Wasira amtumia salamu Martha Karua

Muktasari:
- Amesema Tanzania inaheshimu utawala wa sheria na haina hofu na chama chochote cha upinzani.
Dodoma. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amemjia juu mwanasiasa na mwanasheria wa Kenya, Martha Karua, akimtaka aache kujipima uzito na chama hicho, akisema hakina hofu na chama chochote cha upinzani na hakiwezi kuingilia majukumu ya Mahakama au Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Wasira ametia mguu kwenye sakata hilo, baada ya Aprili 24, 2025, Martha kuishauri Serikali ya Tanzania kuingia kwenye meza ya mazungumzo na Chadema, kwani madai yanayolalamikiwa na chama hicho kuhusu mifumo ya uchaguzi ni ya msingi.
Msingi wa hoja ya Martha ni baada ya kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, anayeshtakiwa kwa makosa ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni.
"Lazima uchaguzi ufanyike kwa uwazi na usawa, na si chama kimoja kuweka masharti ambayo yanawapatia kipaumbele washinde bila kuchaguliwa na wananchi. Tunawaheshimu wenye madaraka lakini nao waheshimu wananchi," alisema Martha Karua.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Dodoma Mjini jana April 25, 2025, akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 - 2025 mkoani Dodoma.
Kulingana na maelezo ya Martha, alidai nchi za Uganda, Kenya na Tanzania kumekuwa na ukanyagaji wa sheria na haki za binadamu.
Akizungumza Ijumaa, Aprili 25, 2025, na wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika viwanja vya Nyerere Square, ikiwa ni muendelezo wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, Wasira amesema Tanzania inaheshimu wageni kuja nchini, lakini wasitumie nafasi hiyo kuingilia mambo ya ndani.
"Tanzania hatuvurugi amani ya Afrika Mashariki isipokuwa tunaendesha mambo yetu kwa amani, na salamu ninazompatia ni kwamba aache kujipima na CCM. CCM ni chama kikubwa Afrika kinachoanza na nyumba kumi kumi.
"CCM haina hofu na chama chochote, lakini hatuwezi kuingilia kazi ya Mahakama na hatuwezi kuingilia shughuli za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwa ni vyombo vyenye mamlaka. Lakini kama ni mjuzi hivyo, ashughulike na mambo ya Kenya," amesema.

Mwanasiasa na mwanasheria wa Kenya, Martha Karua.
Kulingana na Wasira, kama anaona chama chake ni kidogo na anataka umaarufu, basi aangalie mataifa mengine ya Afrika yenye migogoro, akatatue kama ilivyo Sudani ya Kusini.
"Akishindwa, arudi nyumbani akaendeshe chama chake ambacho sera zake hazijulikani. Atuache Tanzania tuchaguane kwa utaratibu wetu. Hata mimi mwenyewe nazungumza hapa, nilichaguliwa kwa kishindo katika nafasi hii ndani ya chama. Naam, dozi hii inamtosha," amesema.
Amesema katika uchaguzi uliopita Kenya, Martha alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga, walikuwa wanalalamikia uamuzi wa tume yao ya uchaguzi, wakaenda hadi Mahakama Kuu, lakini hawakupata kitu, akaenda Mahakama ya Afrika Mashariki na alitoka kapa.
"Kama alitoka, amuache Lissu na kesi yake, matokeo yatapatikana na yeye atayakubali kama alivyokubali yale ya Kenya," amesema Wasira.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Dodoma, Anthony Mavunde, amesema wanajiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, Serikali imefanya makubwa katika kuwasogezea huduma msingi kwa wananchi wake.
"Serikali imejenga shule, vituo vya afya, barabara, na katika miundombinu, Dodoma tunayo mtandao mkubwa wa barabara ikilinganishwa na mikoa mingi. Naamini tunadeni la kulipa katika uchaguzi mkuu," amesema Mavunde.