Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

VIDEO: Kesi ya Lissu mubashara, mahakama kupokea ushahidi

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Muktasari:

  • Lissu, mwenyekiti wa Chadema anakabiliwa na kesi mbili za jinai, moja ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni ambayo imepangwa leo kuanza kutolewa ushahidi na nyingine ya uhaini, leo inatajwa.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Juni 2, 2025 inaanza kupokea ushahidi wa Serikali katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha mitandaoni taarifa za uongo, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Mawakili walivyochauana Kisutu kesi ya Lissu

Mashtaka hayo ni ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam kwa nia ya kulaghai umma.

Kesi hiyo itasikilizwa mbushara kupitia chaneli ya Mahakama hiyo huku watakaoruhusiwa kuingia ni watu wasiozidi 80.

Taarifa ya Mahakama iliyotolewa jana Jumapili, inaeleza sababu ya kuingia idadi hiyo inatokana na ukumbi si mkubwa.

Mahakama hiyo imewataka wananchi wanaohitaji kufuatilia kesi hiyo kufanya hivyo kupitia akaunti ya Mahakama, “lengo la Mahakama kurusha mubashara matangazo ya mwenendo wa mashauri haya ni kuwawezesha wananchi popote pale walipo na ambao wanapenda kufuatilia mwenendo wa mashauri kuweza kufuatilia bila kuwa na ulazima wa kufika mahakamani.”

“Tunaomba umma ufahamu kuwa kwa uwezo huo imekubalika watakaoingia ni mawakili wa Serikali na watu wengine 10, mawakili utetezi na watu wengine 60 na waandishi wa habari,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika shtaka la kwanza Lissu anadaiwa kuchapisha maneno:"Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa  kwa maelekezo ya Rais," wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na ya kupotosha umma.

Shtaka la pili anadaiwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa: "Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi.”

Katika shtaka la tatu anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa: "Majaji ni Ma-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.”

Kesi hii imepangwa kuanza usikilizwaji rasmi leo Jumatatu Juni 2, 2025 huku Mahakama ikianza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka (Serikali) unaokusudiwa kuthibitisha mashtaka hayo ili kumtia hatiani.


Katika kuthibitisha mashtaka hayo, Serikali inatarajiwa kuwaita mashahidi 15 na kiwasilisha vielelezo kadhaa.

Wakati aliposomewa mashtaka hayo kwa mara ya kwanza Aprili 10, 2025 na hata wakati wa usikilizwaji wa awali, Mei 19, 2025, alisomewa maelezo ya awali, Lissu hakuyakana maneno hayo bali alijibu kuwa maneno hayo si kosa kwa kuwa ni ya kweli.

Kwa hali hiyo shauku ya wadau wa masuala ya sheria na au wanaofuatilia kesi hiyo ni kusikia aina ya ushahidi ambao Serikali itauleta kupitia mashahidi wake hao kuthibitisha maneno hayo yanatengeneza makosa ya jinai.

Kama ilivyo kawaida, mashahidi hao katika ushahidi wake watakuwa wanaongozwa na mwendesha mashtaka kwa kuwaulizia maswali elekezi ya kile wanachotakiwa kusema.

Baada ya sehemu hiyo ya kwanza, sehemu ya pili watahojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa mshtakiwa kuhusiana na yale watakayokuwa wameeleza katika ushahidi.

Hata hivyo upande wa mashtaka utakuwa na nafasi nyingine ya kumuuliza shahidi maswali ya kusawazisha majibu yake wakati wa maswali hayo ya dodoso, mahali ambako wataona kuna haja ya kufanya hivyo.

Mbali na kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na kesi nyingine ya uhaini mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mafawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi  Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania, akidaiwa kutamka:

"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...kwa hiyo tunaenda kikinukisha...sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."

Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya maandalizi ya awali ikiwamo kukamilika kwa upelelezi kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kuisikiliza.

Kesi hiyo pia inatajwa mahakamani hapo leo.

Upande wa mashtaka leo unatarajiwa kutoa mrejesho wa upelelezi hatua ulikofikia.

Tangu aliposomewa mashtaka ya kesi hizo zote mbili, Lissu yuko mahabusu kwa kuwa shtaka hilo la uhaini halina dhamana.

Lissu ataendelea kusalia mahabusu kwa muda usiojulikana wakati kesi hiyo ikiendelea mpaka itakapoisha au itakapoamuriwa vinginevyo.