Samia asimame hapo, Lissu pale mechi dakika 90 - Heche

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akizungumza na wananachi (hawako pichani) leo Mei 27, 2025 katika eneo la Tarakea, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Chadema inaendelea na kampeni yake ya ya kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, ikiwa ni zamu ya Kanda ya Kaskazini.
Rombo. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema wanahitaji mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mgombea mteule wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ashindane na mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
Heche amesema hayo leo, Mei 27, 2025 Tarakea, Kilimanjaro, katika kampeni ya chama hicho ya kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi ikiwa ni zamu ya Kanda ya Kaskazini.
“Tumekuja kwenu kuwaomba mtuunge mkono, viongozi wa dini wamesema, viongozi wastaafu wamesema, kuna muda wa kutosha kufanya mabadiliko ili tuwe na uchaguzi huru na haki….. Rais Samia asimame hapa, Tundu Lissu asimame hapa, ipigwe dakika 90… nyie Tarakea mnasemaje?” amesema Heche.
Amesema wanahitaji mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili Rais Samia ashindane na Lissu kwenye uchaguzi mkuu.
Heche amesema hawawezi kwenda kwenye uchaguzi ambao mechi inachezwa kati ya Simba na Yanga halafu muamuzi atoke timu ya Yanga na hicho ni kitu ambacho hakiwezekani.
"Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi ambao mechi inachezwa kati ya Simba na Yanga halafu refa anatoka Yanga, haiwezekani kwenye uchaguzi, inawezekanaje hii kitu? Watu wa Simba mtakubaliana na hii hali.... au mshika kibendera awe Ahmed Ally, outside zote atasema ni magoli... uwongo ukweli,” amehoji.
Heche amesema CCM inataka kuwalazimisha kwenda kwenye mechi ambayo Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ambayo viongozi wake wanateuliwa na Rais ndiyo iamue matokeo ya uchaguzi, jambo alilosema si sahihi.
Wakati huohuo, Heche amesema hakuna kitu chenye thamani duniani kama uhai wa mtu na kunahitajika mabadiliko nchini ili kuhakikisha wananchi wanafikiwa na maendeleo.
"Mimi nimetoa maisha yangu sadaka kubadilisha nchi hii, sitakimbia nchi hii, nitasimama imara. Ndugu zangu tuko kwenye wakati mbaya tumekuja kwenu kuwaomba mtuunge mkono kwani, kuna muda wa kutosha kufanya mabadiliko.
"Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi ambao mechi inachezwa simba na yanga halafu refa anatoka Yanga wafanye mabadiliko kwanza ndipo tuingie kwenye uchaguzi.
“Mimi naogopaje uchaguzi, nimekuwa diwani nikiwa chuo kikuu leo namuogopa nani? Nimekuwa mbunge, nachohitaji ni viwanja vya kutosha watu washindane kwa haki,” amesema Heche.
Pia, amewataka vijana watambue kuwa mabadiliko ni kwa ajili yao katika kuhakikisha wanakuwa na maisha mazuri na yenye ustawi.
"Tunahitaji mabadiliko, vijana mabadiliko duniani ni kwa ajili yenu, mabadiliko ni kwa ajili ya vijana, tuungeni mkono, leo tunaagiza ngano nje wakati mwalimu Nyerere (Julius) aliacha mashamba. Tunachohitaji vijana wa Rombo ni kupewa mashamba, mpewe trekta na mpewe masoko muingie shambani mlime mtajirike,” amesema.
Heche amesema Rombo wanalima parachichi kwa wingi, eneo hilo lilihitaji kuwa na kiwanda ili kuliongezea thamani zao hilo.
“Kiwanda kikiwekwa hapa kitatupatia faida nyingi ikiwamo upatikanaji wa ajira na kuongeza upatikanaji wa kipato na kukuza uchumi,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema, Deogratius Mahinyila amesema vijana wengi wa wanaomaliza vyuo vikuu wana changamoto ya ajira hali ambayo imewafanya baadhi yao kuchanganyikiwa.
Amesema baadhi ya wazazi wamepambana kuuza kahawa na mikungu ya ndizi ili kuwasomesha vijana wao, lakini wapo mtaani hawana ajira.
"Tumekuwa na Taifa ambalo kila mtu amechanganyikiwa, sisi vijana tumechanganyikiwa kwa ukosefu wa ajira, wazazi wetu nao wamechanganyikiwa, vijana wakimaliza vyuo vikuu hawana ajira,” amesema Mahinyila.
Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel amesema wananchi wanaoishi mpakani mwa Kenya na Tanzania eneo la Tarakea, wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano ya simu kutokana na mwingiliano wa mawasiliano na nchi jirani.
"Wananchi wa eneo hili wapo mpakani hapa na Kenya kuna mwingiliano mkubwa wa mtandao wa Kenya na Tanzania hapa, jambo linalowaletea bugdha kubwa mno na shida ya mawasiliano kwenye eneo hili,"amesema Welwel.