Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dola inaposhindwa kudhibiti, Tanzania inageuka pepo ya watekaji

Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi wakati wakimtibu Edgar Mwakabela, maarufu Sativa.

Alaska ni jimbo kubwa sana Marekani, lakini lina idadi ndogo ya watu wanaoishi mbalimbali. Ripoti zinaonesha kuwa ndani ya miaka 50 iliyopita walishapotea watu zaidi ya 20,000. Yaani kwa wastani kila mwaka hupotea watu 400 bila kujulikana wameenda wapi. Mtu akipotea, familia yake hujikunyata na kulia, familia nyingine hazishituki.

Hisia za watu zinabaki kuwa ardhi mbaya ndiyo husababisha watu Alaska wawe wanapotea. Mazingira ya kijiografia yanasingiziwa kuwa ndiyo chanzo cha upotevu wa watu. Wakitokea maharamia na kuteka mtu kisha kumfanyia unyama halafu akawa haonekani, watu wanasema ni kawaida ya Alaska watu kupotea.

Australia, mwaka 2015, walitoa ripoti kuwa kila baada ya dakika 15, mtu mmoja hupotea kisha kueleza kuwa kwa mwaka, watu takriban 35,000 hupotea. Kadhalika Uingereza, mwaka 2009, walitoa ripoti kuwa watu 275,000 hupotea kila mwaka. Hata hivyo, Uingereza na Australia, tafiti zao zilionesha kuwa watu hao, hupatikana baada ya miaka kadhaa.

Kwamba watu wengi huondoka kwenye nchi za Australia na Uingereza bila taarifa kwa lengo la kupata ajira mpya kwenye mataifa mengine. Wapo ambao hubadili majina yao ya awali, hivyo kwenye takwimu za nchi kuonekana wamepotea. Wengine hubainika hawapo kupitia malipo ya bima na fedha za kujikimu. Wachache hugundulika kuwa waliuawa.

Kutokana na hali hiyo, Australia na Uingereza, wakati mwingine watu wakionekana hawapo kwenye kumbukumbu za nchi miaka kwa miaka pasipo taarifa za vifo vyao kuripotiwa, hudhani ni michezo ileile, kwa hiyo wameshazoea. Kumbe wengi wao huwa wameuawa.

Hapa Tanzania, michezo ya kuteka watu ikiendelea itafika wakati watu watazoea. Hata ukitangaza kwenye habari kuwa kuna mtu ametekwa, watu hawatashituka. Nchi haipaswi kupelekwa huko kwenye nyoyo ngumu, zenye kuona majanga ya watu ni mambo ya kawaida.

Kadiri watu wanavyopotea na kupotezwa, halafu wahalifu wa uhalifu huo hawakamatwi, ndivyo wapotezaji au watekaji wanavyopata kiburi cha mafanikio. Wanajenga kujiamini kwamba kazi yao wanaifanya vizuri kiasi kwamba hawagunduliki. Inawezekana wanakuwa kiburi kwa kuona kuwa akipotea mtu, Watanzania wanapiga kelele kisha ukimya unafuata.

Kiburi na kujiamini kwa watekaji ni kielelezo cha kufeli kwa nchi katika kutetea au kupigania usalama na uhai wa watu wake, au Watanzania kwa Watanzania wenzao. Haitakiwi kutoa nafasi hiyo ya watekaji kujiona wanafanikiwa. Ni kosa kubwa! Ndiyo maana wakati huu tunatakiwa kuwa na mshikamano katika kuhoji alipo Azory na kutaka arejeshwe.


Dola imefeli?

Mjadala sasa ni kijana Edgar Mwakabela, ambaye hutumia mtandaoni jina la Sativa. Hivi karibuni, alikutwa ametelekezwa msituni Katavi, akiwa amejeruhiwa. Moja ya majeraha ni pigo la risasi. Maelezo ni kuwa Sativa alitekwa Dar es Salaam, akapelekwa Arusha, halafu akatelekezwa Katavi msituni.

