Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mjadala Sheria ya Fedha wahitimishwa kwa ahueni maeneo haya

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akijibu hoja za wabunge kuhusu muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2025, jijini Dodoma leo Juni 25, 2025. Picha na Hamis Mniha

Muktasari:

  • Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuongeza ushuru wa mazao ambayo Tanzania inajitosheleza.

Dodoma. Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2025, Serikali ikifanya marekebisho kwa baadhi ya maeneo yaliyozua mjadala bungeni na miongoni mwa wadau.

Miongoni mwa maeneo hayo ni kuhusu ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki na tozo ya dola 44 kwa watalii wanaoingia nchini.

Muswada huo umewasilishwa bungeni leo Juni 25, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, ambaye akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala amesema ushuru wa bidhaa kwenye huduma utabaki asilimia 17 badala ya asilimia 17.5 uliopendekezwa.


Serikali yakubali

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Twaha Mpembenwe akiwasilisha maoni ya kamati hiyo bungeni, amesema Serikali imekubali kutoongeza ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.

Amesema katika uchambuzi, kamati ilibaini ushuru wa bidhaa kwenye mawasiliano Tanzania ni mkubwa kuliko nchi za Kanda wa Afrika Mashariki, akitoa mfano Kenya ni asilimia 15, Uganda (asilimia 12), Rwanda (asilimia 10), Malawi (asilimia 10), Botwana na Afrika Kusini hawatozi kabisa.

“Kuongeza kiwango hicho kingeleta madhara kwenye kuchochea kasi ya kuelekea uchumi wa kidijitali. Aidha, hatua hiyo ni kinzani kwa maendeleo yaliyofikiwa na Serikali katika kuchochea matumizi ya teknolojia,” amesema.

Kuhusu kuanzisha bima ya usafiri kwa wageni wanaoingia nchini kwa kiwango cha Dola 44 za Marekani, Mpembenwe amesema hatua hiyo inakwenda kuongeza gharama kwa watalii na wafanyabiashara wanaoingia nchini.

“Hata hivyo, kamati ilikubaliana na Serikali kwamba utekelezaji wa vifungu vinavyopendekezwa katika eneo hilo uanze Januari 2026 ili kutoa fursa ya kufanya majadiliano na sekta zinazoweza kuathirika kabla ya kuanza kutekelezwa,” amesema.

Akizungumzia Sheria ya Kodi ya Mapato, Mpembenwe amesema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ili kutambua faida ambayo haijagawanywa kwa wanahisa kuwa sehemu ya mtaji.

Amesema marekebisho hayo kwa ujumla yatapelekea faida ambayo haijagawanywa kwa wanahisa kutozwa kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 10 baada ya miezi sita, lengo likiwa kuchochea uingizaji wa mitaji katika shughuli za uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.

Amesema baada ya uchambuzi huo, kamati ilibaini kifungu hicho si kipya kilikuwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 1973 na Taifa jirani la Kenya lina kifungu kama hicho.

Amesema kamati iliishauri Serikali kufanya marejeo ya kifungu hicho na kuondoa utata uliopo, akieleza Serikali ilikubali na marekebisho yalifanyika ambayo sasa itakuwa miezi 12 badala ya sita.

Kuhusu kuongeza gawio la asilimia 15 hadi 60 kwa mashirika ya umma, Mpembenwe amesema kamati imejadiliana kwa kina na Serikali kuhusu suala hilo, ikabaini hakuna vigezo vilivyowekwa kisheria vitakavyotumika kubainisha ni taasisi gani au shirika gani lichangie kwa asilimia 15 au zaidi.

“Serikali haikuwasilisha mbele ya kamati uchambuzi wa kitaalamu uliosababisha kufikia mapendekezo hayo,” amesema.

Amesema mapendekezo hayo yanaenda kinyume cha maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati akipokea gawio la mashirika ya umma, alipoagiza yalelewe ili yachangie zaidi.

“Kuna udhaifu katika usimamizi wa matumizi ya mashirika, hivyo badala ya Serikali kushughulikia udhaifu huo imekuja na pendekezo hili,” amesema.

Amesema hivi sasa kuna baadhi ya mashirika na taasisi za umma zinashindwa kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi, hivyo kupanua wigo ni kuleta changamoto kubwa kwenye taasisi na mashirika ya umma.

“Kuongeza kiwango kati ya asilimia 15 hadi 60 kutaleta madhara makubwa katika utendaji kazi wa taasisi hizo na utaratibu huu unaathiri mtiririko wa fedha kwa baadhi ya mashirika, ambayo yanatumia mtiririko wake kukopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema.

Amesema kutokana na sababu hizo kamati haikukubaliana na Serikali na imewasilisha jedwali la marekebisho, ili Bunge lifanye uamuzi sahihi.

Akiwasilisha muswada huo, Dk Mwigulu alisema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Fedha za Umma.

Lengo la marekebisho hayo amesema ni kuongeza kiwango kinachotakiwa kuchangiwa na taasisi na mashirika ya umma kati ya asilimia 15 hadi 60 ya mapato ghafi katika mfuko mkuu wa Serikali kila mwezi.

Pia amependekeza kuongeza kifungu kipya cha 134A katika Sheria ya Bima ili kuanzisha bima ya usafiri kwa wageni wanaoingia nchini kwa kiwango cha Dola 44 za Marekani (Sh116, 000).

“Lengo la marekebisho haya ni kuweka utaratibu utakaowezesha kuwalinda wageni wanapokuwa nchini dhidi ya dharura za kiafya, kupotea kwa mizigo yao na kugharimia wageni wanapoondoshwa kwa lazima au panapokuwapo hatari yenye kulazimu uondoshwaji,” amesema.

Amesema hatua hiyo haitahusisha wakazi wanaotoka nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Vilevile amependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Hifadhi za Taifa, kwa kuweka mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Amesema asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya taasisi hiyo iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na asilimia 40 itawekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Muswada unapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kuweka mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Dk Mwigulu asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya mamlaka hiyo iliyopo BoT na asilimia 40 itawekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Akihitimisha mjadala huo, ameyataja  maeneo mbalimbali ambayo yamefanyiwa marekenisho akiongeza kuwa: “Hii ni sehemu tu—kuna maeneo mengine mengi ambapo tumeyazingatia maoni ya Bunge na Kamati.”


Mchango wa wabunge

Wakati wa kuchangia mjadala, mbunge wa Kuteuliwa, Shamsa Vuai Nahodha ametaka kuangaliwa kwa busara suala la mashirika hayo kutoa gawio la asilimia 15 hadi 60 kwa sababu hakuna uwazi katika vigezo vitakavyotumika.

“Tunataka nini? Tunataka kulinda mapato au tunataka nini. Kwa maoni yangu mambo yetu kama wabunge na viongozi siku zote tuyafanye katika masilahi ya Taifa hili,” amesema.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei alitaka kuangalia upya suala la kuweka bima kwa watalii wanaoingia nchini, huku mbunge wa Kalembo, Josephat Kandege akishauri kuangalia upya suala la kuongeza ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa kuwa litasababisha changamoto, hasa kwa wakazi wa mikoa ya pembezoni.

Ameshauri badala ya kuwapo ongezeko la ushuru, kuwe na vivutio kwa wawekezaji wanaokwenda kuanzisha viwanda mikoa ya pembezoni ili kupunguza gharama ya bidhaa, ikiwamo saruji ambayo imekuwa ikinunuliwa kutoka nje ya nchi katika mikoa ya pembezoni kwa bei nafuu.

“Huwezi kulazimisha mtu wa Kagera aache kununua bidhaa Uganda, ni vizuri kuhakisha wananchi wananufaika na jiografia ya nchi yetu,” amesema.

Mbunge wa Mwera, Zahoro Mohamed Haji amesema haoni maana ya kuongeza ushuru kwenye gesi asilia wakati Serikali ikihamasisha matumizi ya nishati safi.

Kuhusu ushuru kuongezwa katika baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi, Dk Mwigulu akijibu hoja za wabunge amesema ushuru ulioongezwa ni kwa bidhaa ambazo zinazolishwa zaidi ya mara mbili nchini.

 “Tumekubaliana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na wa Kilimo, mwakani tutaenda kuweka ushuru katika mazao yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ambayo huku ndani wameendelea kuongeza uzalishaji,” amesema.

Amesema lengo ni kulinda viwanda na mazao yanayozalishwa nchini na kwamba, wataendelea kuongeza ushuru wa mazao ambayo Tanzania inajitosheleza.