Ulinzi waimarishwa, maombi yafanyika mahakamani kesi ya Lissu

Muktasari:
- Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu leo Jumatatu atapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kusikiliza kesi zinazomkabili ya uhaini nay a kuchapisha taarifa za uongo.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi kwa mara nyingine limeendelea kuimalisha ulinzi katika viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam zinaposikilizwa kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na kesi kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni ambapo leo Jumatatu, Juni 16, 2025, amefikishwa mahakama hapo. kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi hizo.
Kesi hizo ambazo zinasikilizwa na mahakimu wawili tofauti zote zimepangwa kuendelea leo Jumatatu, Juni 16, 2025 lakini katika hatua tofautitofauti.
Wakati kesi ya uhaini leo inatajwa kwa ajili ya Serikali kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi ulikofikia, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo imepangwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji rasmi, yaani Mahakama kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mwananchi ambayo imetia kambi mahakamani hapo imeshuhudia hali ya ulinzi mkali wa polisi ikiimarishwa huku baadhi ya Polisi wakionekana kuzunguka nje ya uzio wa mahakama hiyo na getini kukiwa na ulinzi pia wakiwahoji wanaoingia na kutoka.
Kati ya Polisi hao, wapo wanaotembea kwa miguu huku na kule kuangalia hali ya usalama na wapo wanaozunguka wakiwa wamepanda farasi na baadhi kuonekana kusogelea watu ambao wanaonekana kukaa kwa vikundi.
Ulinzi huo wa askari umekuwa ukifanyika kila kesi hizo za Lissu zinapofanyika. Magari ya washawasha nayo yameegeshwa maeneo ya kuzunguka eneo la mahakama hiyo.
Saa 2:29 asubuhi msafara wa magari ukiongozwa na polisi uliwasili mahakamani hapo, huku gari lilombeba Lissu likiwa na askari magereza.
Kama ilivyokawaida askari magereza wameshuka wakiwa wanakimbia ingawa mara hii wametumia geti la nyuma ya mahakama hiyo kuingia.
Msafara huo wa askari uliingia ndani kwa haraka tayari kwenda mahakamani.
Baadhi ya makada wa Chadema wameonekana kufika maeneo hayo baadhi wakiwa wamevalia fulana zenye maandishi ya 'No Reforms, No Election.'
Pia Dk Azaveli Lwaitama ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, ameonekana katika viunga hivyo japo alipata tabu ya kuruhusiwa kuingia mahakamani hapo na kuonekana kwenda na kurudi nje ya mahakama hiyo.
Mwingine aliyeonekana kupata changamoto ya kuingia ni Eugene Kabendera ambaye ni mwanachama mpya wa Chadema aliyetokea Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) hivi karibuni.
Kutokana na sintofahamu hiyo, Kabendera alionekana akiwa amesimama upande wa pili wa jengo linalotazamana na mahakama na hadi kufika saa 9:15 asubuhi wawili hao walikuwa bado nje.
Akizungumzia hali hiyo, Dk Lwaitama amesema alipofika hapo aliambiwa kwamba ndani kuna idadi kamili ya wanaopaswa kuingia na tayari amejaa.
"Niliambiwa ndani tayari kumejaa kwa sababu kuna idadi kamili ya watu. Hata hivyo nina imani nitaingia kwa kuwa kuna mmoja wa viongozi wa Chadema ameniambia nimsubiri hapa karibu na Mahakama atakuja kunichukua,” amesema Dk Lwaitama.
Maombi yafanyika
Katika chumba cha Mahakama, Askofu Emaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho la Morovian alimtambulisha mmoja wa watu ambaye amesema anapaswa kuiombea kesi hiyo kabla ya kuanza.
Takribani wananchi wote waliokuwa kwenye chumba cha Mahakama walisimama na wengine kufumba macho kushiriki maombi hayo.
Endelea kufuatilia Mwananchi