Prime
Mapya yaibuka kesi ya Lissu

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara.
Muktasari:
- Lissu alikamatwa mwezi uliopita na kushtakiwa kwa uhaini na kuchapisha taarifa za uongo, katika matamshi yake ya kuwataka wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 2025.
Dar es Salaam. Wakati kesi dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu zikitarajiwa kurejea mahakamani Juni 2, 2025, Wakili wake wa kimataifa, Robert Amsterdam ameibua mapya.
Amsterdam amewasilisha malalamiko kwenye Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na watu wanaozuiliwa kiholela (UNWGAD), akitaka uchunguzi wa haraka ufanyike kuhusu kukamatwa na kushikiliwa kwa Lissu na mamlaka za Tanzania.
Wakili huyo aliwasilisha malalamiko hayo Ijumaa iliyopita, akilenga kuongeza shinikizo la kimataifa ili aachiliwe huru, hatua ambayo hata hivyo inayoibua mjadala miongoni mwa wanasheria.
Lissu alikamatwa mkoani Ruvuma mwezi uliopita na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, katika kesi mbili tofauti— uhaini, mashtaka ambayo hayana dhamana na adhabu yake ni kifo na nyingine ya kuchapisha taarifa za uongo, kufuatia matamshi yake ya kuwataka wafuasi wake kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Kesi hiyo imekuwa ikivuta makundi mbalimbali, yakiwemo ya wanaharakati nadani na nje ya Tanzania.
Alipofikishwa mahakamani Mei 19, wanaharakati wawili wa haki za binadamu kutoka Kenya na Uganda, waliokuwa wameingia kushuhudia kesi hiyo, walikamatwa na kurudishwa nchini kwao.
Vilevile, wanasheria wawili – Martha Karua ambaye pia ni mwanasiasa wa Kenya na Jaji Mkuu mstaafu wa nchini moja, Willy Mutunga nao walirejeshwa kwao baada ya kutoa Dar es Salaam. Jaji mkuu mstaafu mwingine, David Maraga yeye alifanikiwa kufika mahakamani na kushuhudia kesi hiyo.
Hali ikiwa hivyo, Kampuni ya uwakili ya Amsterdam imetoa taarifa kwa umma kuhusu uamuzi wake huo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuishinikiza Serikali kumwachia huru mwanasiasa huyo.
Ingawa kitengo hicho cha Umoja wa Mataifa hakiwezi kulazimisha utekelezaji wa uamuzi, kinaweza kutoa maoni ya kisheria kuhusu kinachoendelea.
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema ambaye anaongoza jopo la mawakili wa Lissu katika kesi inayomkabili, Dk Rugemeleza Nshala amesema wao wanapambana kushinda kesi hapa nchini.
“Sisi tunapambana kushinda kesi yetu hapa ndani, huko kwingine Amsterdam mwenyewe anaweza kukueleza vizuri, mimi ni wakili kwenye kesi ya hapa Tanzania,” amesema mwanasheria huyo.
Mbali na kesi inayoendelea hapa nchini, mapema mwezi huu, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio linalopinga kukamatwa kwa Lissu.
Mamlaka za Tanzania hazikupatikana kuzungumzia hatua hiyo ya Wakili Amsterdam. Simu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari haikupokewa. Pia, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Ally Possi naye hakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Mwananchi lilimtafuta pia Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro naye hakupatikana mara moja kuzungumzia hatua hiyo ya Amsterdam.
Wanasheria wazungumza
Wanasheria mbalimbali nchini wametoa maoni mchanganyiko ambapo baadhi yao wanaelezea kuunga mkono hatua hiyo huku wengine wakiamini kuwasilisha ombi la kimataifa, kunaweza kuleta madhara badala ya kusaidia.
“Hili ni suala nyeti, na kulipeleka kimataifa wakati bado linaendelea katika mahakama za ndani kunaweza kuonekana kama kuikosoa au kuipuuza mahakama yetu,” amesema Joseph Kiwanga, mhadhiri wa sheria ya katiba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Ni muhimu kuruhusu mfumo wetu wa sheria kushughulikia kesi hii kwanza. Iwapo kutakuwa na ukiukwaji wa haki, ndipo njia za kimataifa zinaweza kufuatwa,” amesema.
Hata hivyo, amesema kwamba Tanzania imesaini mikataba kadhaa ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, jambo linalomaanisha kuwa hatua kama hizo zina msingi wa kisheria.
“Kuna nafasi ya kuchukua hatua hizi, lakini zinapaswa kusaidiana si kuchukua nafasi ya mchakato wa sheria wa ndani,” amesisitiza.
Baadhi ya wanasheria wanaona hatua hiyo kama ni ishara ya kukata tamaa kwa upande wa upinzani, katika mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa finyu, huku wengine wakiona kama ni makosa ya kimkakati.
“Timu ya kisheria ya Lissu iko sahihi kuhamasisha jamii ya kimataifa,” amesema Michael Mkumbo, mchambuzi wa siasa kutoka Dodoma.
“Lakini kupata tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu suala hili wakati kesi bado ipo mahakamani kunaweza kuchafua uhusiano wa kidiplomasia wa Tanzania na hata kuifanya Serikali iwe na msimamo mkali zaidi,” ameongeza.
Kwa upande mwingine, mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Hamisi Mwakyoma amesema “Tuiache Mahakama ifanye kazi yake.”