Lissu, Serikali kutoana jasho tena leo mahakamani

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Muktasari:
- Lissu anakabiliwa na kesi mbili, ambazo zote zimepangwa leo kwa hatua tofautitofauti. Mara zote kesi hizo zinapotajwa kumekuwa na mvutano mkali wa hoja baina ya pande zote mbili.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu leo Jumatatu Juni 16, 2025, anapandishwa tena kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, katika kesi mbili tofauti zinazomkabili, mahakamani hapo.
Lissu anakabiliwa na kesi ya uhaini pamoja na kesi kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni.
Kesi hizo ambazo zinasikilizwa na mahakimu wawili tofauti zote zimepangwa kuendelea leo lakini katika hatua tofautitofauti.
Wakati kesi ya uhaini leo inatajwa kwa ajili ya Serikali kutoa mrejesho wa hatima ya upelelezi ulikofikia, kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo imepangwa kwa ajili ya kuanza usikilizwaji rasmi, yaani Mahakama kuanza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo kuanza kwa usikilizwaji wa kesi hiyo leo kunategemea na mrejesho wa hatima ya shauri dogo la maombi lililofunguliwa na Jamhuri kuhusiana na ulinzi wa mashahidi wake wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.
Kesi ya uhaini
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mafawidhi wa mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Anadaiwa kuwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Juni 2, 2025, upande wa mashtaka uliieleza Mahakama kuwa jalada la upelelezi lilikuwa limeshawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), lakini baada ya DPP kulipitia alibainisha kuwa kuna jambo ambalo bado lilikuwa halijakaa sawa hivyo alilirejesha tena kwa wapelelezi kufanyia kazi eneo hilo.
Kutokana na taarifa hiyo, kiongozi wa Jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga aliomba Mahakama itoe ahirisho mpaka tarehe nyingine.
Japo hoja hiyo ilipingwa vikali na jopo la mawakili wa Lissu; Mpale Mpoki (kiongozi wa jopo), Dk Rugemeleza Nshala, Peter Kibatala, Jeremiah Mtobesya, Jebra Kambole na Hekima Mwasipu, wakiiomba Mahakama iifute kesi hiyo, lakini Mahakama ilikubali hoja na maombi ya upande wa mashtaka.
Hakimu Kiswaga alisema kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachoipa Mahakama mamlaka kuifuta kesi iliyo katika hatua ya uchunguzi wa awali kwa sababu tu ya upelelezi kuchelewa kukamilika.
Hivyo aliahirisha kesi hiyo mpaka leo, huku akiuelekeza upande wa mashtaka kuja kutoa taarifa ya mahali upelelezi huo ulikofikia.
Kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo
Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu.
Katika mashtaka hayo yote anadaiwa ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa Youtube, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.
Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.
Pia, anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa Jumatatu Juni 2, 2025, yaani upande wa mashtaka kuanza kuwasilisha ushahidi wake kupitia mashahidi wake hao.
Hata hivyo upande wa mashtaka uliwasilisha maombi ya ulinzi kwa mashahidi wake hao, ukiomba yasikilizwe upande mmoja, bila kuwahusisha upande wa utetezi.
Kutokana na kuwepo kwa maombi hayo upande wa mashtaka uliiomba Mahakama iahirishe usikilizwaji wa kesi hiyo kwanza kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi hayo.
Wakili Katuga aliieleza mahakama kuwa uamuzi wa maombi hayo unaweza kuathiri mwenendo wa usikilizwaji wa kesi hiyo, na kwamba ndio utatoa mwangaza namna ya kuendelea na kesi hiyo kulingana na mazingira yake.
Maombi hayo yalipingwa vikali na jopo la mawakili wa Lissu, pamoja mambo mengine wakidai kuwa upande wa mashtaka haujaweza kutoa taarifa za msingi kuwezesha Mahakama kuahirisha kesi hiyo.
Wamesema kuwa upande wa mashtaka haukasema kama katika maombi hayo unaomba ulinzi kwa mashahidi wake wote 15 au ni wachache.
Hivyo uliomba kama ulinzi huo hauhusishi mashahidi wote basi mahakama iendelee na usikilizwaji kwa mashahidi wengine.
Hakimu Mhini katika uamuzi wake alikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo, akisema kuwa ameona kuwa kuna sababu za msingi kuahirisha kesi hiyo ili kupisha usikilizwaji wa maombi ya Jamhuri.
Hivyo aliahirisha kesi hiyo mpaka leo Juni 16, 2025 itakapoendelea kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi huo baada ya maombi hayo ya Jamhuri kuamuriwa.