Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wiki ya hekaheka mchakato majimboni, Rais Samia akielekea kulihutubia Bunge

Muktasari:

  • Sambamba na hilo, ni wiki ambayo Rais Samia Suluhu Hassan atalihutubia Bunge la 12 na kufungua pazia la maandalizi ya kulipokea Bunge la 13 mwishoni mwa mwaka huu.

Dar es Salaam. Ni wiki ya hekaheka katika siasa nchini. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na matukio makubwa katika medani za siasa yanayotarajiwa kufanyika.

Wiki hii, Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafungua pazia la uchukuaji na urejeshaji fomu kwa makada wake wanaotaka kuwania nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi.

Sambamba na hilo, wiki hii ndiyo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan atalihutubia Bunge la 12 kabla ya kutangaza tarehe rasmi ya kuvunjwa kwake na kufungua pazia la maandalizi ya kulipokea Bunge la 13 mwishoni mwa mwaka huu.

Tayari viongozi waandamizi katika nafasi za ukuu wa mikoa, wilaya na wakuu wa taasisi wameshawekwa kando katika uteuzi, huku kukiwa na tetesi kuwa wanakwenda kugombea majimboni.

Mfululizo wa yote hayo yaliyotokea na yanayotarajiwa kutokea ndani ya wiki hii ya mwisho ya Juni 2025, ndiyo unaothibitisha kuwa ni wiki ya hekaheka katika medani za siasa nchini.


Rais Samia kulihutubia Bunge

Ijumaa, Juni 27, 2025, Rais Samia atalihutubia Bunge la 12 linalongozwa na Spika, Dk Tulia Ackson, hotuba itakayolihitimisha Bunge hilo, ikiwa ni ishara ya maandalizi ya Bunge lijalo litakaloanza Novemba 2025, baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu Oktoba.

Mara ya kwanza, Rais Samia alilihutubia Bunge hilo Aprili 22, 2021, lililopokuwa likiongozwa na Spika Job Ndugai, ikiwa ni miezi michache baada ya kushika wadhifa huo Machi 19, 2021, kutokana na kifo cha mtangulizi, Dk John Magufuli, Machi 17, 2021.

Wakati uhai wa Bunge la 12 ukielekea ukingoni, hali ya kisiasa katika majimbo mbalimbali nchini ni kwa moto na hii inachagizwa na wabunge ‘kuhaha’ ndani na nje ya mhimili huo wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali, kuhakikisha wanarejea tena mjengoni.

Katika majimbo mbalimbali, makada hususan wa CCM wanapiga jalamba wakisubiri dirisha la kuchukua na kurejesha fomu za udiwani, ubunge na uwakilishi kufunguliwa saa 2:00 asubuhi ya Juni 28, 2025, ndani ya chama chao.

Duru za siasa kutoka majimboni zinaeleza kuwa kuna fukuto kubwa huko linalochagizwa na makada wakiwamo waliokuwa wakuu wa mikoa, wilaya, wakuu wa taasisi na wakurugenzi wanaozitaka nafasi hizo.

Wengine wanaojipanga kurejea kwa kishindo kwenye mchakato huo wa kuomba ridhaa ya chama chao ni baadhi ya waliokuwa wabunge kwa nyakati tofauti, na wengine waliowahi kushika nyadhifa za uwaziri na unaibu mawaziri.

Wabunge wengine wa sasa wanakwenda kukutana na mchuano mkali hasa ikizingatiwa mchakato wa kura za maoni mwaka 2020 ulivyokuwa; wengi walioongoza, majina yao hayakurudi na waliorudi na kuchaguliwa kuwa wabunge walikuwa wameshika nafasi za pili, tatu au nne.


Kinachoendelea majimboni

Wakati kipenga cha kuchukua na kurejesha fomu kikisubiriwa Juni 28 hadi Julai 2, mwaka huu, hali ya baadhi ya majimbo hivi sasa ni mwendo wa hekaheka, mtifuano na tambo za hapa na pale kwa baadhi ya wagombea.

Awali, mchakato huo kwa CCM ulikuwa uanze Mei mosi hadi Mei 15, 2025, lakini utaratibu ulianza kuleta athari za ushiriki wa wabunge katika vikao vya bajeti katika Bunge la bajeti lililokuwa likiendelea wakati huo.

