Mifumo ya kidijitali ni silaha ya kuongeza mapato
Katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Tanzania imeweka mkazo mkubwa katika kujitegemea kifedha na kupunguza utegemezi wa mikopo pamoja na misaada kutoka nje, suala la kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani linakuwa la msingi zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Serikali inapohitaji kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo, huduma za kijamii na uwekezaji wa kimkakati, lazima iwe na vyanzo vya uhakika vya mapato. Njia mojawapo yenye uwezo mkubwa wa kufanikisha lengo hilo ni matumizi ya mifumo ya kidijitali inayopunguza au kuondoa kabisa uhusika wa binadamu katika ukusanyaji wa kodi, ushuru na ada mbalimbali za Serikali.
Kwa miaka mingi, changamoto kubwa katika ukusanyaji wa mapato si ukosefu wa walipakodi pekee, bali pia uwepo wa mianya ya upotevu wa fedha kutokana na udhaifu wa mifumo, makosa ya kibinadamu na wakati mwingine vitendo vya rushwa.
Pale ambapo fedha zinakusanywa kwa kutegemea maamuzi ya mtu mmoja mmoja, uwezekano wa kutokea kwa upotevu wa mapato huwa mkubwa. Hata hivyo, maendeleo ya teknolojia yameonyesha kuwa mifumo ya kidijitali inaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto hizo.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni mfano mzuri wa taasisi ambayo imeanza kuona matokeo chanya kutokana na uwekezaji katika mifumo ya kidijitali
Mifumo kama Stempu za Kielektroniki (ETS) na matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki na njia nyingine za kidijitali za kufuatilia biashara yameongeza uwazi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato.
Hata hivyo, bado kuna nafasi kubwa ya kuimarisha zaidi matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha kila muamala unaostahili kulipiwa kodi unaonekana na kurekodiwa kwa wakati halisi.
Faida za mifumo ya kidijitali hazipo TRA pekee. Serikali za mitaa nazo zinaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa mapato yao kupitia mifumo ya kisasa ya ukusanyaji wa ushuru na ada. Katika maeneo mengi bado kuna utegemezi wa ukusanyaji wa fedha kwa njia zinazohusisha makarani au wakusanyaji wa kawaida, jambo ambalo linaweza kusababisha upotevu wa mapato.
Mfumo unaowezesha malipo kufanyika moja kwa moja kupitia simu za mkononi, benki au majukwaa ya kidijitali unaweza kuhakikisha kila shilingi inayolipwa inaingia moja kwa moja kwenye akaunti husika bila kupitia mikono ya mtu.
Hali kadhalika, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa sheria za usalama barabarani yanaweza kuongeza mapato ya Serikali huku yakiboresha uadilifu. Katika mataifa mengi, ukiukwaji wa sheria za barabarani hutambuliwa na kamera maalumu zinazorekodi makosa moja kwa moja na kutuma faini kwa mhusika bila kuhitaji mawasiliano ya ana kwa ana na askari.
Mfumo wa aina hiyo unapunguza mianya ya rushwa na kuhakikisha faini zote zinazotozwa zinaingia Serikalini badala ya kupotelea njiani. Teknolojia pia inaweza kusaidia kutambua walipakodi ambao hawalipi kodi stahiki na hivyo kupanua wigo wa mapato bila kuongeza viwango vya kodi.
Faida nyingine kubwa ya mifumo ya kidijitali ni uwezo wake wa kutoa taarifa sahihi kwa ajili ya kufanya maamuzi. Serikali inapokuwa na takwimu za wakati halisi kuhusu mapato yanayokusanywa katika kila sekta, inakuwa rahisi kubaini maeneo yenye udhaifu na kuchukua hatua za haraka.
Mataifa mengi yaliyoendelea na hata baadhi ya nchi zinazoendelea yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kudhibiti uvujaji wa mapato kwa sababu ya uwekezaji katika mifumo madhubuti ya kidijitali. Katika nchi hizo, uwezekano wa fedha kupotea kati ya mlipaji na Serikali ni mdogo sana kwa sababu mifumo mingi imeunganishwa na inawasiliana moja kwa moja.
Kuanzia bandarini, viwandani, katika biashara ndogo na hata kwenye huduma za usafiri, kila muamala muhimu unaacha alama ya kidijitali inayoweza kufuatiliwa.
Kwa Tanzania, safari ya kujitosheleza kibajeti haitategemea tu kuongeza kodi mpya au kupanua mikopo. Itategemea zaidi uwezo wa kukusanya kikamilifu mapato yanayostahili kukusanywa tayari. Hapa ndipo umuhimu wa mifumo ya kidijitali unapodhihirika. Kadiri tunavyopunguza utegemezi wa maamuzi ya kibinadamu katika ukusanyaji wa mapato, ndivyo tunavyoongeza uwazi, uadilifu na tija.
Ni wakati sasa wa kuangalia teknolojia si kama gharama bali kama uwekezaji wenye faida kubwa kwa taifa. Kila shilingi inayowekezwa katika mifumo imara ya kidijitali inaweza kuokoa na kuongeza mabilioni ya shilingi katika mapato ya Serikali.
Ikiwa Tanzania itafanya mageuzi makubwa ya kidijitali katika ukusanyaji wa kodi, ushuru na ada mbalimbali, basi ndoto ya kujitegemea kifedha na kufadhili maendeleo kwa kutumia rasilimali za ndani inaweza kuwa karibu zaidi kutimia kuliko tunavyofikiri.
Ephrahim Bahemu anapatikana kupitia baruapepe ya [email protected]