Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu: Watanzania acheni kujadili kiwango cha deni, angalieni mafanikio

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza bungeni alipokuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma leo Juni 24, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Hadi sasa deni la Serikali linatajwa kufikia Sh107.7 trilioni kiwango ambacho baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wanakitaja kuwa cha juu.

Dodoma. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amewahimiza Watanzania kuacha kujikita katika mijadala kuhusu kiwango cha deni la Taifa badala waelekeze kwenye matumizi ya fedha zilizokopwa na mafanikio yaliyopatikana.

Hadi sasa deni la Serikali linatajwa kufikia Sh107.7 trilioni kiwango ambacho baadhi ya wanasiasa na wachambuzi wanakitaja kuwa cha juu.

Akijibu hoja za wabunge  waliochangia kuhusu Mpango wa Taifa wa Maendeleo na Bajeti Kuu ya Serikali leo Jumanne Juni 24, 2025, Dk Mwigulu amekemea tabia ya kuwatisha Watanzania wakiwamo watoto kwamba wanakuja kudaiwa.

Waziri amesema bado Tanzania ina nafasi kubwa kuhusu deni hilo lakini pia taasisi za kimataifa zimeitaja kuwa miongoni mwa nchi zinazokopa fedha na kuzifanyia kazi kwenye miradi moja kwa moja wakati zipo baadhi ya nchi zinakopa na kupeleka katika matumizi mengine.

“Mheshimiwa Spika, Serikali haikopi kwa ajili ya malipo ya mishahara, uendeshaji wa magari au matumizi ya kawaida, bali inalenga kuinua miradi ya kimkakati yenye tija kwa Taifa,” amesema Dk Mwigulu.

Kiongozi huyo ameitaja baadhi ya miradi ikiwamo barabara ya kutoka Dodoma kwenda Manyara hadi Arusha na kutoka Singida kwenda Arusha ambazo fedha zilikopwa Benki ya Afrika na kuokoa muda uliokuwa ukitumika kwenye safari.

Hata hivyo, amesema si kila mradi mkubwa uliojengwa Tanzania umetokana na mkopo bali mingine ni  makusanyo ya ndani ukiwamo mradi wa Daraja la JP Magufuli  na Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Waziri amesema baadhi ya watu wameanza kueneza taswira potofu kwamba, Serikali inakopa ili kulipa gharama zisizo na tija, jambo ambalo sio ukweli badala yake mikopo inachukuliwa ili kukamilisha miradi iliyopo na si kuanzisha mipya bila mpango.

Amesema hadi sasa kuna miradi 1,112 inayotekelezwa kimkakati na hakuna mradi unaokwenda kwa kusuasua badala yake inajengwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.

Waziri pia amewataka watu wanaojadili kuhusu suala la mkopo waache kufanya hivyo kwa kuwa haina maana kujadili kiwango cha fedha badala yake wajadili fedha zilizokopwa zilielekezwa katika matumizi gani.

Dk Mwigulu amesisitiza kuwa, kuna tofauti kati ya deni la Taifa na la Serikali, akisema hayo ni maeneo tofauti licha ya kuwa yanalenga kuchechemua uchumi na kuibua miradi.

“Tunaposema deni la Taifa tunajumuisha na zile taasisi na kampuni kubwa zinazokopa kwa ajili ya shughuli zao, lakini deni la Serikali ni fedha zinazokopwa kwa ajili ya kuelekeza kwenye miradi mikubwa pekee,” amesema Waziri.

Dk Mwigulu amesema Tanzania inaaminiwa na inaweza kukopa kutoka kwenye benki ili kuendeleza shughuli za miradi na itaendelea kulipa huku miradi ikiwa imekamilika.

Ametolea mfano kuwa, Serikali inaposhindwa kusonga mbele na kutekeleza mradi kwa rasilimali zilizopo, ndipo inatafuta mikopo yenye masharti nafuu kutoka wadau kama Benki ya Afrika (AfDB) na Benki ya Dunia.

Ametaja kuwa malengo ni kuhakikisha shughuli zinazohusishwa na maendeleo zinaendelea bila kusitishwa, na ghala la deni linaweza kuharakisha ukuaji wa uchumi kwa kuwa, Serikali inapokusanya itaendelea kulipa huku miradi ikiwa imekamilika.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kukua hata katika kipindi ambacho mataifa mengine yamekuwa yakipita kwenye msukosuko.

Profesa Mkumbo ameliambia Bunge kuwa sababu ya kuendelea kukua  uchumi wa Tanzania ni kutotegemea sekta moja kama ambavyo baadhi ya nchi wanategemea uchumi katika mlengo mmoja kama ni zao au kitu kingine ambacho kikiyumba kidogo hali inakuwa ngumu.

“Sisi tunategemea uchumi kupitia vitu vingi, kuna sekta tofauti tofauti ambazo zinasaidia kuongeza mapato tofauti na wenzetu wengine, hali hii imefanya tuendelea kuwa Taifa la pekee ambalo haliyumbi kwenye uchumi badala yake tunazidi kusonga mbele,” amesema Profesa Kitila.

Awali, akichangia kwenye hoja hizo, Naibu Waziri wa Fedha Hamad Hassan Chande amesema mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) yatakayokidhi vigezo vya msamaha yatapatiwa bila hofu.

Chande amesema Serikali imesikia kilio cha wabunge kutoka katika kundi hilo isipokuwa ni muhimu kutazama msamaha kwa wanaofikia vigezo vilivyowekwa kwa kuwa, Serikali itawatambua na kuwaweka kwenye kundi la msamaha.


Uhimilivu wa deni

Juni 13 mwaka huu, kampuni inayojihusisha na kufanya tathmini ya nchi kukopesheka katika masoko ya mitaji ya kimataifa ya Fitch Ratings, imeithibitisha Tanzania kuwa katika daraja ‘B+’ ikiwa na mtazamo thabiti, jambo linalodhihirisha kuendelea imani ya kimataifa juu ya misingi ya uchumi wa Tanzania na juhudi zake za mageuzi katika sera zake. 

Taarifa ya Fitch Rating ineeleza kuwa, uthibitisho huo umechangiwa na ukuaji imara wa Pato la Taifa (GDP), mfumuko mdogo wa bei, usimamizi mzuri wa sera za uchumi pamoja na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa. 

Kwa mujibu wa Kampuni ya Fitch, uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, ukichochewa na sekta za kilimo, madini, utalii na uwekezaji katika miundombinu kama mradi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere.


Jambo lingine linaloibeba Tanzania ni mfumuko wa bei, ambao umebaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5, na kwa kuboresha usimamizi wa fedha za umma, madeni yaliyokuwa yakisubiri kulipwa kwa wazabuni na marejesho ya VAT, yamepungua kutoka asilimia 1.2 ya GDP mwaka 2022 hadi asilimia 0.4 kufikia Machi 2025.

Fitch pia inaeleza kuwa, kupitia matokeo hayo, wanatarajia mwelekeo wa sera kuendelea kuwa thabiti, jambo litakaloendelea kuwavutia washirika wa maendeleo na wawekezaji nchini.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, Tanzania imeweza kudumisha akiba ya fedha za kigeni,  hadi Machi 2025 ilifikia Dola 5.7 bilioni za Marekani, sawa na uwezo wa kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi 4.2. 

Aidha, Fitch inaeleza kuwa, kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni, kuendeleza utekelezaji mzuri wa sera za uchumi na kuendelea kuvutia wawekezaji wa sekta binafsi kunaweza kuiwezesha Tanzania kupandishwa daraja zaidi.