Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO- Chadema yatangaza maandamano Januari 24, Polisi yasema mapema kutoa tamko

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Leo Januari 13, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema Jeshi la Polisi majukumu yake ya msingi,  mbali ya kulinda maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kulinda amani na kusimamia sheria

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza maandamano kwa wanachama na wapenzi wa chama hicho yatakayofanyika Jumatano Januari 24, mwaka huu kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau wa uchaguzi nchini.

Kauli ya Mbowe imekuja wakati Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ikikamilisha sheria iliyosomwa bungeni Novemba 2023 jijini Dodoma.

Miswada hiyo ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Hata hivyo, akizungumzia kauli ya Chadema kuhusu maandamano, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema: "Jeshi la Polisi majukumu yake ya msingi,  mbali ya kulinda maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kulinda amani na kusimamia sheria. Jeshi la Polisi na sisi tumesikia tamko hilo, ni mapema sana kusema au kutoa tamko lolote."

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi mpya za chama hicho Mikocheni leo Jumamosi Januari 13, 2024 jijini hapa kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati Kuu cha dharura Januari 8 mwaka huu, Mbowe amesema chama hicho hakijaridhishwa na miswada hiyo na wanataka iondolewe.

Amesema kwa muda mrefu yeye alipigania maridhiano na CCM, huku akipingwa na viongozi na wanachama wenzake, lakini amedai miswada hiyo imeonyesha kutozingatia maridhiano hayo.

Chadema yatangaza maandamano Januari 24

 “Naagiza viongozi wa chama wa mikoa yote kuanza maandalizi tunataka Serikali wajue hatuna utani. Viongozi wa mikoa, wilaya, kata na mitaa kuanza maandalizi ngazi zote hadi tutaratibu hadi kwenye sekretarieti, tuhamasishe majirani kujitokeza itakuwa ni ruti yenye maumivu,” amesema Mbowe

Akieleza tathimini ya kamati kuu ya chama hicho, amesema wamejiridhisha kwamba Serikali haitaki kuwepo kwa maboresho ya msingi katika mfumo wa uendeshaji wa chaguzi nchini na ukuaji wa demokrasia.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema miswada hiyo ilipelekwa bungeni kwa utaratibu wa kawaida ndio maana wadau wakaruhusiwa kutoa maoni kwa lengo la kuboresha mahali walipoona kuna upungufu.

" Serikali imepeleka miswada bungeni kwa utaratibu wa kawaida sio hati ya dharura ambayo isingetoa nafasi ya mjadala, lakini kwa njia ya kawaida kuna nafasi ya mjadala

"Ndio maana  Januari 4,  Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ushirikiano na Baraza la Vyama vya Siasa walifanya mkutano mkuu maalumu wa kujadili miswada hiyo,” amesema Matinyi.

Pia, amesema jambo la kufanya hivi sasa ni wananchi na wadau kutoa maoni na mapendekezo yatakayoboresha kilichopo katika miswada hiyo yenye ya kuimarisha na kudumidha demokrasia.

"Tutumie nafasi kutoa maoni yetu, kwa nini Serikali iondoe kitu walichokileta kukijadili kwa utaratibu wa kawaida na sio hati ya dharura? Mkutano wa Ofisi ya Msajili ulikuwa mzuri na kulikuwa na sekretarieti ya kukusanya maoni, tutoe maoni ya kuboresha sio kuiondoa bungeni au kufanya tukio lolote lisilorajiwa

"Kwa nini uondolewe wakati kuna utaratibu mzuri umewekwa  wa kutoa maoni, ingekuwa Serikali imeleta miswada kwa utaratibu usioruhusu maoni hapo watu wangezungumzia uwezekano wa kuondolewa miswada," amesema Matinyi.

Akiendelea kuzungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mbowe amesema: “Rais Samia aliunda kikosi kazi kilichotumia fedha nyingi za Watanzania na iliandika ripoti yake na kuweka mapendekezo mahususi juu ya haja na nia ya kuwa na Tume Huru ya uchaguzi, lakini katika hali ya kushangaza miswada iliyowasilishwa bungeni haikuzingatia mapendekezo ya kikosi hicho cha rais mwenyewe.”

Amesema hata wadau wengine wakiwamo vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii walitoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kuwa na tume huru ya uchaguzi, ila miswada hiyo haikuyazingatia.

Kuhusu maridhiano Mbowe, amesema Chadema kimekuwa na vikao vya maridhiano na Serikali na CCM kuliwasilisha mapendekezo ya namna ya kukwamua mkwamo uliopo nchini hasa kwenye maeneo ya Katiba Mpya na kuboresha mifumo ya chaguzi.

Mbowe amesema juhudi nyingine zilizofanywa ni kufungua kesi katika Mahakama mbalimbali, ikiwamo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) dhidi ya Serikali, wakilalamikia mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya siasa yam waka 2019.

Katika kesi hiyo, EACJ iliieelekeza Serikali kufuta vifungu 3,4,5,9,15 na 29 kwa kuwa vinakiuka mkataba wa Afrika ya Mashariki ibara za 6 (d),7(2) na 8(1)(c).

Pia, ametaja kesi iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) kupinga wakurugenzi watendaji wa halmashauri kusimamia uchaguzi.

Kutokana na hayo, Mbowe amesisitiza kuwa chama hicho kinataka miswada hiyo iondolewe bungeni na badala yake Serikali iwasilishe muswada bungeni wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya.

“Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpitio ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ili uchaguzi uwe huru na haki baada ya kuondoa mapungufu ya kikatiba yaliyopo sasa,” amesema.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa amesema Serikali iwasilishe bungeni muswada ambapo pamoja na mambo mengine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwe na mamlaka ya kusimamia chaguzi zote ukiwemo wa Serikali za Mitaa.

Pia, kuhusu muswada wa marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa Kamati Kuu imeshauri uondolewe kwa sababu haitatui changamoto zilizopo.