Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachambua Bunge la 12 likimaliza muda wake, Rais Samia kulitubia

Muktasari:

  • Wakati uhai wa Bunge la 12 ukifikia ukingoni kesho Juni 27, 2025, wachambuzi wa siasa wamelitathmini na kutoa maoni yao kwa kulitazama namna lilivyofanya kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano.

Dar es Salaam. Wakati Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likimaliza muda wake kesho Ijumaa Juni 27, 2025, wadau wa siasa wamelichambua Bunge hilo na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha ufanisi katika Bunge lijalo.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutoa hotuba ya kulivunja Bunge hilo huku matarajio ya Watanzania wengi ni kusikia Rais akieleza ufanisi wake tangu alipoingia madarakani, Machi 19, 2021.

Itakumbukwa, Rais Samia alipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Rais John Magufuli ambaye alifariki Machi 17, 2021, hivyo Samia akawa Rais kwa mujibu wa Katiba ya nchi inayoelekeza kwamba endapo Rais atafariki, basi makamu wake ataapishwa kuwa Rais.

Kuvunjwa kwa Bunge hilo ni mwanzo wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika Oktoba mwaka huu.

Tayari vyama vya siasa vimeshaanza michakato ya ndani ya utoaji na urejeshaji wa fomu kwa makada wake kuomba ridhaa ya kuwania nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Vyama ambavyo tayari vimeshaanza mchakato huo wa utoaji wa fomu ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), ACT Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na Alince Democratic Party (ADC).

Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho tayari kimetangaza kuanza rasmi utoaji wa fomu za kuwania ubunge na udiwani Juni 28, 2025, huku kikiwa tayari kimeshawateua Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Dk Hussein Mwinyi (Zanzibar) kuwania nafasi za urais, huku Dk Emmanuel Nchimbi, akiteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia.

Uchaguzi huo utahusisha nafasi ya Rais, wabunge na madiwani upande wa Tanzania Bara na Zanzibar huku Bunge ambalo ndiyo chombo cha kutunga sheria likitarajiwa kuwa na ongezeko la wabunge baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuongeza majimbo mapya ya uchaguzi.

Wakati uhai wa Bunge hili ukifikia ukingoni, wachambuzi wa siasa wamelitathmini na kutoa maoni yao kwa kulitazama namna lilivyofanya kazi kwa kipindi chote cha miaka mitano.


Wachambuzi wafafanua

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Abdulkarim Atiki anasema Bunge linalomaliza muda wake, chimbuko lake linafahamika lilikuwa lile la "nileteeni huyu na yule."

“Ni bunge ambalo kabla yake kulikuwa na mambo yaliyodhoofisha upinzani, kwa hiyo kulikuwa na kuunga mkono juhudi kwingi, wabunge wengi walitoka vyama pinzani kujiunga na chama tawala,” anasema. 

Kwa mujibu wa Atiki, baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 kuna baadhi walirudi na wengi wao hawakurudi, hali hiyo ililifanya Bunge lionekana kama la chama kimoja cha siasa.

“Bunge halikuwa na kauli, wabunge hawakuwa na uwezo wa kuikosoa Serikali kwa kadri na jinsi wanavyoweza kwa sababu wengi wao ilikuwa ni inayotokana na chama chao, halikuwa Bunge lenye hoja ngumu kinzani bali lilionekana ni shamrashamra na tulivu,” anasema.

Hata hivyo, anasema licha ya Bunge kufanya kazi kubwa kama muhimili wa kutunga, kujadili na kuchambua sheria kabla ya kuzipitisha, pia lilijishughulisha na masuala mengine ya kuisimamia na kuishauri Serikali.

Lakini ufanisi wa wabunge wenyewe katika maeneo yao, ulidorora kwa kiasi kikubwa, huku Serikali Kuu ikionekana kutekeleza mambo mengi kwa miongozo yake badala ya kupitia Bunge.

