Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasira, Ndugai watupa ‘kijembe’ upinzani

Muktasari:

  • Wasira awanyooshea kidole wanasiasa wanaopiga kelele majukwaani badala ya kujenga hoja za kushawishi wananchi.

Dodoma.  Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema mtindo ulioibuka kwa baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaopiga kelele majukwaani bila kujenga hoja, wanataka shari huku akisisitiza demokrasi si vurugu bali ni majadiliano, hoja na maelewano.

Hoja hiyo ameizungumzia Wilaya Kongwa mkoani Dodoma anakoendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho aliyoianza jana Jumatano, Aprili 23, 2025 akiwa ameambatana na Waziri wa Nchi Ofisi Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

Amesema kufanya siasa za kupiga kelele majukwaani bila kujenga hoja ni jambo ambalo hakubaliani nalo na kuwashauri wanasiasa hao ambao hakuwataja majina kuja na sera nzuri za kushawishi umma ili waeleweke.

"Kama una hoja za kuwashawishi wapigakura wakukubali toa, kama huna kubali, kuna sehemu wanapita kwa sababu hawana watu, uchaguzi wa Serikali za mitaa wameshindwa kwa sababu hawana wagombea, sasa wanalalamika tumeibiwa... mumeibiwa wapi?" amesema.

"Vijijini humo hawana watu, hata mkienda kwenye Kijiji cha Kongwa mkasema niitieni hata watu 10 wa chama cha upinzani nitakulipa, atapata tabu na atakosa hela maana hawapo, kwa sababu watu hawaoni hoja, na ukiweza kupata wawili utakuta ni watu wa ajabu," amesema Wasira.

Amesema changamoto ya wanasiasa wengi ni kokosa ujuzi wa kujenga hoja kushawishi umma uwaelewe matokea yake wanaibua hoja wanaibiwa kura.

"Watu wanasema sema maneno hayana maana hata ukisema kuwaweka kugombea watu wanasema hawa hatuwezi kuwachagua maana hawana sifa, baadaye wanasema mmeiba, tumeiba nini? Wakati asilimia 60 ya wagombea wa CCM walikuwa wanapita bila kupigwa, tunawapigia kura ya ndio au hapana maana hawana wapinzani," amesema Wasira.

Huku akishangiliwa, mwanasiasa huyo mkongwe amesema:"Sasa wewe ukose asiliamia 60, ugombee asilimia 40, uweke watu hawana sifa, ushindwe alafu uende Umoja wa Mataifa (UN), huko utaenda lakini sisi tutakuwa tumeshamaliza hiyo kazi.”

"Kuna mzungu mmoja aliniuliza inawezekana vipi Tanzania CCM mkashinda uchaguzi asilimia 90, akasema jambo hili kwetu haliwezekani, nikasema hata mimi niliishi huko kwenu, lakini mazingira yenu sio hapa…ninyi hamna vitongoji, wala hamna vijiji tuna utaratibu wetu," amesema.

Amesema CCM wana ajenda ya kudumu ya kubadili maisha ya watu, wanataka maisha yawe mazuri kila mwaka, ya leo yawe mazuri kuliko jana na ya kesho yawe mazuri kuliko ya leo.

"Sasa wengine wanatuuliza CCM mmekaa sana na sisi tunawauliza tulipotafuta uhuru tuliwaambia tunakaa mpaka lini? Tunamkataba gani na ninyi? Maana wanaotuuliza ni wajukuu wa waliotutawala pamoja na vibaraka wao wa ndani.

"Tunawaambia tuko kwa idhini ya Watanzania ambao wako kwa idhini ya Mungu, ilimradi wanatuunga mkono, hatutaki kuulizwa swali la nini kwasababu tunakazi ya kufanya, kazi yetu lazima itaendelea," amesema.


Alichokisema Ndugai

Hoja ya kujenga hoja imeungwa mkono na mbunge wa Kongwa, Job Ndugai aliyesema kuna umuhimu kwa wanasiasa kujifunza jambo hilo huku akimtolea mfano Wasira amekuwa mfano bora.

"Binafsi nampongeza mzee Wasira ni kaka yangu, lakini pia nilimkuta kule bungeni ni mmoja wa walezi wangu ninyi mlioko huko hamuwezi kumfaidi ila kama tuliyekuwa naye bungeni kwenye kusukuma na kujenga hoja akisimama utajua mzee Wasira ni mashine," amesema.

"Ukitaka kupambana na mzee Wasira kwa hoja jipange, jabali hili lakini nimshukuru kwa kipekee kwa sababu siku za huko nyuma kabla ya wadhifa wa sasa, alikuja hapa Kongwa alinitembelea kama mdogo na ndugu yake tulikaa nyumbani saa kadhaa tukala nyama kidogo," amesema.

"Ninavyosema kaka yangu namaanisha kweli nakushuru mbele ya wananchi wangu hawa kwa kuwa muda ni mchache nikukaribishe na siku nyingine," amesema Ndugai ambaye amewahi kuwa Spika wa Bunge.

Kwa upande wake, Waziri Simbachawene anazunguka katika ziara hiyo na Wasira kutekeleza maelezo aliyopewa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa.

"Nimeagizwa kwa niaba ya Serikali niambatane na Wasira ili kupokea maelekezo ya chama kinachotawala kwakuwa inalenga kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi," amesema