Watekaji wana nguvu kiasi gani? Wana rasilimali nyingi kiasi gani? Kumtoa mtu Dar es Salaam (Mashariki), kisha Arusha (Kaskazini), halafu kumtelekeza Katavi (Magharibi). Dar es Salaam hadi Arusha ni umbali wa kilomita 630. Arusha hadi Katavi ni sawa na kilomita 732. Hii ina maana watekaji walitembea na Sativa kwa kilomita 1,362, bila kukamatwa.

Barabarani kuna askari wa usalama barabarani na doria. Wapo maofisa wa uhamiaji. Watekaji walisafiri na Sativa kilomita 1,362, kutoka Mashariki hadi Kaskazini, kisha Magharibi, bila kukaguliwa hata mara moja? Walitumia magari gani yasiyopigwa mkono na kukaguliwa?

Kipande cha Moshi kwenda Arusha kupitia Kia, katikati kuna askari wengi wa doria. Ukiendesha gari, utaona kero kwa namna utakavyosimamishwa mara kwa mara kukaguliwa. Askari huingia hadi ndani kutafuta wanavyovijua wao. Utamuuliza askari “unatafuta nini”, atakujibu “utakiona ninachokitafuta nikishakipata”. Si utafutaji ni usumbufu.

Ajabu, askari hao ambao hufanya kazi hiyo, unajiuliza walikuwa wapi wakati Sativa akitembezwa barabarani kilomita 1,362? Yupo mtu amewahi kuniambia, doria za wanausalama barabarani hutazama aina ya magari, halafu hutafuta ulaji kuliko kulinda usalama. Ndiyo maana wafanyabishara haramu ya watu, walikamatwa wakitumia Toyota Land Cruiser 200 Series (VX), likiwa na bendera ya CCM. Ni kwa sababu magari hayo hayakaguliwi, ongeza na bendera ya chama.

Je, waliomteka Sativa ndiyo walitumia njia hiyo kumfanyisha utalii wa mateso? Walimpandisha magari ambayo ni mwiko kukaguliwa barabarani? Wahalifu wana mbinu nyingi. Wanapogundua kuna aina ya magari yasiyokaguliwa, watayatumia, hasa uhalifu wenyewe ukiwa na bajeti kubwa.

Tuweke mkazo wa swali, dola ya Tanzania imefeli kukabili matukio ya utekaji? Imepita miaka nane tangu kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane, alipotoweka. Alipotea au alitekwa? Kuna watu wamemficha au wameshamdhuru? Majibu hayo hakuna mwenye nayo, isipokuwa Mungu na malaika wake.

Ben ambaye alikuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, nini kimemsibu? Yupo wapi? Watu hawamuulizii tena. Waliopo nyuma ya kupotea kwake, bila shaka wanajipongeza kuwa walifanya kazi yao kwa umakini mkubwa. Dola imenyamaza. Polisi hawajawahi kuiridhisha jamii kama walifanya kazi ipasavyo kumtafuta Ben.

Imepita miaka saba tangu mwandishi wa habari Azory Gwanda alipochukuliwa na wasiojulikana. Miaka hiyohiyo inahusu kupotea (kupotezwa) kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye. Dola imeshindwa kutoa majibu ya mahali Kanguye na Azory walipo kwa miaka saba sasa.

Tukio la Sativa linafanana kiasi na lililompata mwanamuziki Ibrahim Mshana “Roma Mkatoliki”. Aprili 2017, taifa liliingia kwenye tafakuri ya kupotea kisha kupatikana kwa Roma Mkatoliki na wenzake watatu.

Kati ya mwaka 2016 hadi 2024, imekuwa miaka nane ya utekaji. Watu kupotea Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Miili ya watu kuokotwa fukwe za Bahari ya Hindi na mito ya Ruvu na Rufiji. Shambulio la risasi la Makamu Mwenyekiti Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu, na mengine mengi, ni mambo yanayotengeneza alama za uhalifu ndani ya miaka minane, bila wahalifu kukamatwa.