Tunategemea Bunge lijalo litakuwa na mabadiliko makubwa. Kwa mtazamo wangu, wabunge wengi waliopo sasa hawatarejea na kwa kuwa kumekuwa na mabadiliko ya sheria ya uchaguzi pamoja na uwepo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyama vya upinzani vina nafasi kubwa ya kupata wawakilishi wengi,” anasema mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa.

Anaeleza kuwa Bunge lijalo litakuwa tofauti endapo litakuwa na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani, kwa sababu ukosoaji wa upinzani ni wa hoja zaidi ukilinganisha na ukosoaji unaotolewa na wabunge wa chama tawala ambao mara zote hutumia staha zaidi.
 

Ukosoaji wa vyama vya upinzani unaamsha ari na kuchangamsha Bunge na kuongeza chachu ya hoja zenye msingi na masilahi kwa wananchi,” anasema.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk Ponsian Ntui anasema Bunge linalomaliza muda wake halikuwa la wananchi, bali lilionekana kama sehemu tu ya kuziba nafasi.
 

Sehemu kubwa ya wabunge hawakufanya kazi zao ipasavyo kama wawakilishi wa wananchi, badala yake lilijigeuza kuwa Bunge linaloitumikia Serikali bila kuisimamia ipasavyo,” anasema Dk Ntui.

Anaongeza kuwa Bunge hilo lilikosa uhalisia wa kiuwakilishi, hali iliyosababisha wananchi kuhisi fedha zao za kodi hazikuzaa matunda.
 

“Tunatamani kuona Bunge lijalo likiwa bora zaidi, kama yalivyokuwa mambunge ya 10 na 11. Tunatamani Bunge lenye uwakilishi wa kweli wa wananchi, yaani wanaochaguliwa ni wale waliotokana na matakwa halisi ya umma, si wale wanaotafuta nafasi kwa masilahi binafsi,” anasema msomi huyo.

Dk Ntui anasisitiza kuwa ni muhimu taasisi ya Bunge ifanye kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema Bunge linalomaliza muda wake lilikuwa kimya zaidi kwa sababu lilijumuisha wabunge wengi wa chama kimoja pekee.
 

“Tofauti na Bunge la mwaka 2015 na 2010, ambalo lilijumuisha wabunge wa upinzani, Bunge la sasa halikuwa na sauti yenye ushawishi mkubwa. Hata wabunge 19 wa viti maalumu na mmoja wa jimbo kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanne kutoka Chama cha ACT Wazalendo, hawakuonyesha uimara, kwa sababu walizidiwa nguvu na idadi kubwa ya wale wa CCM,” anasema.

Anabainisha kuwa masuala mengi muhimu kwa jamii yalikosa mjadala mzito na kulifanya Bunge lilionekana kama la chama kimoja pekee.
 

“Hata nafasi ya Bunge ya kuisimamia Serikali haikufanywa kwa ufanisi ukilinganisha na Bunge la 11,” anasema Dk Mbunda na kuongeza;

Kuna idadi kubwa ya wananchi wanaoona kuwa wabunge wao wa sasa hawakuwatendea haki, ndiyo maana kinyang’anyiro cha nafasi hizo kinaonekana kikichangamka zaidi.

Pamoja na hayo, Dk Mbunda anaeleza wasiwasi wake kwamba hadi wakati wa uchaguzi, huenda chama kikuu cha upinzani cha Chadema kama hakitashiriki,  huenda inaweza kusababisha Bunge lijalo likabaki likiwa na sura ileile.
 

Kama hali hiyo itajitokeza, tutakuwa na Bunge lenye mwendelezo wa mtangulizi wake. Lakini iwapo upinzani utakuwa imara na kushiriki kwa wingi, Bunge linaweza kubadilika na kuwa lenye uchangamfu zaidi, likiisimamia vyema Serikali, anamalizia Dk Mbunda.