Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tukitaka elimu bora tuanze kwa walimu

Muktasari:

Taifa ambalo watu wake wameelimika, wanaweza kuvuna, kutumia na kulinda rasilimali zake za asili na rasilimali watu katika kujiletea maendeleo endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Ni dhahiri kwamba ili taifa liweze kupiga hatua ya kimaendeleo katika nyanja zote, elimu ni jambo la muhimu.

Taifa ambalo watu wake wameelimika, wanaweza kuvuna, kutumia na kulinda rasilimali zake za asili na rasilimali watu katika kujiletea maendeleo endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Katika utoaji na upatikanaji wa elimu iliyo bora, sahihi na kwa usawa, wadau wakubwa ni Serikali, wazazi, walimu na wanafunzi.

Serikali ina jukumu la kuhakikisha kwamba kunakuwapo mazingira bora ya kupatia elimu kwa maana ya kutenga bajeti inayojitosheleza kwa ajili kuendesha shughuli zote za utoaji wa elimu katika ngazi zote.

Bajeti hiyo pamoja na mengineyo, kimsingi ilenge katika kuhakikisha upatikanaji wa vyumba bora vya madarasa vinavyokidhi mazingira safi na rafiki ya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya kujifunza na kufundishia kwa ujumla wake, vyumba vya kisasa vya maabara pamoja na vifaa vyake.

Jambo linalotia shaka hivi sasa ni suala la ubora wa elimu inayotolewa katika shule zetu hasa shule za umma. Elimu bora ni ile inayomsaidia mnufaika katika ngazi husika aweze kupambana na mazingira mara baada ya kuhitimu, na kuweza kujitegemea huku akitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Kwa kiasi kikubwa tunaweza kuona tofauti kubwa kati ya kwenda shule na kupata elimu. Kinachotokea sasa ni wimbi kubwa la vijana kuhudhuria shule na sio kupata elimu ambayo itawasaidia kupambana na hali halisi ya maisha ya kila siku na kuiletea nchi maendeleo endelevu yanayotarajiwa. Akili za wanafunzi wengi zipo katika kuajiriwa na sio kujiajri au kutengeneza ajira.

Katika hili tunapaswa kukaa chini na kujitafakari kuwa je, tunataka kuwafurahisha wananchi kuona kuwa watoto wao au watoto wetu wanakwenda shuleni bila kujua hatima yao? Suala hili linahitaji mjadala mpana wa kitaifa na sio maamuzi ya mtu mmoja au kikundi cha watu fulani ikiwa tunataka Tanzania mpya kufikia mwaka 2025.

Tunahitaji kuangalia upya na kuwa na mfumo imara wa mafunzo kwa walimu. Kwa sasa tunashuhudia mabadiliko kadhaa hasa katika mafunzo ya ualimu katika ngazi ya astashahada na stashahada, mabadiliko haya yanaliweka Taifa njia panda.

Naamini kwamba tukiwa na mfumo imara wa kuwapata watu watakaokuwa walimu ambao watatoa elimu kwa vijana wetu, tutakuwa na wasomi ambao wana tija kwa taifa letu. Ili kufikia malengo haya lazima Serikali ikubali kuwa ipo haja ya kuleta mezani mjadala juu ya kuwa na mtaalaa wa elimu ya Tanzania ambao ni imara na endelevu usioyumbishwa na maamuzi ya kisiasa, bali maamuzi ya kitaaluma yanayozingatia utafiti.

Katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata elimu bora, suala la walimu limekua likipuuzwa na kutojadiliwa. Walimu wamekuwa waathirika wa ahadi hewa, huku wakilaumiwa pindi matokeo ya wanafunzi yanapokuwa mabaya.

Ni vyema Serikali, wazazi, walezi na wadau wote wa elimu wakatambua kwamba kazi ya ualimu siyo kazi ya kufyatua matofali, ambayo ufanisi wake unapimwa kwa idadi ya mifuko ya saruji, ndoo za mchanga, lita za ujazo wa maji vilivyotumika ili kuzalisha matofali yaliyopo.

Kazi ya ualimu ni taaluma ambayo inahusu shughuli ya kisaikolojia, kitaalamu tunasema; “psychological process” Shughuli hii ndiyo inayomtoa mtu katika hali ya ujinga na kuwa na ujuzi au elimu. Mwalimu hawezi kufanya kazi hii iwapo kisaikolojia hana utulivu. Ndio maana wanasaikolojia wanasema ili kujifunza mwanafunzi na mwalimu lazima wawe tayari kisaikolojia na kimwili.

Maslahi ya walimu yanapuuzwa kila kukicha, bado wanalipwa mishahara duni ambayo hailingani hata kidogo na kazi wanayoifanya. Wakati mwingine wanapofanya kazi za nje hulipwa posho kidogo ukilinganisha na kada nyingine za utumishi.

Ingawa Serikali inajitahidi kulipa madai mbalimbali lakini bado tatizo ni kubwa kiasi cha kushusha ari ya ufundishaji. Wakati kada nyingine zikilipwa marupurupu na posho za mazingira magumu, walimu wamekua wakisisitizwa kuwa kazi yao ni wito. Kukopwa imekua kawaida kwa walimu wanapofanya kazi maalumu nje ya vituo vyao vya kazi.

Suala la mazingira magumu ya kufanyia kazi hasa nyumba za walimu limekua ni tatizo sugu na hivyo kuwafanya walimu kukosa ari ya kufundisha kwa moyo. Kutoheshimika kwa taaluma ya ualimu ni tatizo kubwa linaloshusha ubora wa elimu yetu. Licha ya mwalimu kuwawezesha wanataaluma wengine wote kufikia malengo yao, mwalimu amebaki kuwa daraja na kudharauliwa siku zote. Taaluma ya ualimu inaonekana ni taaluma ya watu waliofeli.

Mwandishi ni mwalimu na pia ni mwanafunzi wa shahada ya pili katika masuala ya utawala, sera na mipango Elimu Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania. 0784325447