Sintofahamu zaidi matukio ya utekaji

Muktasari:

  • Kauli ya Kamanda Muliro imekuja siku moja baada ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime kusema jeshi hilo linaendelea kuyafanyia kazi matukio ya watu kupotea na kutekwa.

Dar es Salaam. Sakata la watu kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha, limeibua sintofahamu zaidi baada ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kusema baadhi ya watu wanaopotea ni kwa sababu ya visasi na wengine wanajipoteza.

Kauli ya Kamanda Muliro imekuja siku moja baada ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime kusema jeshi hilo linaendelea kuyafanyia kazi matukio ya watu kupotea na kutekwa.

“Kila tukio linapotokea jalada linafunguliwa na taratibu za kukusanya ushahidi na ufuatiliaji zinaanza,” alisema Misime, aliyekuwa akizungumza katika mahojiano na televisheni ya Azam jana usiku.

“Kulingana na tulivyofanya uchunguzi wetu, haya matukio kuna baadhi watu waliripotiwa wamepotea, lakini tunakuja kubaini tofauti na hivyo ila hatutasita kuchukua hatua kwa askari endapo itathibitika amehusika kwenye matukio ya aina hii, kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria,” aliongeza Misime.

Kauli hizo zinakuja wakati matukio ya watu kudaiwa kutekwa yakiibuka na hivi karibuni ndugu wa waliotoweka wakilalamika katika mikoa ya Dar es Singida, Shinyanga, Simiyu na Kigoma.


Kauli ya Muliro

Leo Alhamisi Februari 8, 2024 katika mahojiano yake na Kituo cha Redio cha Clouds FM, Kamanda Muliro alisema si kila anayepotea huwa anachukuliwa na polisi kama inavyodaiwa.

Kamanda huyo amesema miongoni mwa watu wanaosadikika kutekwa au kukamatwa na polisi, wana historia za uhalifu na wengine wana changamoto katika mazingira ya biashara au kazi.

Kuhusu tukio la mfanyabiashara Mussa Mziba aliyetekwa Desemba 7, 2023 eneo la Mikocheni, Muliro alikanusha taarifa kuwa waliomteka ni askari.

Amesema katika taarifa za awali jeshi hilo limebaini Mziba ni mfanyabiashara wa madini na kupotea kwake kunaweza kuhusisha mvutano wa kibiashara na wenzake, hata hivyo hakueleza kama kuna watu wanaoshikiliwa au kuhojiwa kuhusu sakata hilo.

Amesema jeshi hilo linakutana na kesi nyingi za watu wanaojifanya ni maofisa wa Serikali wakihusisha polisi, usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), hivyo upo uwezekano watu waliomteka Mziba walijitambulisha kuwa ni askari, lakini uhalisia haiko hivyo.

“Musa Mziba hayupo polisi na hakuchukuliwa na polisi na wala hatuna rekodi zake za uhalifu, lakini tumefuatilia na kubaini baadhi ya mambo.

“Sisi tukihitaji kumkamata mtu, hatuna sababu ya kuficha wala kusubiri usiku tumkamate gizani, tutakuja muda wowote ule tutajitambulisha na tutasema tunampeleka wapi mhusika, si kama hivyo ilivyofanyika,” amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu Mziba, Muliro alisema, “taarifa ambazo tunazichunguza, anafanya baadhi ya biashara, ikiwemo ya madini ndani na nje ya nchi na baadhi ya taarifa zisizo rasmi inadaiwa amewadhulumu watu, hili bado tunalichunguza, inawezekana watu wanafanya revenge (wanalipa kisasi).”

Amesema pamoja na taarifa hizo, Jeshi la Polisi linaendelea na wajibu wake wa kuchunguza watu hao waliomteka Mziba walimpeleka wapi na kwa sababu gani.

Hata hivyo, mke wa Mziba, Dorcas Tarimo aliyekuwepo katika kipindi hicho, alieleza kushangazwa na maelezo ya Muliro, akisema hana taarifa zozote kuhusu hatua iliyofikiwa wala kilichobainika kwenye uchunguzi.

“Hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kati ya familia na polisi, hizi taarifa kwamba mume wangu amewadhulumu watu ndiyo nazisikia hapa, siku zote nilipokuwa naenda polisi kuulizia kinachoendelea, napewa jibu kwamba uchunguzi unaendelea.

“Sasa kama kuna taarifa hizi za kuwadhulumu watu naamini mkewe nilistahili kuzipata ili labda na mimi niwe makini huenda kuna wanaoweza kunifuata au nikapata taarifa nyingine ambazo zingeweza kusaidia kwenye huo uchunguzi,” alisema.

Akijibu kuhusu hilo, Kamanda Muliro amesema, “miongoni mwa maboresho yaliyofanyika kwenye jeshi na ipo kisheria kabisa, tunatakiwa kutoa mrejesho wa mwendelezo wa taarifa za kiuchunguzi kwa waathirika na mamlaka nyingine za juu. Ikitokea hilo halijafanyika basi ni udhaifu, kwa hiyo kama Dorcas hana taarifa hizi, kuna shida mahali.

“Nilikuwa naamini anafahamu kila kinachoendelea, ndiyo maana nikalifafanua hapa, lakini kuna suala lingine, inawezekana wakati yeye hafahamu kuna wanaofahamu. Unaweza kujiona mimi ndiyo mke, lakini kuna watu wanaojitambulisha kuwa wake, huenda wao ndio wanapewa hizo taarifa,” amesema.


Tukio jingine

Kamanda Muliro amezungumzia pia taarifa za kutoweka kwa Deo Mgassa, ambaye familia yake inadai kuwa alichukuliwa na askari Oktoba 14, 2023 katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa dada wa Deo, Nilam Mgassa, kaka yake alifuatwa na askari wawili waliomchukua na kila walipojaribu kufuatilia polisi hawapati majibu.

Kuhusu hilo, Muliro alisema, “wakati hawa wanafamilia wanasema ndugu yao ametekwa na polisi, taarifa ni kwamba Jeshi la Polisi linamtafuta huyo Deo kwa kuwa alihusika kwenye tukio la uhalifu wa kutumia silaha akiwa na wenzake.

“Tukio hili lilitokea Oktoba, yeye akiwa na wenzake walimvamia dada mmoja anafanya kazi pale bandarini, wakajitambulisha kuwa ni maofisa wa TRA na Takukuru wakachukua Sh90 milioni.

“Tulifanya uchunguzi tukawakamata baadhi yao, wengine akiwemo Deo bado tunawatafuta. Sasa tunashangaa kusikia ndugu wanasema polisi wamemteka,” alisema.

Kutokana na ufafanuzi huo wa Kamanda Muliro, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuona kawaida matukio ya watu kulipiza visasi, badala yake linapaswa kuchukua hatua na kuelimisha jamii kuwa haitakiwi kuwa hivyo.

“Kulipiza kisasi ni kujichukulia sheria mkononi, polisi wanapaswa kukemea, unapokuwa na tatizo na mtu unapaswa kufuata taratibu kwa kumshtaki kwa vyombo husika, vyenyewe ndivyo vina jukumu la kuchukua hatua, si wewe kuamua kumteka au kumdhuru,” amesema.


Mapya watano wa Kariakoo

Miongoni mwa matukio yaliyoibua gumzo ni lile lililotokea Desemba 26, 2021 katika eneo la Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo vijana watano, Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abas na Rajabu Mdoe walikamatwa na watu waliokuwa wamevalia sare za polisi na hadi leo hawajulikani walipo.

Akizungumzia hilo, Kamanda Muliro alisema, “kimsingi ukiwa na taaluma ya kiuchunguzi unapopata taarifa lazima ina mambo mawili, nayo ni kuthibitisha au kukanusha. Ishu ya hao vijana ambao inasemekana walichukuliwa Kamata, tulichokiona hawakuwa wote eneo hilo, ila cha muhimu tunaendelea kufuatilia kujua wako wapi.

