Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zitto atahadharisha Watanzania na watu wanaosaka ubunge

Kigoma/Katavi. Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka Watanzania kuwa makini na watu wanaosaka ubunge akisema imefikia hatua wachekeshaji, wasanii na watangazaji wanautaka ubunge.

“Bunge linadogoshwa, kwamba limekuwa eneo la machawa au la uchekeshaji au ni la mtu yeyote anayetaka kwenda,” amesema Zitto.

Amesema Bunge ni chombo cha kutunga  sheria na linaisimamia Serikali na ndilo ambalo linawawakilisha watu, hivyo watu wasichukulie kwamba ni chombo cha kila mmoja anaweza kufanya vile atakavyo, bali lipewe hadhi yake.

“Ukilifanyia utani Bunge, utakuwa umefanya utani na uhai wa Taifa, ili kuhakikisha mhimili huu haufanyiwi utani, watu wa Tabora pamoja na machungu mliyonayo, hasira mlizonazo au kukata tamaa, pigeni moyo konde twendeni kwenye uchaguzi mkachague watu sahihi," amesema Zitto.

Amewataka wananchi wa Tabora na Watanzania kushiriki uchaguzi kwa kuichagua ACT Wazalendo ili kurejesha thamani ya kura zao na hatimaye kupata Bunge litakaloibana Serikali kwa kupitia mikataba, kuzuia wizi  na kuzuia sheria mbovu zisipite bungeni.

“Hii ni changamoto kwa vijana wetu, tusikubali kwa miaka mingine mitano ya kukaa na Bunge kama lililomaliza muda wake. Njia pekee ya kuzuia hilo ni kwenda katika uchaguzi kupambana," amesema Zitto.

Chama cha ACT Wazalendo ambacho kinaendelea kuchanja mbuga katika ziara zake kwenye mikoa mbalimbali nchini, kinaelezea pia sababu za kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku kikiuelezea umma kwa nini kinastahili kuchaguliwa kama chama mbadala kushika dola.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa na chama hicho za kushiriki uchaguzi ni kukabili umaskini wa wananchi, jambo ambalo kinadai watawala wameshindwa kulitimiza, licha ya kuainishwa katika Ibara ya 9(i) ya Katiba.

Katikati ya msimamo huo wa ACT Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaendelea na ajenda yake ya kuzuia uchaguzi iwapo hakutafanyika mabadiliko ya kisheria 'no reforms no election.'

Hata hivyo, ACT Wazalendo inasisitiza sababu za msimamo wake huo wa kushiriki uchaguzi, ni rejea ya historia inayoonyesha hakukuwahi kutokea mafanikio ya kukabiliana na utawala unaokiuka haki za raia kwa kususia uchaguzi.

Kimekwenda mbali zaidi na kurejea historia enzi za Serikali ya kikoloni, iliyokuwa ikiwanyima haki Watanganyika, lakini wazee hawakususa, badala yake walishikamana na kushirikiana na hatimaye kuwashinda wakoloni na Taifa likawa huru.

Chama hicho leo, Ijumaa Julai 4, 2025 kinatimiza siku ya nne za ziara yake ya Operesheni Majimaji Linda Kura Yako, inayolenga kuuelezea umma katika mikoa mbalimbali kuhusu msimamo wake wa kushiriki uchaguzi na sababu za kuingia kwenye mchakato huo.


Umaskini

Akiwa mkoani Katavi, Kiongozi mstaafu wa chama hicho, amewasihi Watanzania wawapime watawala kwa kuangalia kwa kiwango gani wametimiza lengo la kupunguza umaskini kwa Watanzania.

"Tumefanya uchaguzi mwaka 2020 na mwingine tutafanya mwaka huu, tujiulize katika utekelezaji ibara ya 9 (i) Serikali iliyopo madarakani imefanya nini. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 idadi ya wananchi maskini Tanzania walikuwa milioni 14,” amesema Zitto.

Zitto amedai sera za Chama cha Mapinduzi bado haziondoi umaskini wa Watanzania, ndio maana ACT Wazalendo kinawaomba wananchi kuwaunga mkono kukiondoa chama hicho tawala.

"Bunge lililoisha limeshindwa kuhoji Serikali kuhusu hili kwa sababu lilikuwa la chama kimoja. Kipindi ambacho umaskini ulipungua ni pale ambapo kulikuwa na wabunge wa upinzani na demokrasia imetamalaki, ambao walikua wakiihoji Serikali," amedai Zitto.

Kwa mujibu wa Zitto, mikoa kanda ya magharibi ikiwemo ya Tabora, Rukwa, Kigoma na Katavi ndio inayoongoza kwa umaskini na kuna tofauti kubwa kati ya walioanacho na wasionacho.

Mwaka 2024 akihojiwa na TBC Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo alisema katika miaka 25 ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo (2000-2025) kiwango cha umaskini kimepunguzwa hadi kufikia asilimia 26, na lengo ni kumaliza katika miaka 25 ijayo.

"Kama tumeweza kupunguza hadi kufikia asilimia 26, tunataka kuona hii asilimia 26 kuelekea mwaka 2050 tuweze kuondoa kabisa," alisema Profesa Mkumbo huku akiongeza kuwa suala la kuondoa umaskini ni la nchi zote duniani kwani hakuna iliyofanikiwa kwa asilimia 100.

Katika hotuba yake Zitto, amesema hali ya umaskini iliyopo wananchi watakwenda nayo katika uchaguzi, ndio maana ACT Wazalendo inawaomba Watanzania wakiunge mkono ili kukomesha changamoto hiyo, na wasipofanya hivyo Bunge litarudi lilelile la CCM pekee.


Ilani ya uchumi kukamilika karibu

Akiwa wilayani Kibondo katika Mkoa wa Kigoma, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amesema wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya ilani ya uchaguzi na kwamba itakuwa tumaini la ustawi wa kiuchumi na maisha bora kwa Watanzania.

"Tunaandaa ilani ambayo itakuwa na sera zitakazokuwa tumaini jipya la ukombozi wa kiuchumi kwa Taifa. Tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha," amesema.

Akisisitiza sababu za kwa nini chama hicho kinashiriki uchaguzi, Dorothy amesema wanaamini ndilo jukwaa la kuyasemea makundi mbalimbali ya Watanzania.

"Tunashiriki ili kuhakikisha tunautumia uchaguzi kama jukwaa la kumsemea Mtanzania na kueleza sera zitakazomnufaisha. Jukwaa la kumsemea bodaboda, mamalishe ambaye kila siku anakimbizwa kunyang'anywa au kudaiwa rushwa," amesema.

Amesema ziara hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwahamasisha wananchi wajibu wao wa kupiga kura na kuzilinda ipasavyo.

Amesema katika msimamo huo wa kushiriki uchaguzi, chama hicho kinapendekeza kufuatwa sheria katika usimamizi wa uchaguzi na mawakala wa upinzani waachwe huru kufanya kazi zao.


Thamani ya uraia ipo kwenye nguvu ya kura

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita amesema hatua ya wananchi kupokwa haki na nguvu ya kura yao, imesababisha wengi wapoteze ari ya kushiriki uchaguzi, kiasi cha wengine kuona hakuna haja ya kwenda kupiga kura.

Ingawa zipo sababu za msingi za wananchi kupoteza ari hiyo, amesema historia inaonyesha hakuna mafanikio yaliyopatikana kwa kupoteza mwamko wa kushiriki uchaguzi.

Mchinjita, amesema chama chake kinatambua changamoto za kisheria na haki ndani ya mchakato wa uchaguzi, lakini hawaoni sababu ya kutoshiriki kwa sababu kufanya hivyo, kunawafaidisha watawala.

"Watu wameanza kujadili katika nchi hii kwamba bora tuwaachie CCM wenyewe, kwa sababu uchaguzi umepoteza thamani na kura ya raia imepoteza nguvu yake," amesema.

Mitazamo waliyonayo wananchi kuhusu uchaguzi, amesema ndiyo iliyokifanya chama hicho kione sababu ya kuja na operesheni Majimaji itakayohusika na kuwahamasisha wananchi baada ya kupiga kura wazilinde.

"Tumeiita operesheni hiyo kwa jina la Majimaji kuwakumbusha enzi za wazee wetu kuwa iliwahi kuwepo Serikali ya kikoloni isiyotenda haki, lakini wazee wetu walipigana kuhakikisha wanaishinda na walishinda," amesema.

Amesema lazima kurejea historia ya nchi ya kuunganisha nguvu za raia kukabiliana na udhalimu uliokuwa inafanyika.

Amesema mapambano hayo, yalitokana na ukweli kwamba Serikali ya kikoloni haikuwa imepewa ridhaa ya wananchi, badala yake ilijiweka yenyewe madarakani.

Kada wa chama hicho, Emmanuel Ntobi amesema kuna umuhimu wa vyama vya upinzani kuunganisha nguvu kufanikisha kuiondoa CCM madarakani.

Amesema alipokuwa Chadema alisikia ajenda mbalimbali na hatimaye ukatoka msimamo wa kususia uchaguzi, jambo lililomfanya kubadili uamuzi na hatimaye kujiunga na ACT Wazalendo.

Ntobi amesema sio dhambi wala usaliti kuhamia chama kingine, ilimradi tu, shabaha ya kufanya hivyo iwe ni kufuata misingi ambayo pengine imepotea kutoka pale ulikokuwa.

Kwa upande wa Wakili Peter Madeleka, amesema raia wana wajibu wa kwenda kupiga kura kwenye uchaguzi wa mwaka huu kwa sababu ni haki yao.

"Tunatakiwa kwenda kutimiza haki yetu ya kuwachagua viongozi tunaowataka. Ukishapiga kura yako Oktoba, hakikisha unailinda," amesema.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, amesema ni uchaguzi ndiyo mchakato unaomwezesha mwananchi apate kiongozi anayemtaka.

Ameeleza ni muhimu kuhakikisha wanapatikana viongozi watakaoweza kusimama mbele ya wananchi na akapaza sauti kuiambia mamlaka husika kwamba kuna changamoto fulani.

Waziri Kivuli wa Fedha wa chama hicho, Kiza Mayeye amesema ziara hiyo si maagizo bali kuzungumzia changamoto za Watanzania kwa sababu siasa ndio maisha na wanasiasa wanaohusika kupanga mipango ya maendeleo.

"Hapa Katavi mmebarikiwa ardhi yenye rutuba ya kilimo, lakini bado mkoa huu wananchi wana hali ya umaskini. Licha ya kulima bado kilimo hakijawanufaisha,"

"Siasa ni maisha lazima ifike mahali tuseme tunataka mabadiliko, wakati wa mabadiliko ndio sasa, tuungane tukaitoa CCM madarakani ili kubadilisha maisha ya Watanzania," amesema Mayeye ambaye ni mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma.

"Watu wa Katavi tuungane katika safari ya mabadiliko, msiogope twendeni tukapige kura atakayeshinda ndiye atakayetangazwa. Kigoma tutasimama imara atakayeshinda ndiye atakayetangazwa," amesema Mayeye ambaye aliwahi kuwa mbunge wa viti maalumu 2015/ 2020.