Prime
Msimamo, mwelekeo mpya wa Chadema 2024

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Muktasari:
- Kwa mara ya kwanza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa kwenye jengo jipya wa makao makuu ya chama hicho zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam ametangaza...
Dar es Salaam. Siku mbili tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiwasilishe maoni yake kuhusu miswada mbalimbali ya sheria zinazohusu uchaguzi, chama hicho kinatarajia kutangaza msimamo wake mpya kesho Jumamosi, Januari 13, 2024.
Januari 10, 2024, chama hicho kupitia Katibu Mkuu wake, John Mnyika kiliwasilisha mapendekezo yake kwa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria juu ya miswada hiyo mitatu inayohusu uchaguzi na kupendekeza masuala mbalimbali.
Miongoni mwa mapendekezo ni kuondolewa bungeni kwa miswada hiyo, wakurugenzi wa halmashauri kutosimamia uchaguzi, ushindi wa kura za Rais ziwe zaidi ya asilimia 50 na kuwe na mwanya wa matokeo yake kupingwa mahakamani.
Mnyika alikwenda mbele ya kamati ikiwa ni siku mbili tangu Kamati Kuu ya chama hicho chini ya uenyekiti wa Freeman Mbowe kukutana kwa njia ya mtandao Januari 8, 2024.
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka ndani ya chama hicho, pamoja na mambo mengine kamati hiyo ilijadili kwa kina miswada hiyo ilipo bungeni ambayo itaendelea na mchakato kwenye mkutano wa Bunge utakaoanza Januari 30, 2024.
“Tulikutana katika kamati kuu Janauri 8 na kesho mwenyekiti atatoa maazimio, miongoni ni kuitisha maandamano, sasa kama hatafanya hivyo labda abadili gia ngani,” amesema mmoja wa wajumbe wa kamati kuu.

Muonekano wa ofisi mpya za Chadema zilizoko Mikocheni Jijini Dar es Salaam ambazo zitatumika kufanya mkutano na waandishi wa habari kwqa mara ya kwanza kesho. Picha na Fortune Francis
Kiongozi mwingine wa chama hicho Kanda ya Pwani aliyekuwepo kwenye kufanya usafiri na maandalizi ya ukumbi utakaotumika kwenye mkutano huo amesema kabla ya kutolewa kwa maazimio ya kamati kuu, Mbowe alikutana na viongozi wote wa kanda hiyo.
“Uhamasishaji umekwenda kuanza, tulifanya kikao hivi karibuni na maandamano huenda yakatangazwa kufanyika Jumatano ya Januari 24, sasa yatakuwaje tusubiri,” amesma.
Gazeti hili limemtafuta, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliyesema mkutano huo na waandishi wa habari utakuwa ni kutoa hotuba yake ya ufunguzi wa mwaka na kueleza msimamo wa chama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Hatuna uzinduzi wa ofisi, tunatumia ukumbi tu ambao mwenyekiti atazungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa chama kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na hotuba ya mwaka mpya,” amesema Mrema.
Mkutano huo unafanyika makao makuu mapya yaliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam ambapo gazeti hili limefika leo asubuhi Ijumaa Januari 12, 2024 na kukuta maandalizi ya ukumbi yakiendelea chini ya usimamizi wa Mbowe ambaye hakuwa tayari kuzungumza lolote.
Ukarabati mwingine uliokuwa unafanyika ni pamoja na kufyeka nyasi nje ya jengo hilo, marekebisho ya mfumo wa umeme na maji taka huku baadhi ya vijana wakionekana kufuta vumbi kwenye vioo vya jengo hilo la ghorofa mbili.
Mchambuzi wa masuala ya sisiasa, Dk Onesmo Kyauke akizungumzia msimamo huo wa Chadema, ameshauri uchaguzi wa serikali za mitaa uahirishwe na kuchanganywa na uchaguzi mkuu kwa kuwa ushiriki wa wananchi umekuwa mdogo kutokana na namna unavyofanyika.
Amesema Serikali ya Zanzibar huwa inapiga kura nyingi kwa wakati mmoja tofauti na Tanzania Bara, hivyo ili kuokoa gharama, chaguzi hizi zinaweza kuchanganywa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi (NEC).
“Chadema wanahitaji sana kufikiria njia ya majadiliano kuliko maandamano, suala la uchaguzi linahusisha wadau wengi si chama kimoja au viwili, wote wanapaswa kushirikishwa ili kupata muafaka.