Maelezo hayo ya Muliro hayakutofautiana sana na yaliyotolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shuli kuhusu sakata la kupotea kwa vijana hao.

“Hili suala baada ya kuliona kwenye vyombo vya habari tuliamua kulifuatilia kwa sababu hawa waliopotea ni watu na wana haki ya kuishi. Tulifika Polisi kujua kama wamewashikilia hawa vijana, jibu lao likawa ni hapana, ila upelelezi unaendelea. Hapo ikatulazimu na sisi tufanye uchunguzi wetu kutaka kujua hawa vijana wako wapi,” amesema Shuli.

Kamishna huyo alisema uchunguzi huo ulibaini mambo kadhaa, mojawapo likiwa kwamba vijana hao watano hawakutekwa kwa pamoja katika eneo hilo la Kamata.

“Hawa vijana hawakuwa pamoja wakati wa kupotea au kutekwa kama inavyodaiwa na hili tulilithibitisha kiteknolojia, waliokamatwa pale Kamata walikuwa watatu.

“Ingawa tulipata wakati mgumu kupata ushirikiano kwa mashuhuda kutokana na woga, tulitumia mbinu zetu wakatueleza kwamba hawakuwa watano, bali watatu.

“Tulipowasiliana na familia zao kupata namba zao za simu na tukaingia kwenye mifumo ya kiteknolojia, tukabaini ni kweli hawakuwa pamoja, hao wawili walichukuliwa katika maeneo mawili tofauti jijini Dar es Salaam.

“Baadaye ikaonekana wapo sehemu moja na teknolojia ikatuonyesha kuwa simu zao zilizimwa kwenye eneo moja,” amesema.

Shuli alisema baada ya tume kubaini kuna jinai inayohusika kwenye upoteaji wa vijana hao na kwamba hawako mikononi mwa polisi, waliliacha suala hilo kwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo linahusika na ufuatiliaji wa matukio ya aina hiyo.

“Chombo kinachopaswa kuchunguza matukio ya uhalifu ni Jeshi la Polisi, tulichofanya ni katika kutimiza jukumu letu la kutetea haki ya kuishi, hivyo tuliamua kuchunguza kujua wako wapi na uchunguzi wetu ukatuthibitishia pasi na shaka kwamba vijana wale hawako mikononi mwa polisi.

“Taarifa zote tulizozipata katika uchunguzi wetu tukaziwasilisha Jeshi la Polisi ili waendelee nazo kwa kuwa zinaweza kuwa na msaada katika uchunguzi wanaoendelea nao katika jalada hilo,” amesema Shuli.




Kauli tofauti

Mara baada ya maelezo hayo, gazeti hili lilizungumza na Longili Martin, kwa niaba ya wazazi waliopotelewa na vijana hao, aliyesema Polisi wamekuwa wakibadilibadili kauli, kila wakikutana nao wanaeleza vitu tofauti na wanavyovieleza kwenye vyombo vya habari, jambo ambalo alisema haliwafurahishi.

“Ni jambo lisilopingika Polisi wameshiriki kuteka watoto wetu, sasa huyo Muliro anasema hana ushahidi kama walitekwa maeneo ya Kamata, tulivyoongea naye hakusema maneno hayo…kimsingi ni vigeugeu, hatukubali,” amesema.

Martin, ambaye ni baba mzazi wa Edwin Kunambi alisema wameshafuatilia mazungumzo yake na kutambua ni kigeugeu ndiyo, maana hata wakitafutwa kwenye simu hawapatikani “wametublock”, wakati mwanzoni walikuwa wanatupa ushirikiano.

“Tunakusudia kwenda kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda na Rais Samia Suluhu Hassan labda wanaweza kutusikiliza kwa sababu tulishakwenda Dodoma kukutana na Mkuu wa Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hatuoni msaada,” amesema.

Alisema wanachoamini watoto wao wametekwa na jeshi hilo kwa sababu zao na waliohusika wanawajua ila wanaficha taarifa kwa kuwa wanajua kinachoendelea.

Nyongeza na Tuzo Mapunda