Ahadi ya Katiba mpya ilivyowakosha wadau
Muktasari:
- Mbali na rekodi mpya, baadhi ya wadau wa sheria na wanazuoni wa sayansi ya siasa, wamesema utekelezwaji wake utatoa tafsiri halisi ya kuwa kilio sasa kimesikika.
Dar es Salaam. Ahadi ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ya kuandaa mazingira ya mchakato wa Katiba mpya ndani ya siku 100 za uongozi wake, imeelezwa kuwa ikitekelezwa na mchakato ukaanza, itakuwa miongoni mwa mambo yatakayomweka kiongozi huyo katika rekodi mpya.
Mbali na rekodi mpya, baadhi ya wadau wa sheria na wanazuoni wa sayansi ya siasa, wamesema utekelezwaji wake utatoa tafsiri kuwa licha ya kilio hicho kuwa cha muda mrefu, hatimaye CCM husikiliza.
Hadi kufikiwa kwa mchakato huo, amesema ataanza na kushauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda tume ya kuanzisha mazungumzo ya maridhiano na upatanishi.
"Tutaendeleza mashauriano na wadau wa siasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda tume ya kuanzisha mazungumzo ya maridhiano na upatanishi na kuandaa mazingira ya kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya," alisema mgombea huyo alipokuwa Dar es Salaam katika uzinduzi wa kampeni.
Walichosema wadau
Akizungumzia hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Fulgence Massawe amesema hana mashaka kuhusu utekelezwaji wa ahadi hiyo.
Anasema kinachomwondolewa shaka ni kuwa ahadi hiyo haikutoka kinywani kwa mgombea wa CCM pekee, bali ni sehemu ya mambo yaliyoandikwa katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Hata hivyo, ameeleza hatua hiyo ya Samia, itaongeza wigo wa utawala wa sheria na atakuwa amekata kiu ya makundi mbalimbali ambayo mara nyingi yamesikika yakidai Katiba mpya.
Amesema hatua hiyo itamfanya mgombea huyo aingie katika rekodi ya pekee ya kukwamua jambo lililoshindikana kutekelezwa na awamu mbalimbali za Serikali.
“Mwaka 2014 mchakato wa Katiba mpya ulikwama katika hatua za mwisho baada ya kupatikana Katiba Inayopendekezwa na kiongozi aliyefuata alisema si kipaumbele chake. Lakini Samia ameahidi kuukwamua atakapochaguliwa, hii itamfanya awe katika rekodi ya kipekee,” amesema.
Wakili Massawe amesisitiza kwa kuwa katiba mpya ni dai la muda mrefu la wadau wa kada mbalimbali hasa siasa, kulitekeleza kutamfanya mtekelezaji awe kielelezo cha usikivu wa matakwa ya wananchi wake.
Amesisitiza kwamba anaiona ahadi hiyo kuwa hai, kwa sababu imebebwa ndani ya ilani ya uchaguzi ya chama husika, pia kuna nia ya dhati ya kutekelezwa hilo, ingawa itahitaji zaidi ya siku 100 kukamilisha.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema mchakato wa Katiba mpya ulikwamishwa na utashi wa kisiasa, lakini ahadi iliyotolewa na Samia ni kielelezo cha kuwepo utashi huo.
“Kama utashi wa kisiasa upo, sioni chochote cha kukwamisha mchakato huo,” amesema Dk Kabobe.
Amesema Katiba mpya kimekuwa kilio cha makundi mengi ikiwemo ndani ya CCM yenyewe na manufaa yake ni makubwa kwa Taifa.
“CCM kukubali sasa kuweka katiba mpya kama kipaumbele ndani ya siku 100, ni dhahiri kuwa nacho sasa kinahitaji kufanya mabadiliko ndani yake, maana Katiba mpya itachochea mageuzi makubwa,” amesema.
Naibu Kamishna wa Katiba na Sheria wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Aron Semi amesema kwa kuwa kumekuwa na mijadala kuhusu suala hilo, ni muhimu kwa mgombea huyo wa chama tawala kuonyesha utashi wa kulitekeleza.
“Katiba tunayoitumia ya mwaka 1977 ambapo hadi sasa ni miaka zaidi ya 40 na sheria zinatakiwa kuendana na mazingira ya wakati husika. Hivyo kuifufua ni suala zuri,” amesema.
Historia ya Mchakato wa Katiba
Tanzania ilianza mchakato wa Katiba mpya mwaka 2011 chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Tume ya Jaji Joseph Warioba iliundwa, ikakusanya maoni ya wananchi zaidi ya milioni 1.4 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Ripoti hiyo ilizaa Rasimu ya kwanza, ya pili na Katiba Inayopendekezwa, iliyopewa sifa kwa kugusia masuala ya msingi kama ugatuzi wa madaraka, uwajibikaji wa viongozi, mgawanyo wa rasilimali na haki za makundi maalumu.
Kwa kuahidi kurejesha kuweka mazingira ya mchakato huo ndani ya siku 100, Dk Samia ameonyesha kipaumbele cha haraka katika masuala ya kidemokrasia.