Serikali ikomeshe matukio ya utekaji

Edgar Mwakabela (27) maarufu kama 'Sativa' akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani katavi.
Katika siku za karibuni, kumekuwa na ongezeko la matukio ya utekaji na kupotea kwa watu katika mazingira ya kutatanisha, hali ambayo imeleta upya hofu na sintofahamu kwa familia husika na wananchi kwa ujumla.
Matukio haya yamezua maswali mengi kuhusu usalama wa wananchi na jukumu la Serikali na vyombo vya usalama katika kudhibiti hali hii.
Tukio la hivi karibuni la kutoweka na kupatikana kwa Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa akiwa na majeraha makubwa mwilini, limetufanya tutafakari kwa kina kuhusu usalama wa wananchi na sisi wenyewe.
Sativa alipatikana katika Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha ya na hivi sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam. Ni wazi kuwa tukio hili linapaswa kuwa kengele ya hatari kwa Serikali na jamii kwa ujumla.
Si tukio la Sativa pekee linaloibua hofu. Lipo pia la mwanachama wa Chadema, Kombo Mbwana, ambaye ameripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana, na hadi sasa hajulikani alipo. Hali hii inatishia amani na usalama wa wananchi na ni muhimu kwa Serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukabiliana na tukio moja moja na kwa ujumla wake.
Tunapokumbuka juhudi zilizofanywa na Serikali katika miaka ya nyuma kukomesha matukio kama haya yaliyotamalaki nchini wakati wa awamu ya tano, tunahimiza kuwa juhudi hizo zirejeshwe na ziwe endelevu.
Matukio haya yanaendelea kuleta taharuki kwa wananchi, lakini hatuoni kama kuna juhudi za wazi zinazofanyika kukabiliana nayo.
Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, na ni lazima litoe majibu ya maswali haya yanayoibuka kuhusu utekaji na upoteaji wa watu. Na lisiishie kutoa majibu, wakati mwingine liende hadi hatua ya kuwajibika na kuwajibishashana kwa kuwa wakati mwingine lawama zinakuwa linalalia kwake
Familia ambazo zimewapoteza wapendwa wao zinaendelea kuumia, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa matukio haya yanathibitiwa, ili kuepuka machafuko, hasira miongoni na kulipiza visasi mwa wananchi.
Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa inachukua hatua madhubuti na za haraka kukomesha matukio haya yasiyokubalika.
Matukio haya pia yanachafua taswira nzuri ya Serikali ndani na nje ya nchi, na yanaweza kuwatisha wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini.
Ni lazima Serikali ihakikishe inachukua hatua za kuimarisha usalama wa wananchi na kuleta imani miongoni mwao, ili waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu.
Tunatoa wito kwa Serikali iweke mikakati madhubuti na hatua zichukuliwe ili kukomesha matukio haya. Pia Serikali itoe taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua zinazochukuliwa na mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti matukio haya.
Wananchi wanahitaji kuona juhudi za Serikali katika kudhibiti hali hii, ili waweze kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kujiingizia kipato bila wasiwasi.
Kwa pamoja, tunapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa matukio haya yanakomeshwa na kwamba usalama wa wananchi unakuwa kipaumbele cha juu.
Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa nchi ya amani na usalama kwa kila mmoja wetu.