Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mikakati ya ujenzi iwekwe katika utekelezaji

Wizara ya Ujenzi imeliomba Bunge liidhinishe Sh2.28 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambazo kati ya yake, Sh2.18 trilioni zitaelekezwa kwenye maendeleo na Sh90 bilioni zitatumika katika matumizi ya kawaida.

Mathalan, kiwango hicho cha fedha kimeongezeka kutoka ile ya mwaka 2024/25 iliyokuwa Sh1.77 trilioni.

Hatua ya Serikali kuongeza bajeti eneo la ujenzi inaonyesha nia ya kutaka kuboresha miundombinu ya usafiri kama njia ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa ya ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa barabara, hasa maeneo ya vijijini na pembezoni mwa nchi, hata barabara zinazoharibika kwenye miji.

 Kwa miaka mingi, mipango mingi ya ujenzi wa barabara imekuwa ikibuniwa, lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu. Hivyo ili kuleta mabadiliko ya kweli na ya kudumu kwa wananchi, ni muhimu Serikali ielekeze nguvu zake katika kukamilisha miradi ya barabara badala ya kuendelea kuanzisha mikakati mingi ambayo huishia kwenye makaratasi bila utekelezaji.

Barabara ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa. Upatikanaji wa barabara nzuri huwezesha wakulima kufikisha mazao yao sokoni kwa wakati, huwavutia wawekezaji, na huongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za jamii kama afya na elimu.

Tunasikia kwenye vyombo vya habari wajawazito baadhi ya maeneo vijijini wakijifungulia njiani kutokana na ubovu wa barabara.

Tumesikia michango ya wabunge namna walivyo hatarini kutopokewa jimboni au kukataliwa kwa sababu ya barabara walizoahidi kutokujengwa au kukamilika.

Vilevile wakulima wamekuwa wakipata hasara kutokana na mazao kuharibika yakiwa shambani kutokana na ubovu wa barabara au hata kama magari yakifika huishia kuharibika kuzama kwenye tope na wakati mwingine kuanguka.

Kwa ujumla kukosekana kwa barabara huchangia kupanda kwa gharama za maisha na kupunguza tija ya shughuli za uzalishaji na kuchelewesha kukua kwa miji.

Serikali imekuwa ikibuni mipango kama Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26), pamoja na mipango ya kikanda kama “Mkakati wa Taifa wa Kuendeleza Sekta ya Usafirishaji.” Hata hivyo, baadhi ya mikakati hii hukosa utekelezaji madhubuti kwa sababu ya ukosefu wa fedha, mabadiliko ya vipaumbele kisiasa, au ukosefu wa usimamizi thabiti.

Katika mazingira haya, Serikali inapaswa kuacha kurundika mipango mingi katika ujenzi na badala yake ichukue hatua za kuhakikisha miradi iliyoanzishwa inakamilishwa kwa wakati ili kuondoa malalamiko kama walivyowasilisha wabunge katika michango yao.

Moja ya njia muhimu za kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa barabara ni kupitia vyanzo bunifu vya fedha kama vile "Samia Bond”, ambayo tunasubiri kuona matunda yake.

Huu ni mkopo wa ndani ambao Serikali imekuwa ikiweza kufadhili miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea misaada au mikopo ya masharti magumu kutoka nje. Kupitia dhamana kama hizi, Serikali inaweza kupata fedha nyingi kwa wakati mfupi na kuelekeza moja kwa moja kwenye ujenzi wa barabara muhimu.

Aidha, ushirikishwaji wa sekta binafsi kupitia mikataba ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) unaweza kuwa njia nyingine ya kuharakisha ukamilishaji wa miradi ya barabara.