kwa msingi huu, iwapo Tanzania itakiuka sheria yoyote ya kimataifa iliyoiridhia, taasisi za kimataifa kama Bunge la Ulaya zina mamlaka ya kuijadili au kutoa maazimio ya kutaka utekelezaji wa sheria hizo.
Watanzania wengi hawajui kuwa Tanzania imeridhia mikataba mingi ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, kama Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (UDHR).
Hata hivyo, utekelezaji wake bado ni changamoto, mfano ni uwepo wa hukumu ya kifo, licha ya haki ya kuishi kutambuliwa katika mikataba hiyo.
Ili kurekebisha hali hii, hatua ya kwanza ni kuhakikisha Bunge linatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya JMT ya mwaka 1977.
Ibara ya 63(2) ya Katiba inaelekeza kuwa Bunge lina wajibu wa kuisimamia Serikali na vyombo vyake vyote, kuhakikisha havikiuki sheria za ndani wala za kimataifa.
Kwa maneno mengine, Bunge lina wajibu wa kuhakikisha Serikali inafuata Katiba kikamilifu, na kutoidhinisha utekelezaji wa jambo lolote linalokiuka Katiba.
Mara kadhaa nimeeleza kuwa mabadiliko ya katiba ni jambo la lazima kabla ya kufanya marekebisho ya sheria nyingine, kwa sababu ndiyo sheria mama. Hatuwezi kutunga sheria mpya zinazokinzana na Katiba.
Kwa mfano, sheria iliyounda Tume Huru ya Uchaguzi si halali kwa sababu Katiba haijafanya mabadiliko ya kuitambua tume hiyo (INEC); Katiba bado inatambua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Hali hii inaifanya sheria hiyo kuwa batili.
Mfano mwingine ni sharti la mgombea uongozi kuwa na udhamini wa chama cha siasa. Hili ni kinyume cha Ibara ya 21 ya Katiba ya JMT na pia linakiuka Tamko la Kimataifa kuhusu Haki za Kisiasa na Kiraia (ICCPR), pamoja na Hati ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR)—ambazo zote Tanzania imeridhia lakini haijazitekeleza ipasavyo.
Tangu mwaka 1979 hadi 2005, Bunge limefanya mabadiliko ya Katiba mara 14 kwa kutumia sheria za kawaida, jambo ambalo halistahili. Bunge ni zao la Katiba, hivyo halipaswi kubadilisha Katiba kwa kutumia utaratibu ule ule unaotumika kubadilisha sheria nyingine za kawaida.
Dunia ya sasa imekuwa kijiji, matendo ya taifa moja yanaangaliwa na mataifa mengine. Sote tunakumbuka yaliyowapata viongozi kama Uhuru Kenyatta, Omar al-Bashir, Muammar Gaddafi na Saddam Hussein.
Historia ya Tanzania pia inatufundisha enzi za utawala wa Rais Julius Nyerere tuliwasaidia majirani wetu Uganda kuondoa utawala wa kidikteta.
Ombi langu kwa Bunge ni kuhakikisha linaiwajibisha Serikali ipasavyo. Na kwa Serikali yetu, ni vyema iendelee kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa Katiba na sheria.
Tukifanya hivyo, hatutakumbwa na malalamiko au mashinikizo kutoka nje. Ingawa kelele za nje haziwezi kumnyima mwenye nyumba usingizi, zikiwa nyingi sana huwa kero.
Ombi langu kwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kutumia muda uliobaki kabla ya uchaguzi mkuu kufanya mabadiliko madogo ya Katiba.
Hii itazima kabisa kelele hizi na kurejesha imani kwa wananchi na jamii ya kimataifa.