Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapya kesi za Lissu, Mahakama yatoa utaratibu zitakavyosikilizwa

Muktasari:

  • Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma mwezi uliopita na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, katika kesi mbili tofauti ya uhaini, mashitaka ambayo hayana dhamana na adhabu yake ni kifo na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo, kufuatia matamshi yake ya kuwataka wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Dar es Salaam. Mahakama ya Tanzania imesema kuwa mwenendo wa kesi zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu itarushwa mubashara ‘Live’ kupitia chaneli ya Mahakama hiyo.

Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma mwezi uliopita na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, katika kesi mbili tofauti ya  uhaini, mashitaka ambayo hayana dhamana na adhabu yake ni kifo na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo, kufuatia matamshi yake ya kuwataka wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Kupitia taarifa yake kwa Umma iliyotolewa leo Jumapili Juni Mosi, 2025, na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Mahakama ya Tanzania, Gerard Chami amesema pamoja na kwamba mshtakiwa huyo (Lissu) atafikishwa mahakamani kusikiza kesi zinazomkabili ila zitarushwa mubashara.

“Mashauri hayo vamepangwa kutajwa na kusikilizwa kesho Jumatatu Juni 2, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pamoja na kwamba mshtakiwa atafikishwa mahakamani, lakini mwenendo wote wa mashauri haya, utarushwa mubashara (live).”

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo imesema kuwa uwezo wa Mahakama ya wazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni kuhimili watu 80 pekee, huku ikisisitiza wananchi wenye nia ya kufuatilia mwenendo wa kesi hizo kufanya hivyo kupitia akaunti ya mahakama.

“Lengo la Mahakama kurusha mubashara matangazo ya mwenendo wa mashauri haya ni kuwawezesha wananchi popote pale walipo na ambao wanapenda kufuatilia mwenendo wa mashauri kuweza kufuatilia bila kuwa na ulazima wa kufika mahakamani,” imesema taarifa hiyo.

“Tunaomba umma ufahamu kuwa kwa uwezo huo imekubalika watakaoingia ni mawakili wa Serikali na watu wengine (10), mawakili utetezi na watu wengine (60) na waandishi wa habari,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, Mahakama hiyo imewahakakishia wananchi kuendelea kutoa haki kwa uwazi kwa wakati na kwa wote.

“Tunawahimiza wananchi wote kuendelea kushirikiana na Mahakama katika kujenga mfumo wa utoaji haki unaozingatia misingi ya kikatiba, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali. Kiungo cha matangazo hayo mubashara kitapatikana kabla ya saa 2:30 asubuhi ya kesho Juni 2, 2025 kupitia kurasa/ akaunti rasmi za Mahakama ya Tanzania katika mitandao ya kijamii na tovuti ya Mahakama www.judiciary.go.tz kabla ya mashauri kuanza,” imeeleza taarifa hiyo.

Mahakama hiyo imewataka watakaohudhuria mahakamani kufuatilia kesi hiyo kuhakikisha wanazingatia kanuni zote za kitaalam za kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama taarifa ya Wizara ya Afya ilivyoelekeza.