Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema kupeleka operesheni No reforms, no election Kaskazini

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel.

Muktasari:

  • Baada ya operesheni hiyo kumalizika katika mikoa ya kanda ya Ziwa iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, sasa inahamia mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuanzia kesho Mei 28 hadi Juni Mosi, 2025

Arusha. Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), kimepanga kuanza operesheni ya No reforms, no election ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’ katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuanzia kesho Mei 28, 2025.

Operesheni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa kesho Mei 28,2025 katika viwanja vya Kilombero jijini Arusha.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Samwel Welwel amesema uzinduzi huo kesho utaongozwa na Makamu Mwenyekiti bara, John Heche na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika.

Amesema operesheni hiyo itakayoanzia Mkoa wa Arusha itafanyika katika mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na kuhitimishwa mkoani Tanga Juni Mosi, 2025.

Amewataja viongozi wengine watakaokuwepo katika uzinduzi huo ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Wilbroad Slaa  na viongozi wengine wakiwemo wajumbe wa kamati kuu.

“Kesho tunaanza uzinduzi eneo la Kilombero, Mei 29 tutakuwa na mikutano ya barabarani Kikatiti, Kisongo na Mto wa Mbu (Monduli). Siku hiyo ya Mei 29, tutakuwa na mkutano wa hadhara eneo la Mirerani (Simanjiro) na Karatu tutakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara.”

Mwenyekiti huyo amesema mkutano wa Karatu utaongozwa na Mnyika na  Dk Slaa na kuwa mikutano mingine itaendelea mkoani Kilimanjaro na Tanga kuanzia Mei 29,2025 hadi Juni Mosi.

“Tunaanza na mikutano mitatu ikiwemo maeneo la Useri na Tarakea wilayani Rombo ila uzinduzi ni kesho Arusha Mjini (Viwanja vya Kilombero),”amesema

“Na kuanzia Mei 29,2025 watagawanyika makundi mawili kundi moja litaongozwa na Heche na lingine litaongozwa na Mnyika ambao watagawana maeneo na kushirikiana na viongozi wengine. Tukimaliza kanda hii inafuata Kanda ya Kati,”ameongeza.

Operesheni hiyo ilianza  mwaka huu ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, ambaye kwa sasa yuko mahabusu ambapo anakabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya uhaini ambayo haina dhamana.

Operesheni hiyo ilianza Mei 8, 2025 kanda ya Victoria yenye mikoa ya Mwanza, Kagera na Geita ambayo ilimalizika Mei 17, 2025 kwenye kanda ya Serengeti iliyojumlisha mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walijigawa kwenye makundi mawili ambapo pamoja na kunadi sera zake, walitumia mikutano yao ya hadhara kutoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa chama hicho kutoingia kwenye uchaguzi bila mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaoweka sawa wanja wa siasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa.