No reforms, no election rasmi kaskazini leo, wachambuzi wanena

Muktasari:
- Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema uzinduzi wa No reforms, no election kanda ya Kaskazini, utafanyika uwanja Reli jijini Arusha kuanzia saa saba mchana hadi saa 12 jioni
Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) leo Jumatano kikianza operesheni ya ‘No reforms, no Election’ katika mikoa minne ya kaskazini, baadhi ya wachambuzi wa siasa wameshauri hoja za kukaziwa na kuepukwa katika ziara hiyo.
Hoja hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu sababu za chama hicho kutoshiriki uchaguzi, suala la rasilimali za nchi kumnufaisha kila mwananchi huku wakitakiwa kupunguza mihemko, kutomzungumzia Freeman Mbowe (mwenyekiti wa zamani wa Chadema) au uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wao, John Heche leo Jumatano Mei 28, 2025 wataanza rasmi ziara ya Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kunadi kampeni yao ya No reforms, no election.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, uzinduzi wa kampeni hiyo unafanyika katika Uwanja Reli jijini Arusha kuanzia saa saba mchana hadi saa 12 jioni leo Jumatano Mei 28, 2025.
Amesema Chadema wanakwenda Kanda ya Kaskazini ambayo ni ngome yao. Hata hivyo, wiki chache zilizopita ilipata misukosuko baada ya baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya kanda hadi wilaya wakiwamo wa mabaraza kutimikia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Miongoni mwa viongozi walioondoka ni pamoja na Emma Kimambo aliyekuwa mhazini wa kanda ya kaskazini, Basil Lema, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilamanjaro, Gervas Mgonja, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro na Grace Kiwelu, Mwenyekiti wa Bawacha, Kilimanjaro.
Hata hivyo, Chadema Kanda ya Kaskazini tayari wameshaziba nafasi za viongozi waliotimka kwa kuzikaimisha.
Katika ziara hiyo watakuwa na kibarua cha kuweka mambo sawa katika kila mkoa watakaokanyaga.
Kampeni hii ni mwendelezo baada ya kukamilisha ile ya Kanda ya Victoria (Kagera, Mwanza na Geita) na Kanda ya Serengeti (Simiyu, Shinyanga na Mara) iliyofanyika kwa siku 12.
Kabla ya kwenda katika mikoa hiyo, ziara ya kwanza Chadema walianza kunadi No reforms, no election kanda ya Nyasa (Songwe, Mbeya, Rukwa, Njombe na Iringa.
Kisha msafara wa viongozi hao ukaelekea kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, ambako mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu ndiko alikokamatwa na kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akikabiliwa mashtaka ya uhaini na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni.
Akizungumzia ziara hiyo, Mchambuzi wa siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi amesema No reforms, no election bado haijaeleweka vizuri kwa wananchi hasa wa kawaida hivyo watumie mwaya huo kutoa elimu kwa kina kuhusu ajenda hiyo.
“Mwanzo nilipata shida kuelewa ajenda hii, ilichukua muda kuelewa kwa kina nilijitahidi kutenga muda ili kupata ufahamu wa suala hili. Sasa najaribu kufikiria kama mimi nilichukua muda mrefu kuelewa je, hao wengine? Nadhani watakuwa wamekwama tu kwa kiasi fulani.
“Sasa Chadema wanatakiwa kumuelewesha kwa kina yule bodaboda au mkulima nini maana ya No reforms, no election ina maana gani? Kwa nini wamekuja na hii ajenda, hii no reforms nini? No election maana yake ni nini? Na madhara yake,”amesema Dk Mushi.
Mchambuzi mwingine wa siasa, Ramadhani Manyeko amesema bado kuna changamoto kuhusu matumizi ya rasilimali za nchi, ndio maana katika kila ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anabainisha ufisadi na fedha za umma zinavyotafunwa.
“Hatuoni hatua zikichukuliwa ikiwemo kupelekwa mahakamani kwa wanaohusika au kutajwa kwenye ripoti ya CAG. Hoja iliyoko na mjadala kwa wananchi ni namna gani rasilimali zinatumika kwa manufaa yetu, si kwa manufaa ya waliopewa mamlaka,”amesema Manyeko.
Manyeko amesema Kaskazini hasa Kilimanjaro, Arusha na Manyara ni ngome ya Chadema hivyo katika ziara hiyo, wajikite kueleza kasoro za uchaguzi wa mwaka 2020 na 2024 wa serikali za mitaa ikiwemo wagombea wao kuenguliwa.
“Mbowe wasimtaje kabisa katika ziara yao, kwa sababu mwenyekiti huyo wa zamani hajasema lolote hadharani, wazungumzie kasoro na kwa nini wanahitaji reforms badala ya kueleza yaliyojiri kwani uchaguzi wao umeisha,” amesema Manyeko.
Hoja hiyo, iliungwa mkono na mchambuzi mwingine Kiama Mwaimu aliyesema Heche na wenzake wakifika huko wasizungumzie habari ya Mbowe, huku akitoa tahadhali huenda wakakumbana na zomeazomea.
“Huenda wakakumbana na hali hiyo, kutoka kwa watu watakaohudhuria mikutano yao ili watoke kwenye reli ili kuwajibu. Kwa jinsi viongozi wa Chadema wa sasa walivyo wanaweza kujibu na kupoteza uelekeo wa mkutano,"
“Wajitahidi kuzuia mihemko yao, wasijionyeshe wala kujibu, maana huenda ikatokea ugomvi na kuleta taswira ya Chadema mpya haina maana. Wakae kwenye hoja na kueleza kwa kina kwa nini wanasimamia No reforsm, no election,” amesema Mwaimu.