Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Mapigo’ saba yanayoikabili Chadema baada ya ‘No reforms, No election’

Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika (aliyesimama) akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kamati kuu ya chama hicho, inayoanza leo na kuhitimishwa kesho jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Baadhi ya mambo hayo ni kupingwa kwa uamuzi wa baraza kuu wa kuwapitisha wajumbe wa sekretarieti na kutengenezwa dhana potofu kuwa ndani ya chama hicho, kuna mpasuko, mgogoro, usaliti, uasi na hujuma.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaja mambo saba yanayokikabili ikiwa ni vita inayopigwa dhidi ya ajenda yake ya kuzuia uchaguzi iwapo hakutafanyika mabadiliko ‘No reforms, No election.’

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, baadhi ya mambo hayo ni kupingwa kwa uamuzi wa baraza kuu wa kuwapitisha wajumbe wa sekretarieti na kutengenezwa dhana potofu kuwa ndani ya chama hicho, kuna mpasuko, mgogoro, usaliti, uasi na hujuma.

Wakati Mnyika akiyasema hayo, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche amefafanua kuwa hakuna mgogoro ndani ya chama hicho na hata idadi ya waliohama ni ndogo, isipokuwa kuna nguvu inayotumika kusukuma taarifa kuwa chama hicho kiko taabani.

Mnyika ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Mei 23, 2025 alipozungumza kumkaribisha Heche kabla ya kuanza kwa kikao cha kamati kuu ya chama hicho, inayoanza leo na kuhitimishwa kesho jijini Dar es Salaam.

Amesema chama hicho kinakabiliwa na kile alichokiita mapigo saba kutoka kwa watawala, ikiwemo lile la kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoitambua sekretarieti ya Chadema.

Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwa katika kikao cha kamati kuu ya chama hicho, inayoanza leo na kuhitimishwa kesho jijini Dar es Salaam.

“Watawala wanakipiga vita Chadema na kupinga uamuzi wa kikao cha baraza la Januari 22, 2025 dhidi ya uteuzi wa Katibu Mkuu na wasaidizi wake, wakiwa na nia ovu ya kubatilisha uamuzi wa baraza kuu uliofanyika mara baada ya uongozi mpya kuingia madarakani. Hili ni pigo la kwanza ambalo watawala wanaipiga Chadema,” amesema.

Pigo lingine kwa mujibu wa Mnyika, kutumiwa kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohammed na wenzake kufungua kesi ya kutaka kuzuiwa kwa shughuli za chama nchi nzima.

“Wamejaribu pigo la tatu la kumkamata Mwenyekiti wa chama (Tundu Lissu) na kumweka ndani ili kukwamisha mapambano ya no reforms no election,” amesema.

Mnyika amesema pigo lingine ni kutengenezwa dhana potofu kuwa ndani ya chama hicho, kuna mpasuko, mgogoro, usaliti, uasi, hujuma na mambo mengine ikiwa ni mbinu ya kuendesha mapambano dhidi ya ajenda ya No reforms, no election.

“Wanaendesha dhana ambayo iko kinyume na katiba kwamba hata mabadiliko yakipatika, Chadema haiwezi kushiriki uchaguzi hadi baada ya miaka mitano kwa kile kinachoitwa Katibu Mkuu kutokusaini kanuni za maadili ya uchaguzi,” amesema.

Kadhalika, amesema kuna hujuma dhidi ya mikakati na mifumo ya chama hicho, kukusanya rasilimali zake, huku akiwasihi Watanzania waendelee kukichangia.

Pigo aliloliita la saba, amesema ni kutengenezwa vyama mbadala viwili vya siasa kuziba nafasi ya Chadema kwa kuwa ipo karibu kuiondoa CCM madarakani.

“Mapigano yote saba yanalenga kuipiga vita ‘no reforms no election’ na vita ya urais. Ni imani yangu chini ya uongozi wenu, vita hii tutaishinda na mapigano yote tutayashinda,” amesema.

Sambamba na hayo, Mnyika amewaeleza wajumbe wa kamati kuu kuhusu kupokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kubatilisha uamuzi wa baraza kuu.

Kwa kuwa barua hiyo iliwasilishwa akiwa safarini na iligongwa muhuri wa siri, amesema haikuwa imefunguliwa hadi pale aliporudi ofisini.

“Nafahamu kwamba kamati kuu ya chama hamna ufahamu wa maudhui yake kwa ukamilifu zaidi ya taarifa ambazo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilizivujisha kwa uchache kwa baadhi ya vyombo vya habari,” amesema.


Heche apinga mpasuko

Katika hotuba yake, Heche amesema kumekuwepo kelele za kuonyesha chama hicho kimepasuka, zinazofanywa kupitia vyombo vya habari, akidai kuna msukumo nyuma ya hilo.

“Kwa sababu haiwezekani taarifa moja unakuta imeandikwa na gazeti moja inafanana na jingine na jingine na jingine, luninga zimeripoti taarifa zote zinafanana unajua hii ni kanyaboya,” amesema.

Kabla ya kusema chama hicho kimepasuka, amesema ni vema wanahabari wafanye utafiti, akifafanua wajumbe wa kamati kuu ndio Chadema yenyewe na aliyeondoka ni mmoja sawa na asilimia mbili.

“Chadema ni kamati kuu na kati ya wajumbe wote wa kamati kuu ameondoka mjumbe mmoja ambaye kwa asilimia ni mbili kati ya wajumbe wote. Baraza kuu lina wajumbe 456, walioondoka ni 20,” amesema.

Baadhi ya viongozi wa Chadema wakiwa katika kikao cha kamati kuu ya chama hicho, inayoanza leo na kuhitimishwa kesho jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa wajumbe wa mkutano mkuu ambao kwa ujumla wake ni 1,194, amesema walioondoka ni 34 ambayo ni sawa na asilimia nne.

Amesema katika ziara walizotembelea kanda mbalimbali, maelfu ya Watanzania wamejitokeza kuwalaki, kuwachangia na kuunga mkono ajenda yao.

“Chama kiko imara, kimetulia na kinachapa kazi, walioondoka tunawatakia safari njema, tukutane kazini na kuanzia keshokutwa tutakuwa barabarani tena kukutana na wananchi wa kanda inayofuata,” amesema.

Katika hotuba yake hiyo, amesema ni ajabu kusikia taarifa kuwa chama hicho kimepoteza wanachama 3,000 akitaka Watanzania walitafakari hilo.

“Je, tunachokipigania ni cha kweli kwenye ajenda ya ‘no reforms no election’? Ni kweli. Je, uchaguzi wa nchi hii unaibiwa? Ni kweli unaibiwa, kwenye uchaguzi wa nchi hii watu wanauawa? Ni kweli, watu wanauawa ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa, waliuawa wawili,” amesema.

Kwa sababu mambo hayo yote yana ukweli, amesema nini wanapaswa kufanya kati ya kukubali siasa za ulaghai kwa ahadi ya kugawiwa majimbo au kusimamia msimamo wa kuiondoa nchi kwenye mikono ya wale aliowaita mafisadi.

“Msimamo wa chama chetu ni kusimama na msimamo wa wananchi na kutofanya siasa za ulaghai, tumekataa siasa za ulaghai. Kwa hiyo nilitaka muwafikishie Watanzania huo ujumbe kwamba Chadema sio chama cha kufanya siasa za janjajanja, siasa za uongo uongo, siasa za ulaghai, tunapitia njia ngumu na tutashinda,” amesema.

Amesema chama hicho kimeamua kishirikiane na Watanzania, kuhakikisha nguvu yao ya kuamua nani awe kiongozi ili awajibike kwao inarudishwa.