“Kuna sababu ya kuangalia upya sheria inaweza kutamka uchaguzi huu uunganishwe na uchaguzi mkuu, uzoefu unaonyesha ushiriki wa wananchi ni mdogo sana kuanzia kwenye kujiandikisha hadi kupiga kura na kusababisha gharama zisizo za msingi,” amesema Dk Kyauke.
Akizungumzia suala la maridhiano, Dk Kyauke amesema kuna haja ya kuliangalia upya kwa kuwa Tanzania ni kubwa kuliko vyama hivyo na kushauri kuwepo ushirikishwaji wa wadau wengine katika majadiliano hayo.
Ofisi mpya
Kuhusu ofisi za makao makuu ya Chadema, Gazeti la Mwananchi ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti juu ya chama hicho kuhamia katika ofisi mpya za kisasa maeneo ya Mikocheni huku ofisi zao za Kinondoni zikibaki kama sehemu ya makumbusho.
Chadema ilianza kukaa ofisi za Kinondoni, Mtaa wa Ufipa kuanzia mwaka 2000. Katika ofisi hizo kuna majengo matatu ya kawaida mali ya chama hicho yanayotumiwa na katibu mkuu, manaibu wake, ofisi za idara, mwenyekiti na mabaraza ya chama.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Chadema ilitenga zaidi ya Sh2 bilioni kwa ajili ya ofisi mpya ya makao makuu huku ofisi ndogo ya chama hicho Zanzibar ikiwekewa kati ya Sh400 milioni hadi Sh500 milioni.
Ununuzi wa ofisi hizo ulichangiwa na uamuzi wa Chadema kuanza kuchukua ruzuku waliyoisusia tangu mwaka 2020 baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Mariadhiano
Mei 20, 2022, ujumbe wa Chadema wakiongozwa na Mbowe walikuwana na viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na walifanya mazungumzo katika Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Baada ya mazungumzo hayo, Mbowe alikutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa CCM wakiongozwa na makamu mwenyekiti bara, Abdulrahman Kinana.
Unaweza kusema maridhiano hayo yamezaa matunda ikiwemo Chadema, kukubali kuchukua ruzuku, viongozi wao waliokuwa wakiishi ughaibuni akiwemo Godbless Lema na Makamu Mwenyekiti-Bara, Tundu Lissu kurejea Tanzania baada ya Serikali kuwahakikisha usalama wao.
Mazungumzo yalichochea hatua ya Rais Samia kuhudhuria mkutano wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani uliandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) uliofanyika Machi 8, 2023 mkoani Kilimanjaro.
Kama hiyo hiyo haitoshi, Machi 19, 2023 viongozi wa Bawacha walihudhuria sherehe zilizoandaliwa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT), zilizokuwa na lengo la kumpongeza Rais Samia kwa kutimiza miaka miwili wakati huo.
Maridhiano yamesaidia kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara iliyopigwa marufuku kwa takribani miaka saba na Serikali ya awamu ya tano. Januari 3, 2023 Rais Samia aliruhusu mikutano ya hadhara.
Mbali na hilo, Rais Samia aliukwamua mchakato wa Katiba uliokwama tangu mwaka 2014 kwa hatua ya Katiba Pendekezwa kufutwa.
Kwa mara ya kwanza viongozi wa Chadema walihudhuria mkutano mkuu maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa, uliokuwatanisha wadau wa demokrasia.
Tangu mwaka 2020, Chadema kimekuwa kikisusia shughuli mbalimbali za Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini walishiriki mkutano ulioitishwa Januari 3-4, 2024 jijini Dar es Salaam kujadili miswada ya sheria za uchaguzi.
Katika mkutano huo, Chadema waliwakilishwa na Manaibu Katibu Mkuu, Benson Kigaila (Bara), Salumu Mwalimu (Zanzibar), Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Hashim Juma Issa na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Sharifa Suleiman.
Katika mahojiano maalum na Gazeti la Mwananchi yaliyofanyika Desemba 21, 2023, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema chama hicho kimeanza kushiriki shughuli za Baraza la Vyama vya Siasa na kitakuwa kikiwakilishwa na manaibu katibu wakuu wake wawili na pale itakapohitajika Mbowe na yeye mwenyewe watashiriki.