Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu achaguliwa IDU akiwa gerezeni

Muktasari:

  • Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema), amechaguliwa sambamba na Waziri Mkuu mstaafu wa 22 wa Canada, Stephen Harper ambaye anaendelea kuwa mwenyekiti wa muungano huo.

Dar es Salaam. Muungano wa vyama vya kidemokrasia duniani (IDU) umemchagua, Tundu Lissu kuwa mmoja kati ya jopo la makamu wenyeviti wa muungano huo Kanda ya Afrika.

Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokarasia na Maendeleo (Chadema), amechaguliwa sambamba na Waziri Mkuu mstaafu wa 22 wa Canada, Stephen Harper anayeendelea kuwa mwenyekiti wa muungano huo.

Kuchaguliwa kwa Lissu, kumefanyika akiwa mahabusu kutokana na kukabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni ambapo zinaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya kuchaguliwa kwa Lissu, imetolewa leo, Jumamosi Mei 24, 2025 na Chadema ikirejea taarifa ya IDU kuhusu mfululizo wa vikao vyake, vilivyohusisha uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, uchaguzi wa Lissu na Harper umefanyika jijini Brussels, Ubelgiji vilikokuwa vinafanyika vikao vya muungano huo.

“Katika mkutano huo ambao chama kiliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Democracy Union of Africa (DUA) Kanda ya Afrika Mashariki, Deogratias Munishi, wajumbe walimchagua Harper kuendelea kuwa mwenyekiti kwa miaka mitatu ijayo,” imeeleza taarifa hiyo.

Sambamba naye, mkutano mkuu huo, kwa kauli moja ulimchagua Lissu kuwa sehemu ya jopo la makamu wenyeviti wa umoja huo.

Uamuzi wa kuchaguliwa kwa Lissu, umetokana na rekodi ya msimamo usioyumba katika kupigania haki, utawala bora na demokrasia Tanzania licha ya mazingira hatarishi ikiwemo jaribio la kutolewa uhai Septemba 7, 2017.

“Zaidi, wajumbe wa mkutano mkuu wa IDU walitanabaisha kuwa, kwa uzoefu wake (Lissu) katika mapambano ya kutafuta demokrasia ya kweli, haki na uhuru wa kweli, Lissu atatoa mchango mkubwa ndani ya IDU hasa katika kumulika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za kuporomoka au kudorora kwa demokrasia na kuibuka kwa tawala za kiimla husani katika bara la Afrika,” amesema.