Prime
Lissu, wafuasi waonywa kutaja ‘No reforms, no election’ mahakamani

Muktasari:
- Lissu, Mwenyekiti wa Chadema anakabiliwa na kesi mbili za jinai, ikiwemo ya uhaini inayotajwa leo. Akiwa kizimbani akatamka kauli ya no reforms, no election, jambo lililoibua mvutano baada ya Jamhuri kuiomba Mahakama imchukulie hatua kwa kosa la kuidharau Mahakama.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amezua jambo baada ya kutamka kaulimbiu ya chama hicho kupinga uchaguzi ya ‘No reforms, no election’ akiwa kizimbani mbele ya hakimu na kusababisha Mahakama hiyo kumpa onyo.
Lissu ametamka kaulimbiu hiyo baada kupanda kizimbani katika kesi ya uhaini inayomkabili, leo Jumatatu, Juni 2, 2025, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Lissu anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shitaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Anadaiwa siku hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania, akidaiwa kutamka kuwa:
"Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli...kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko...kwa hiyo tunaenda kukinukisha...sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli..., tunaenda kukinukisha vibaya sana..."
Kesi hiyo imetajwa leo Jumatatu, kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi umeshakamilika na kama bado upande wa mashitaka kueleza mahali ulikofikia.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akiwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Lissu amepanda kizimbani baada ya Hakimu Kiswaga kuwa ameingia mahakamani na kukaa kwenye kiti chake tayari kuendelea na kesi hiyo.
Baada ya kupanda kizimbani tu akawasalimia wanachama na wafuasi wa chama hicho kwa kaulimbiu hiyo kwa kuwa ‘No reforms’ nao wakiitikia kwa pamoja kwa sauti kubwa ‘No election.’
Kutoka na mwenendo huo, upande wa mashitaka umeiomba Mahakama iangalie na kuchukua hatua dhidi ya Lissu kwa madai ametenda kosa la kidharau Mahakama.
Mawakili wa utetezi wanaomtetea Lissu wakipinga hoja za upande wa mashitaka, kuwa licha ya hakimu kuingia mahakamani lakini kesi ilikuwa haijaanza na kwamba kusema maneno hayo hajatenda kosa.
Hata hivyo, Hakimu Kiswaga katika uamuzi wake amekubaliana na hoja za upande wa mashitaka akisema kilichofanywa na mshtakiwa huyo na wale walioitikia ni kosa na kwamba anatoka onyo kwa mshtakiwa huyo na watu wengine wote.
Hakimu Kiswaga amesema kwa mujibu wa kifungu cha 6(1) (c) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu Mahakama inakamilika pale ambapo anakuwepo Hakimu Mkazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi au Hakimu wa Wilaya kwa Mahakama za Wilaya au Mahakama za Mwanzo.
“Hivyo niseme Hakimu anapofika mahakamani Mahakama inakuwa imekamilika na maneno aliyasema mshtakiwa hayakuwa sahihi kwa sababu tayari Mahakama ilishakamilika," amesema Hakimu Kiswaga.
“Hata walioitikia hawakuwa sahihi kwa sababu baada ya Mahakama kukaa hakuna mwingine ambaye anapaswa kuongea. Kwa hiyo kilichofanyika si sahihi na ninatoa onyo si tu kwa mshtakiwa bali kwa mtu yeyote."
Amewataka mawakili wa pande zote ambao ni maofisa wa Mahakama kuhakikisha wanasimamia hilo.
Hakimu Kiswaga amesisitiza Mahakama inapaswa kuongozwa na sheria na si sahihi kufanya yale yaliyotokea kwa sababu mshtakiwa alichelewa kuingia mahakamani.
Amesema kwa kuwa Mahakama inakamilika pale anapokuwepo Hakimu basi shauri linaanzia kuitwa pale Hakimu anapofika, hivyo huku akielekeza kuwa kwa kuwa mshtakiwa ana kesi zaidi ya moja basi hata tarehe ijayo shauri litaitwa kwanza ndipo mshtakiwa ataingia.
Katika hatua nyingine Hakimu Kiswaga amekataa hoja na maombi ya upande wa utetezi kutaka iifute kesi hiyo na kumwachilia huru Lissu, kutokana na upande wa mashitaka kutokukamilisha upelelezi mpaka sasa.
Hakimu Kiswaga amekubaliana na hoja za upande wa mashitaka akisema Mahakama inapofanya uchunguzi wa awali wa shauri lolote haina mamlaka juu ya shauri hilo.
Amesema kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kilichorejewa na upande wa utetezi hakisemi upelelezi ukichelewa kesi inafutwa.
Amesema kifungu cha 131 kinataka kesi ifunguliwe baada ya upelelezi lakini kifungu kidogo cha (1) kinaweka mazingira kwa makosa makubwa yanayosikilizwa na Mahakama Kuu (likiwemo uhaini) Jamhuri inaweza alifungua kesi hata kabla ya upelelezi kukamilika.
Amesema hivyo Mahakama haiwezi kufuta kesi hiyo kwa sababu ya upelelezi kutokamilika lakini, Mahakama inaendelea kuuelekeza upande wa mashitaka kuendelea kutoa taarifa za maendeleo ya upelelezi.
Amesema kwa kuwa Jamhuri wamesema upelelezi umefikia hatua ya mwisho basi tarehe ijayo waendelee kutoa taarifa ulikofikia.
Amesisitiza pande zote zihakikishe shauri hilo linaendeshwa kwa mujibu wa sheria na si mihemko.
Hivyo ameiahirisha kesi hiyo mpaka Juni 16, itakapotajwa.
Jopo la waendesha mashitaka katika kesi hiyo linaongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga huku Lissu aliwakilishwa na jopo la mawakili 30, linaloongozwa na Wakili Mpale Mpoki.