Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mnyukano wa kisheria kortini

Muktasari:

  • Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam.  Upande wa mashtaka katika kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo mitandaoni inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, umewasilisha maombi ya kupewa ulinzi kwa mashahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Maombi hayo yakikubaliwa, mashahidi hao watatoa ushahidi bila kuonekana hadharani.

Hata hivyo, jopo la mawakili wanaomtetea Lissu limepinga maombi hayo huku mmoja wa mawakili wa jopo hilo,  Peter Kibatala, akiibua jambo kuwa, wanajua upande wa mashtaka unaogopa aibu ambayo mashahidi wake hao wataipata baada ya kutoa ushahidi wao.

Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa YouTube, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao Na. 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Jopo la mawakili wa Lissu wakiwa ndani ya Mahakama ya Kisutu kabla ya kesi kuanza kusikilizwa. Picha na Ally Mlanzi

Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.

Upande wa mashtaka umeeleza kuwa unatarajia kuwaita mashahidi 15 na kuwasilisha vielelezo kadhaa kuthibitisha madai yao.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa leo Jumatatu Juni 2, 2025, yaani upande wa mashtaka kuanza kuwasilisha ushahidi wake kupitia mashahidi wake hao.

Hata hivyo, upande wa mashtaka umewasilisha maombi ya ulinzi kwa mashahidi wake hao, ukiomba yasikilizwe upande mmoja, bila kuwahusIsha upande wa utetezi.

Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ameieleza Mahakama kuwa, uamuzi wa maombi hayo unaweza kuathiri mwenendo wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

"Hivyo chini ya kifungu cha 225(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), tunaomba Mahakama iahirishe  shauri hili ili kutoa nafasi maombi haya ya jamhuri yaweze kusikilizwa na kutolewa uamuzi," amesema Wakili Katuga.

"Uamuzi huu utakuwa umetupa mwangaza wa jinsi gani kuendelea kwenye shauri hili kulingana na mazingira. Hivyo, tunaona ni busara Mahakama kutoa aahirisho ili tuweze kusubiri uamuzi wa Mahakama."

Maombi hayo yamepingwa vikali na jopo la mawakili wa Lissu likiongozwa na Wakili Mpale Mpoki, likidai kuwa, upande wa mashtaka haujaweza kutoa taarifa za msingi kuwezesha Mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Limedai kuwa, hawakusema kama katika maombi hayo, wanaomba ulinzi kwa mashahidi wake wote 15 au wachache.

Hivyo, limeomba kama ulinzi huo hauhusishi mashahidi wote, Mahakama iendelee na usikilizwaji kwa mashahidi wengine.

Akijibu maombi hayo, Wakili Peter Kibatala amesema wanajua kuwa sababu ya jamhuri kutaka mashahidi wake wafichwe ni kwa kuwa watawagaragaza.

"Hizi proceedings ( mwenendo) ziko live na kila mtu ataona, kwa hiyo wanaogopa mashahidi wao hasa polisi maana tutawagaragaza hapa,"amesema Kibatala.

Mawakili hao wa utetezi wamesema kama maombi hayo yanahusu ulinzi kwa mashahidi wote, basi hapo kutakuwa na ukiukwaji wa haki za mteja wao kinyume na Ibara ya 13 ya Katiba kuhusu usawa katika usikilizwaji.

Wamesisitiza kuwa, mshtakiwa ana haki ya kumjua shahidi na nyaraka anazozipia katika ushahidi wake.

Hivyo, wameiomba Mahakama hiyo ipeleke shauri hilo Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Mpoki ameieleza Mahakama kuwa,  hawadhani upande wa mashtaka hauna nia ya dhati ya kuendelea na kesi hiyo, akidai wangeweza kuendelea na mashahidi wengine ambao hawahitaji ulinzi.

Hivyo, amesema wanapinga maombi hayo ya kuahirishwa.

Wakili Dk Rugemeleza Nshala ameiambia Mahakama kuwa, mambo yanayoendelea katika kesi hiyo kwa mtu anayeyasikiliza, atakuwa na taswira mbaya akidai kuna mambo Serikali inataka kuyaficha.

Hata hivyo, Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake, amekubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

"Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, nimeona kuwa kuna sababu za msingi kuahirisha kesi hii ili kupisha usikilizwaji wa maombi ya jamhuri," amesema Hakimu Mhini.

Hivyo, ameiahirisha kesi hiyo mpaka Juni 16, 2025 itakapoendelea kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi huo baada ya maombi hayo ya jamhuri kuamuriwa.

Katika kesi hiyo, kwa shtaka la kwanza, Lissu anadaiwa kutamka kuwa: “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa kwa maelekezo ya Rais," wakati akijua maneno hayo ni ya uwongo na ya kupotosha umma.

Shtaka la pili anadaiwa kuwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa za uwongo na za kupotosha umma kuwa: "Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi.”

Katika shtaka la tatu mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa siku hiyoh iyo alichapisha taarifa kuwa: "Majaji ni MA-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.”

Lissu aonywa No reforms, wafuasi no election

Awali mahakamani hapo, Lissu alizua jambo baada ya kutamka kaulimbiu ya chama hicho kupinga uchaguzi ya ‘No reforms, no election’ akiwa kizimbani mbele ya hakimu na kusababisha Mahakama hiyo kumpa onyo.

Lissu alitamka, “No reforms,” na wafuasi kuitikia “No election,” baada kupanda kizimbani katika kesi ya uhaini inayomkabili.

“Hata walioitikia hawakuwa sahihi kwa sababu baada ya Mahakama kukaa hakuna mwingine ambaye anapaswa kuongea. Kwa hiyo kilichofanyika si sahihi na ninatoa onyo si tu kwa mshtakiwa bali kwa mtu yeyote,” amesema Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga.

Lissu anakabiliwa pia na kesi ya uhani katika Mahakama hiyo.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.

Anadaiwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi mkuu wa Serikali ya Tanzania, akidaiwa kutamka kuwa: "Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...kwa hiyo tunaenda kukinukisha...sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli... tunaenda kukinukisha vibaya sana..."

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akiwa ndani ya chumba cha mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Ally Mlanzi

Kesi hiyo imetajwa leo Jumatatu, kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umeshakamilika na kama bado upande wa mashtaka ueleze mahali ulikofikia.

Hata hivyo, ulisema upelelezi badi haujakamilika.