Mkazi wa Sengerema mkoani Mwanza, Frank Masanja amesema kwa wiki kadhaa kumekuwa na mishemishe zisizoisha kwa wagombea wanaosaka ubunge katika majimbo ya Buchosa na Sengerema mkoani humo.

“Hawa jamaa wakiwa na wapambe wao wanapita kwa wajumbe usiku ili kuzungumza na wajumbe kwa lengo la kuwaomba wawaunge mkono. Baadhi yao wanatamba kuwa watawaondoa wabunge waliopo wakidai wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

“Wabunge waliopo wao wanajibu mapigo wakisema wametimiza wajibu wao inavyotakiwa na kazi zinaonekana, hivyo wana kila sababu za kuusaka ubunge kwa mara nyingine,” amesema Masanja.

Hali hiyo ipo pia katika baadhi ya majimbo ya Mkoa wa Tanga, ambapo wagombea wamekuwa wakijipitisha nyakati za usiku wakiambatana na wapambe wao kwa lengo la kuonana na wajumbe ili kuyajenga.

Ni mwendo wa kitimutimu katika majimbo ya mkoa huo, na rafu za kimyakimya zinazofanywa na wanaosaka uongozi hasa ubunge.

Mathalani, inadaiwa kuwa siasa za ubunge wa Tanga Mjini zimesababisha hivi karibuni kuhamishwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga Mjini.

Ingawa CCM wanasema ni uhamisho wa kawaida, lakini taarifa zilizopo zinadaiwa amehamishwa kutokana na hali ya kisiasa hasa ya ubunge wa Tanga Mjini.

Inadaiwa katibu huyo amepelekwa Wilaya ya Bagamoyo na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Katibu wa CCM Mtama, wilayani Lindi.

Mkoani Kilimanjaro, baadhi ya wanaosaka ubunge wamekuwa na mbinu tofauti wanayoitumia katika kuhakikisha wanaungwa mkono na wajumbe pamoja na wananchi katika baadhi ya majimbo, ikiwemo Moshi Mjini na Vijijini.

Joshua Kimario, amesema baadhi ya wanaotaka kugombea hasa ubunge wamekuwa karibu na wananchi kwa kushiriki matukio ya kijamii ikiwemo harusi, misiba, hata pale maafa yanapojitokeza, mathalani mafuriko.

“Hivi karibuni kulitokea mafuriko, walikuja kwa wingi wakitoa misaada ya vyakula kama sukari, mchele, maziwa, mitungi ya gesi,” amesema Kimario.

Hata hivyo, Kimario amesema wakati hayo yakiendelea, wapambe wa wagombea ‘machawa’ wamekuwa wakipigana vikumbo na kurushiana vijembe kupitia makundi ya sogezi, huku kila mmoja akitamba mgombea wake ni bora.


CCM yapiga marufuku

Wakati hayo yakiendelea, CCM kupitia Katibu Mkuu wake, Dk Emmanuel Nchimbi, kimesitisha matukio yote yanayohusisha wanaopiga kura za maoni, ikiwemo ziara, semina na makongamano.

Katika mchakato wa uchukuaji wa fomu utakaoanza Juni 28, 2025, kunatarajiwa kuonekana sura mpya za waliokuwa wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa taasisi na halmashauri wakiwania ubunge katika majimbo mbalimbali.

Ingawa miongoni mwao walishawahi kuwa wabunge wa majimbo na viti maalumu, lakini katika uchaguzi wa mwaka 2020 waliangukia pua kwa kushindwa kura za maoni, huku wengine wakienguliwa na Kamati Kuu.

Hatua ya juzi, Juni 23, 2025, ya Rais Samia kutangaza kuwaweka kando baadhi ya wakuu wa mikoa, wakuu wa taasisi na halmashauri, inaongeza joto na presha kwa wabunge wa sasa wanaotetea tena nafasi hiyo.

Rais Samia alifanya uteuzi na kuwahamisha watendaji wake, ambapo amewaweka kando wakuu wa mikoa watano, akiwemo Paul Makonda wa Arusha.

Mbali na Makonda aliyeachwa, wengine na mikoa yao kwenye mabano ni Peter Serukamba (Iringa), Thobias Andengenye (Kigoma), Dk Juma Homera (Mbeya) na Daniel Chongolo (Songwe).

Taarifa zilizopo zinaeleza kuwa vigogo hao waliowekwa kando huenda wakawania majimbo mbalimbali likiwemo la Namtumbo (Ruvuma), Kigoma Kaskazini (Kigoma), Makambako (Njombe).